Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 ameanza hija yake ya 34 ya Kimataifa nchini Hungaria na Slovakia. Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 ameanza hija yake ya 34 ya Kimataifa nchini Hungaria na Slovakia.  (AFP or licensors)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Budapest: Ekaristi Takatifu!

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Hungaria, amemtumia Rais Sergio Mattarella wa Italia, salam na matashi mema, akimshirikisha kuhusu Hija yake ya Kitume huko Budapest, Hungaria ili kufunga rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa linalonogeshwa na kauli mbiu: Visima vyangu vyote vimo kwako. Zab 87:7.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya 34 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Slovakia inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu anafanya hija hii baada ya kuhitimisha kwa Ibada ya Misa Takatifu Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) yaliyozinduliwa na Kardinali Angelo Bagnasco, Jumapili tarehe 5 Septemba 2021 huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu, Ijumaa jioni tarehe 10 Septemba 2021 alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, ili kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wakati wa hija yake ya Kitume nchini Hungaria na Slovakia.

Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea Hungaria, amemtumia Rais Sergio Mattarella wa Italia, salam na matashi mema, akimshirikisha kuhusu Hija yake ya Kitume huko Budapest, Hungaria ili kufunga rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Baadaye ataelekea nchini Slovakia ili kukutana na ndugu zake katika imani pamoja na watu wote wa Mungu nchini Slovakia. Baba Mtakatifu anamtakia Rais Mattarella pamoja na watu wa Mungu nchini Italia katika ujumla wao: amani na utulivu, huku wakiendelea kujikita katika ukarimu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Italia. Baba Mtakatifu katika ujumbe aliomwandikia Rais Zoran Milanović wa Croatia alipokuwa anapita kwenye anga za Croatia amemtakia: heri, baraka, amani na ustawi kwa Taifa hili na kwamba, amemhakikishia sala zake.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kumkirimia afya njema mara baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa kwenye utumbo mpana. Shukrani hizi, atazitoa kwa namna ya pekee wakati atakapotembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Šaštin nchini Slovakia. Waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, unaowawezesha waamini wote kujenga umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Hii ni hija inayojikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Ni hija inayotoa kipaumbele kwa maskini, amana na utajiri wa Kanisa. Baba Mtakatifu ametia nia ya kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu, Hungaria na Slovakia.

Papa Salam
12 September 2021, 07:40