Tafuta

Papa Francisko amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya katika uwanja wa Lokomotiva huko Kosice na kuwapatia ushauri makini. Papa Francisko amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya katika uwanja wa Lokomotiva huko Kosice na kuwapatia ushauri makini. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Ushauri kwa Vijana!

Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana kuwa na upendo wa dhati unaofumbatwa katika uaminifu, unaopokelewa kama zawadi na kuwajibisha. Upatanisho ni Sakramenti ya furaha. Vijana wajitahidi kukumbatia Msalaba, huku wakiwa wameungana na Kristo Yesu. Upendo unaobubujika kutoka katika Msaba ni nguvu ya Mungu inagonga, kuponya na inayopyaisha maisha ya waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 14 Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba, amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Slovakia, kwenye Uwanja wa Lokomotiva, Jimbo kuu la Košice. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusikiliza shuhuda na maswali mbalimbali ya vijana na hatimaye akawapatia ujumbe ambao wanapaswa kuufanyia kazi katika maisha yao kama vijana. Amewataka vijana kuwa na upendo wa dhati na kamwe wasiangalie mambo ya nje tu yanayoweza kuwadanganya kwa sababu, upendo wa dhati unafumbatwa katika uaminifu, unaopokelewa kama zawadi na unawajibisha. Upatanisho ni Sakramenti ya furaha. Vijana wajitahidi kukumbatia Msalaba, huku wakiwa wameungana na Kristo Yesu. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, awe ni kielelezo cha upendo wa dhati katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Vijana wajenge maisha yao katika ujasiri, daima wakitamani kufikia kilele cha mafanikio na kamwe maisha yasiwe kama maji kwa glasi! Kila mtu ni wa pekee kabisa katika maisha na mbele ya Mwenyezi Mungu.

Vijana wasibakie kuota ndoto ya kupata wenza wazuri na watanashati katika maisha, bali waangalie wenza watakaosaidiana kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani; kwa kuwatunza, kuwalea na kuwaelimisha vyema watoto wao. Kuteleza na kuanguka ni sehemu ya maisha ya ujana, na wala hili lisiwasumbue hata kidogo. Vijana wasipende kujilegeza na kubweteka kwa kuwa na ndoto ya mambo makubwa kama vile magari ya kifahari, “pamba nyepesi ya kufa mtu” au kufanya utalii sehemu mbalimbali za dunia, kuonesha ile jeuri ya fedha! Mambo haya mara nyingi yamewaachia vijana machungu moyoni badala ya kuwapatia furaha ya kweli! Vijana wajitahidi kuwapenda wenzao jinsi walivyo na kamwe wasitake kuwabadilisha na kutaka kuwa kama wao! Wathubutu kupenda bila masharti! Baba Mtakatifu anawashauri vijana kuwa waaminifu katika mila na desturi njema, kielelezo cha mizizi ya utambulisho wao. Wasikubali kuleweshwa na habari za mitandao ya kijamii, bali wajitahidi kuwa na “connection katika maisha.” Mwenyezi Mungu anawataka vijana kuwa na “Connection katika maisha” kwa kuonesha ushirikiano na mshikamano na vijana wengine.

Baba Mtakatifu anasema, changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi kipya ni kujiangalia na kujitafuta wao wenyewe, kwa kuwa na mawazo mgando yasiyotaka mabadiliko. Huu ni ugonjwa unaoweza kuwazeesha vijana haraka sana. Litania ya malalamiko na tabia ya kujikatia tamaa katika maisha ni mambo ambayo hayana nafasi katika utume wa Kanisa. Hawa ni vijana wanaoangalia mabaya kiasi hata cha kushindwa kugundua uzuri unaowazunguka! Vijana wajenge ujasiri wa kuangalia juu na kamwe wasikubali kutembea huku wakiwa wameinamisha kichwa, utadhani kondoo! Sakramenti ya Upatanisho ni mahakama ya upendo na huruma ya Mungu inayomwezesha mwamini kuchunguza dhambi zake, kutubu, kuungamana na kutimiza malipizi, tayari kuanza maisha mapya yanayomwezesha mwamini kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, Kisima cha huruma ya Mungu. Hapa waamini wanaponywa na kupewa neema ya kuendelea na mapambano ya maisha ya kiroho, hadi kuufikia uzima wa milele. Waamini wajenge utamaduni wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kujenga mazoea ya kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Baada ya maungamo, vijana watumie muda kidogo ili kumshukuru Mungu aliyewaondolea dhambi zao! Upatanisho ni Sakramenti ya furaha, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu. Mapadre waungamishaji wawe ni watu wenye huruma na mapendo na kamwe wasiwe ni wadadisi wa kutaka kuchokonoa hata yale yasiyowahusu. Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vinavyotoa: huruma na msamaha wa Mungu. Vijana wasikate tamaa wanapojisikia na kuona aibu ya kwenda kuungama dhambi zao, kwani hata katika hali na mazingira kama haya, Mwenyezi Mungu bado anawapenda na kuwajali jinsi walivyo! Vijana wajenge utamaduni wa kujisamehe wenyewe kwani Mwenyezi Mungu anafurahi kuwaona watu wanaotubu na kumwongokea na anawangalia kama watoto wake wapendwa na wala si kama wadhambi! Sakramenti ya Upatanisho iwe ni chemchemi ya furaha mbinguni na amani duniani.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuambata na kukumbatia Msalaba, ili kuondokana na hofu ili kuweza kujiamini. Vijana wajitahidi kukumbatia Msalaba, huku wakishirikiana na Kristo Yesu na kamwe wasiwe peke yao. Upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba una nguvu ya kuleta mabadiliko yanayosimikwa katika furaha, amani na utulivu hata kama ni katikati ya magumu ya maisha na machungu ya maisha. Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu inawaweza waamini kupata furaha ya maisha! Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha, huruma na mapendo kwa vijana wengine. Wajitahidi kutenda yote haya kwa upendo, takabasamu na urafiki wa udugu wa kibinadamu; daima wakijitahidi kushikamana na kuungana kwa pamoja.

Vijana Slovakia
14 September 2021, 17:56