Tafuta

Papa Francisko Kanisa Katoliki litaendeleza majadiliano ya kidini na Wayahudi ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu Papa Francisko Kanisa Katoliki litaendeleza majadiliano ya kidini na Wayahudi ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Majadiliano na Wayahudi

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Septemba 2021 ametembelea Jumuiya ya Wayahudi wanaoishi kwenye Uwanja wa Rybné Námestie mjini Bratislava. Katika hotuba yake amegusia kuhusu: Chuki, uhasama na mauaji ya kimbari wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na Kumbukumbu ya Shoah, Majadiliano ya Kidini na kwamba, kila mwamini anapaswa kuwa ni baraka kwa jirani zake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 13 Septemba 2021 ametembelea Jumuiya ya Wayahudi wanaoishi kwenye Uwanja wa Rybné Námestie mjini Bratislava. Katika hotuba yake amegusia kuhusu: Chuki, uhasama na mauaji ya kimbari wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na Kumbukumbu ya Shoah, Majadiliano ya Kidini na Wayahudi na kwamba, kila mwamini anapaswa kuwa ni baraka kwa jirani zake. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kutembelea eneo hili ambalo lina utajiri mkubwa unaosimikwa katika misingi ya amani, utulivu na umoja wa watu wa Mungu. Hili ni eneo takatifu kwa ajili ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa heshima ya Mungu aliye hai! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wananchi wengi wa Slovakia waliuwawa kikatili, Sinagogi lao linabomolewa kama njia ya kufyekelea mbali uwepo wa Dini ya Kiyahudi jambo ambalo ni kinyume kabisa cha mapenzi ya Mungu.

Haya ni mauaji yaliyomkufuru Mungu na hivyo kushindwa kuheshimu fadhila ya upendo kwa jirani. Kufuru hii inaendelea wakati wowote ule ambao utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu zinasiginwa. Mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi ni fedheha kubwa sana kwa binadamu na ni kwenda kinyume kabisa cha Mungu. Kumbukumbu ya Shoah ni mahali ambapo Wayahudi wanaweza kwenda kuwakumbuka na kuwaombea wapendwa wao. Na Baba Mtakatifu amechukua fursa hii, ili kujiunga nao kufanya kumbukumbu hii, ili hatimaye, kujenga umoja na udugu wa kibinadamu baada ya kuvuka nyakati hizi za giza nene! Uchu wa mali, madaraka na utajiri wa harakaharaka ni mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna baadhi ya watu wanapenda kutumia dini kwa ajili ya mafao yao binafsi au wakati mwingine wanaibeza dini. Ukosefu wa kumbukumbu ya historia iliyopita pamoja na ujinga ni mambo ambayo yanaweza kuwatumbukiza watu katika kinzani, chuki na uhasama. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungaisha nguvu zao ili kulaani mauaji dhidi ya Wayahudi, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Uwanja wa Rybné Námestie mjini Bratislava ni kielelezo cha matumaini, ili kufukuzia mbali giza la kifo na kuwasha mwanga unaopyaisha maisha. Hapa ni mahali ambapo Jumuiya ya Wayahudi imeendelea kubaki licha ya Sinagogi lake kubomolewa. Ni mahali pa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini; mahali ambapo historia ya watu wa Mungu nchini Slovakia inakutana, ili kuendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Kanisa Katoliki linataka kuendeleza majadiliano ya kidini na Wayahudi. Lengo ni kushirikishana mambo msingi yanayowaunganisha waamini wa dini hizi mbili, ili hatimaye, kusonga mbele katika ukweli, uwazi na uaminifu, ili kutakasa kumbukumbu, kuganga na kuponya madonda na hatimaye, kukumbuka mazuri na mema waliyopokea na kutoa kwa jirani zao. Mchakato wa majadiliano ya kidini anasema Baba Mtakatifu ni muhimu sana. Slovakia ni daraja linalowakutanisha watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anawaombea Wayahudi ili waweze kuendeleza wito wao kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama chemchemi ya baraka kwa jirani zao. Ili kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kupendana na kujaliana; waweze kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wote wa Mungu kwa pamoja wawe ni mashuhuda wa amani!

Wayahudi
13 September 2021, 17:20