Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Septemba 2021 amesali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mteso Saba!  Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Septemba 2021 amesali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mteso Saba!  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Sala ya Papa & Maaskofu

Tarehe 15 Septemba 2021, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mateso Saba, Papa meungana pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Slokavia kusali kwenye Madhahabu ya Bikira Maria wa Mateso Saba huko mjini Šaštín, anaheshimiwa sana nchini Slovakia. Kwa mara ya kwanza, kumbukumbu hii kitaifa, imeadhimishwa kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 15 Septemba 2021, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mateso Saba, ameungana pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Slokavia kusali kwenye Madhahabu ya Bikira Maria wa Mateso Saba huko mjini Šaštín. Bikira Maria wa Mateso saba, anaheshimiwa sana nchini Slovakia. Kwa namna ya pekee kabisa, tarehe 15 Septemba 2021 Mama Kanisa ameadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria, Mama wa Mateso saba. Kwa mara ya kwanza, kumbukumbu hii kitaifa, imeadhimishwa kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni Sikukuu ambayo imepata chimbuko lake kunako Karne ya kumi na nne. Kunako Mwaka 1727 Papa Benedikto XIII akaiingiza rasmi kwenye Kalenda ya Kanisa. Mwaka 1913 Papa Pio X akatangaza rasmi kwamba, itakuwa inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Septemba baada ya Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba.  

Hata leo hii, Bikira Maria anawaonesha huruma wale wote wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini, ujinga, njaa, magonjwa sanjari na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na wakuu wa ulimwengu huu. Bikira Maria Mama wa Mateso awe ni faraja kwa wale wanaoteseka; matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo na awe ni chemchemi ya huruma na mapendo kwa wenye huzuni na mahangaiko makubwa. Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia linasema kwamba, kwa hakika, Bikira Maria alimpenda sana Mwanaye wa pekee tangu alipopashwa habari ya kutungwa kwake mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akamsindikiza katika safari ya maisha na utume wake. Bikira Maria alimfuata Mwanaye Mpendwa hata akadiri kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye mpendwa! Baba Mtakatifu Francisko katika sala yake pamoja na Maaskofu Katoliki Slovakia, wamejikabidhi kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Mateso Saba, wakimshukuru Kristo Yesu aliyewajalia upendo wenye huruma. Wanatambua uwepo wake kama ilivyokuwa wakati wa kungojea ujio wa Roho Mtakatifu, alipoungana na Mitume kusali.

Maaskofu wanamkimbilia Bikira Maria Mama wa Kanisa na Mfariji katika furaha na mahangaiko ya maisha na utume wao, ili aweze kuwaangalia kwa macho yenye huruma na kuwafungulia mikono yake, ili aweze kuwakumbatia. Bikira Maria Malkia wa Mitume na Kimbilio la Wakosefu, anatambua fika mapungufu ya Maaskofu kama binadamu na udhaifu wao wa maisha ya kiroho; machungu na magumu wakati wa upweke na kutengwa, kwa mkono wake wa upole aguse, agange na kuponya madonda yao. Baba Mtakatifu na Maaskofu Katoliki wa Slovakia wameukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, wakiyaaminisha maisha yao na yale ya Taifa la Slovakia. Wanapenda kuuaminisha umoja na mshikamano wao kama Maaskofu kwa Bikira Maria. Wanamwomba Bikira Maria ili awaombee neema ya kuwa waaminifu kwa maneno waliyofundishwa na Kristo Yesu ili kwa njia yake pamoja naye na ndani yake waweze kuinuliwa kwenda mbinguni kwa Baba wa milele!

Baba Mtakatifu na Maaskofu wote kwa pamoja wamesali ile Sala kuu ya Baba Yetu kwa kusema: Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama huko mbinguni, utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu kama nasi tunavyowasamehe wale waliotukosea usituache katika vishawishi lakini utuopoe maovuni. Amina. Baba Mtakatifu amehitimisha Sala hii pamoja na Maaskofu Katoliki wa Slovakia kwa kumwomba Mwenyezi Mungu anayelialika Kanisa kutafakari mateso ya Kristo Yesu kwa kuiga mfano wa Bikira Maria. Kwa maombezi yake, awakirimie uwezo wa kufanana na Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu ili hatimaye, waweze kupata neema zake, Yeye anayeishi na kutawala daima na milele, Amina.

Sala na Maaskofu
15 September 2021, 14:52