Tafuta

Papa Francisko Asasi ya Mfuko wa Archè ni alama ya alama ya huruma na matumaini kwa maskini na watoto Papa Francisko Asasi ya Mfuko wa Archè ni alama ya alama ya huruma na matumaini kwa maskini na watoto 

Asasi ya Mfuko wa Archè Ni Alama Upendo na Matumaini kwa Maskini

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi asili ya asasi ya Mfuko wa Archè ni upendo wa Mungu kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye asili ya uhai wote! Ni chemchemi ya kile kilicho chema, kizuri, cha kweli na kitakatifu. Mungu ni upendo uliotwaa mwili na kukaa kati ya binadamu kwa yeye Bikira Maria, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu, kiini cha matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Asasi ya Mfuko wa Archè “Fondazione Archè – ONLUS” ilianzishwa na Padre Giuseppe Bettoni kunako mwaka 1991 huko Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia, ili kukabiliana na changamoto zilizokuwa zimeibuliwa na ugonjwa wa UKIMWI, yaani Ukosefu wa Kinga Mwilini. Kuna watoto waliokuwa wanaachwa yatima baada ya mama zao wazazi kufariki dunia kutokana na UKIMWI. Katika kipindi cha Miaka 30 iliyopita Asasi ya Mfuko wa Archè: “Fondazione Archè – ONLUS” imeendelea kujipambanua kwa kuwasaidia na kuwasindikiza watoto na familia zenye uhitaji mkubwa katika mchakato wa kujitegemea kiuchumi na kijamii; kwa kuzitafutia makazi bora, fursa za ajira pamoja na huduma ya afya. Asasi hii inawapokea na kuwapatia hifadhi akina mama wanaodhulumiwa na kunyanyaswa kwa vipigo majumbani. Inatoa hifadhi kwa maskini, watu wenye matatizo ya afya ya akili; wakimbizi na wahamiaji ili kuwawezesha kuendeleza ndoto katika maisha yao. Asasi inawasaidia pia watoto wenye wazazi ambao wako gerezani au kulazwa hospitalini kwa muda mrefu. Inatoa makazi ya dharura kwa akina mama na watoto pamoja na stadi za maisha, ili kuwawezesha watu kujitegemea. Hii ni asasi ambayo imejielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Kwa sasa Asasi ya Mfuko wa Archè “Fondazione Archè – ONLUS” ina vituo vyake vya huduma: Milano ambako ndiko yaliyoko Makao makuu, Roma na San Benedetto del Tronto. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 2 Septemba 2021 amekutana na kuzungumza na wanachama wa Asasi ya Mfuko wa Archè “Fondazione Archè – ONLUS” waliofika kutoa ushuhuda wa maneno, sura, lakini zaidi kwa uwepo wao! Baba anasema, kimsingi asili ya asasi hii ni upendo wa Mungu kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye asili ya uhai wote! Ni chemchemi ya kile kilicho chema, kizuri, cha kweli na kitakatifu. Mungu ni upendo uliotwaa mwili na kukaa kati ya binadamu kwa yeye Bikira Maria, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Kumbe, asili ya yote haya ni Sura ya ufunuo wa huruma ya Mungu. Kwa upande wa Asasi ya Mfuko wa Archè sura hizi ni wanawake pamoja na watoto wao wanaosaidiwa ili kujikomboa kutoka katika dhuluma na nyanyaso. Hii ni huduma inayotolewa pia kwa wanawake wakimbizi na wahamiaji wanaobeba ndani mwao mang’amuzi machungu ya maisha!

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Asasi ya Mfuko wa Archè “Fondazione Archè – ONLUS” ni alama ya matumaini kwa wanawake na watoto wao na jamii katika ujumla wake. Hizi ni jumuiya zinazofanya mang’amuzi makubwa ya maisha kwa kushirikiana, kushikamana na kufanya kazi kwa ajili pamoja na maskini. Mama na mtoto ni kielelezo kinachofahamika sana kwa Wakristo. Mang’amuzi haya yamemwilishwa katika huduma makini kwa watu. Hiki ni kielelezo cha matatizo, shida na machungu ya maisha, lakini kwa wakati huo huo, ni kielelezo cha furaha inayojielekeza katika upendo unaosimikwa kwenye mshikamano, chemchemi ya uhuru, mwanzo mpya, utu na heshima. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapatia baraka zake za kitume, huku akiwataka kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Anakiri na kutambua kazi kubwa wanayoitekeleza hata kwenye mji wa Roma, kwa kufungua Jumuiya mpya. Huu ni mwaliko wa kuishi kadiri ya mtindo wa Mungu unaojikita hasa katika ujirani mwema, huruma na upendo. Jumuiya hii, iwe ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu na wala si kinyume chake. Roho Mtakatifu aendelee kupyaisha furaha ya Injili na Bikira Maria awalinde na kuwapatia tunza yake ya kimama.

Papa Ushuhuda
02 September 2021, 16:01