Tafuta

Papa Francisko wakati akirejea kutoka Slovakia amefanya mahojiano maalum na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Papa Francisko wakati akirejea kutoka Slovakia amefanya mahojiano maalum na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Mahojiano Maalum na Papa

Papa amejibu maswali sita kuhusu: Utambulisho wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Tunu msingi za maisha ya Kikristo; Mwenendo wa afya yake baada kufanyiwa upasuaji mkubwa; Ekaristi Takatifu na wanasiasa wanaoshabikia utamaduni wa kifo. Maswali mengine yamehusu ubaguzi na mauaji dhidi ya Wayahudi pamoja na Ndoa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya 34 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Slovakia kuanzia tarehe 12-15 Septemba, imenogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu amefanya hija hii baada ya kuhitimisha kwa Ibada ya Misa Takatifu Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) kuanzia tarehe 5 hadi 12 Septemba 2021 huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu alipowasili mjini Roma, moja kwa moja alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ili kumshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya kimama wakati wote wa hija yake ya kitume huko nchini Hungaria na Slovakia. Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea kutoka katika hija yake ya kitume, kama kawaida amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Amejibu kwa ufasaha maswali sita kuhusu: Utambulisho wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Tunu msingi za maisha ya Kikristo; Mwenendo wa afya yake baada kufanyiwa upasuaji mkubwa; Ekaristi Takatifu na wanasiasa wanaoshabikia utamaduni wa kifo.

Maswali mengine yamehusu ubaguzi na mauaji dhidi ya Wayahudi pamoja na Sakramenti ya Ndoa! Baba Mtakatifu anasema, mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU hapo tarehe 25 Machi 1957, walijiwekea sera na mikakati ya kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, lakini hasa kwa kuwekeza katika ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu. Waasisi walitaka kulinda na kudumisha uhai, udugu na haki, kama chachu muhimu sana ya mabadiliko Barani Ulaya, baada ya patashika nguo kuchanika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Waasisi wa Umoja wa Ulaya, EU walikazia kwa namna ya pekee zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Jumuiya ya Ulaya itaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama itaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inapaswa kushughulikia masilahi mapana zaidi kuliko kujielekeza kwenye masuala ya fedha na uchumi peke yake. Hii ni changamoto ya kuzama kwenye asili ya Umoja huu, ili hatimaye, kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya nchi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya zinataka kutumia Umoja huu kama fursa ya kupandikiza ukoloni wa kiitikadi, jambo ambalo ni hatari sana na linakwenda kinyume cha mawazo ya waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hija yake nchini Hungaria ilipokelewa kwa hisia tofauti sana kutokana na ufinyu wa muda alioutumia nchini humo, ikilinganishwa na nchi jirani la Slovakia. Lakini, huu ndio uliokuwa utaratibu uliopangwa tangu awali. Katika mazungumzo yake na viongozi wa Hungaria, wamepanga, ikiwa kama mambo yatakwenda vyema, aweze kuitembelea Hungaria mwaka 2022. Baba Mtakatifu ameguswa kwa namna ya pekee kabisa na mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Ni hija iliyotoa kipaumbele kwa maskini, amana na utajiri wa Kanisa.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema ni wajibu wa kimaadili kwa makampuni ya dawa, mawakala na watengenezaji wa dawa za Serikali kuhakikisha kwamba, wanazalisha, wanaidhinisha, kugawa na kutoa chanjo ambazo zinakubalika kimaadili na kiutu, ambazo kimsingi hazisababishi matatizo kwenye dhamiri za watu. Ikumbukwe kwamba, kimsingi chanjo si kanuni wala jambo la lazima kimaadili, bali linapaswa kuwa ni hiyari ya mtu mwenyewe na inapasa kuzingatia mafao na ustawi wa wengi katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Chanjo itoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuchanjwa chanjo iliyoidhinishwa na Serikali na Mamlaka husika ni kitendo cha upendo. Na ikiwa kama watu wengi zaidi watapata chanjo dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 ni kitendo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Huu ni upendo wa mtu binafsi; upendo kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na hatimaye ni upendo kwa watu wote. Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikitoa chanjo ya magonjwa hatari kama vile: surua, dondakoo, pepopunda na kifaduro na wala hakukuwa na malalamiko makubwa kama inavyojitokeza wakati huu wa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Baba Mtakatifu Francisko anadhani kwamba, hofu imezuka kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; tofauti ya chanjo inayotolewa. Kumekuwepo na chanjo ambazo zinadhaniwa kuwa na ubora wa kiwango cha juu na chanjo nyingine, zinahofiwa na watu wengi duniani, kiasi hata cha kutaka kuzikwepa. Muda uliotumika kutengeneza na kuzijaribia chanjo hizi nao unatia shaka kwa watu wengi. Watu wengine wana hofu ya mahali ambapo chanjo hii inazalishwa! Kimsingi chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 imepokelewa na watu wengi kwa hisia tofauti, kiasi kwamba, watu wamegawanyika sana. Si jambo la kushangaza hata kuona kwamba, hata katika Baraza la Makardinali kuna Kardinali ambaye anapinga katakata chanjo hii, lakini hivi karibuni, aliugua ugonjwa wa UVIKO-19. Yote haya anasema Baba Mtakatifu ni mambo ambayo yanapaswa kufafanuliwa kitaalam, ili kuwaondolea watu hofu dhidi ya chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, amani na utulivu wa ndani viweze kutawala. Wafanyakazi wote wa Vatican wamechanjwa, lakini hata huku kuna baadhi ya watu ambao bado wamegoma kuchanjwa, timu ya ushauri imeundwa ili kuwasaidia waweze kupata chanjo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati, ili kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Baba Mtakatifu anasema, wakati wa hija yake ya kitume nchini Hungaria amepata nafasi ya kutembelewa na viongozi wakuu wa Hungaria. Wakimbizi na wahamiaji, hawakuwa ni sehemu ya ajenda za mazungumzo yao. Wao wamezungumzia kuhusu: Ikolojia na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na jinsi Hungaria inavyosafisha maji ya mito yake, ili yaweze kuwa safi na salama. Wamejadiliana kuhusu ongezeko la idadi ya watu nchini Hungaria na kwamba, Serikali imetunga sheria ili kuwasaidia vijana kupata wenzi wa maisha, ili hatimaye, waweze kupata watoto tofauti kabisa na hali halisi ilivyo nchini Italia na Hispania kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa. Baba Mtakatifu amewapongeza wale wote wanaothubutu kufunga ndoa na kuanzisha familia. Changamoto kubwa kwa vijana wengi ni fursa za ajira. Mazungumzo na viongozi wakuu wa Hungaria yalidumu kwa takribani dakika 35 hadi 40.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo wa kidugu. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Kristo Yesu kwa maneno na matendo yake, amewaachia waamini Sakramenti kuu, Sadaka ya sifa, ili kuweza kushirikishana. Mwishoni mwa maisha na utume wake hapa duniani, anajitoa mwenyewe kwa wafuasi wake kuwa ni sadaka ya Pasaka. Hatima ya maisha ya mwanadamu ni kujitoa sadaka kwa ajili ya huduma ya upendo. Ukuu na utukufu wa Mungu unajionesha katika kipande cha Mkate uliomegwa, katika hali ya udhaifu na unyonge unaobubujika upendo wa Mungu ambao waamini wanapaswa kushirikishana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni Mkate unaomegwa kielelezo cha nguvu ya upendo inayopaswa kupokelewa kwa mikono miwili, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine, ili waweze kupata maisha mapya; nguvu ya upendo inayowaunganisha waamini. Ekaristi Takatifu ni nguvu inayowahamasisha waamini kuwapenda wale wanaokosea. Usiku ule uliotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu aliwapatia wafuasi wake Mkate wa maisha ya uzima wa milele. Hii ni zawadi ya hali ya juu kabisa kutoka katika sakafu ya Moyo wake Mtakatifu. Anakula na Mtume wake ambaye atamsaliti. Hakuna uchungu mkubwa kama kusalitiwa na mtu unayempenda. Kumtenga mtu na Kanisa ni maneno mazito sana! Kuna wakati alipokuwa anawahudumia wagonjwa wazee aliwauliza wale waliokuwa tayari kupokea Ekaristi Takatifu wanyooshe mkono, wakanyoosha wengi na baada ya kukomunika mmoja wao akasema alikuwa ni Myahudi na Baba Mtakatifu akamjibu kwamba, alikuwa amempatia Myahudi mwenzake, Yesu wa Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama waamini wanaitwa na kuhamasishwa kulinda, kuitunza na kuidumisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu, hata pale watu wanapokumbana na magonjwa pamoja na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Hakuna mwenye haki ya “kufyekelea mbali zawadi ya maisha ya binadamu”. Kutoa mimba ni mauaji. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, uhai wa binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa na kwa njia hii, kuweza kutangaza na kushuhudi tunu msingi za maisha ya Kikristo katika mazingira ya kifamilia. Kila huduma ya matibabu inayotolewa kwa mgonjwa iwe ni chemchemi ya huruma na upendo kwa wagonjwa wanaoteseka. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya mwanadamu yanapaswa kuwa kweli ni chombo cha huduma kwa wagonjwa na wala si vinginevyo.

Kamwe mgonjwa asionekane kuwa ni mzigo mzito, kiasi cha kuanza kuhalalisha kisheria mchakato wa kifolaini. Kwa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu, jambo hili linaweza kuonekana kuwa kama sehemu ya uhuru wa mtu binafsi; lakini ndani mwake, uhuru huu unafumbata ubinafsi unao thubutu kupima: haki, heshima na utu wa mtu kutokana na umuhimu wake. Kifolaini hakumsaidii mtu kumpunguzia maumivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, umefika wakati wa kusimama kidete kupinga utamaduni na utandawazi usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utoaji mimba, kifo laini na adhabu ya kifo ni mauaji yanayokwenda kinyume cha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kwa zile nchi ambazo zimetunga Sheria ya kutoa mimba, zimejikuta zikiwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa na matokeo yake ni watu wenye umri mkubwa kuongezeka maradufu! Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Kanisa kujikita katika shughuli za kichungaji na wala si kuwahukumu wanasiasa wanaojihusisha na utamaduni wa kifo. Kanisa lijitahidi kujenga ujirani mwema, kwa kuwaendea kwa huruma na upole.

Baba Mtakatifu Francisko amekumbushia kuhusu Tsunami iliyojitokeza ndani ya Kanisa baada ya kuchapisha Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia.” Kardinali Christoph Schönborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna ndiye alitoa ufafanuzi wa kina na hivyo kuokoa Jahazi! Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji isaidie kujenga mahusiano na mafungamano na watu, kadiri ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Ndoa ya Kikristo ina uzuri wake kwani hii ni Sakramenti inayoadhimishwa ndani ya Kanisa pamoja na kusaidia mchakato wa ujenzi wa Jumuiya mpya, Kanisa familia ya Mungu inayowajibika pamoja na jamii. Hili ni fumbo kuu linaloonesha uhusiano wa upendo wa dhati kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Hiki ni kielelezo makini cha upendo na imani ya Kanisa. Ndoa ni sehemu ya mpango wa kazi ya uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu na kwa njia ya neema na baraka za Mwenyezi Mungu, wakristo wameweza kuishi Sakramenti hii katika utimilifu wake. Sakramenti ya Ndoa ni tendo la imani mintarafu mpango wa Mungu kwa binadamu na ni kielelezo cha sadaka ya upendo. Mtakatifu Paulo katika nyaraka zake anaoanisha upendo wa Kristo kwa Kanisa lake kama ulivyo upendo kwa watu wa ndoa wanavyopaswa kupendana kwa dhati, kama Kristo alivyolipenda Kanisa kiasi cha kujisadaka kwa ajili yake. Pale ambapo mwanaume na mwanamke wanaamua kuoana katika Kristo Bwana, wanashiriki katika umisionari wa Kanisa, kwa kuishi si tu kwa ajili ya familia zao, bali kwa ajili ya wote.

Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa linadhalilishwa pale ndoa inapobomolewa. Wanandoa wanaoishi kikamilifu na kwa ujasiri neema ya Sakramenti ya Ndoa, wanalisaidia Kanisa kutoa zawadi ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wote sanjari na kuwasaidia watu wengine kuonja zawadi hizi katika maisha ya ndoa na familia zao. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna waamini ambao kweli wanajitahidi kuliishi Fumbo hili kwa ukamilifu wake, kwa kujiaminisha kwa Mungu na tunza kutoka kwa Mama Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa halina uwezo wa kubadili Sakramenti zilizoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe. Kuna sheria zilizowekwa na Kanisa ili kuwasaidia watu wenye mielekeo ya ndoa za watu wa jinsia moja. Serikali zina wajibika kuwapatia ulinzi na usalama, lakini Sakramenti ya Ndoa itabaki kuwa ni Sakramenti kati ya Bwana na Bibi. Watu wenye mielekeo ya ndoa za jinsia moja wasaidiwe, kwani Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu na Kristo Yesu anataka watu wote waokoke!

Papa Mahojiano
16 September 2021, 15:51