Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Vijana Kimataifa huko Bosnia ed Erzegovina: Mladifest, 2021 huko Medjugorje Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Vijana Kimataifa huko Bosnia ed Erzegovina: Mladifest, 2021 huko Medjugorje 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Vijana wa Medjugorje 2021: Ujasiri!

Maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, Papa anapenda kuwaonesha mambo msingi ya kuzingatia: Mosi, ni kuwatendea mema jirani kama sehemu ya utekelezaji wa Amri kuu ya upendo. Pili, vijana wakitaka kuwa wakamilifu, wauze walivyo navyo na wawape maskini na watajiwekea hazina mbinguni. Tatu, wakishatekeleza yote hayo, wamfuase Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 1 Agosti hadi tarehe 6 Agosti 2021, Sherehe ya Kung’ara Bwana, yanaongozwa na kauli mbiu “Mladifest 2021”: “Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?” (Mt 19:16). Maadhimisho haya yamepambwa kwa Ibada ya Misa Takatifu zilizoongozwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa. Tafakari ya kina ya Neno la Mungu sanjari na Katekesi makini kama sehemu ya majiundo endelevu na fungamani kwa vijana wa kizazi kipya. Huu ni utekelezaji wa mapendekezo ya Mababa wa Sinodi kuhusu utume wa vijana. Vijana wanapata fursa ya kujitenga na malimwengu kwa ajili ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kuadhimisha Sakramenti ya Upatanisho.

Hiki ni kipindi cha shuhuda mbalimbali za maisha na utume wa vijana katika kukabiliana na changamoto mamboleo na hatimaye kuna Ibada ya Njia ya Msalaba, kwa kuwakumbusha vijana kubeba vyema Misalaba yao na kuanza kumfuasa Kristo Yesu; njia, ukweli na uzima katika maisha ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina anapenda kuwaonesha mambo makuu matatu ya kuzingatia. Mosi, ni kuwatendea mema jirani kama sehemu ya utekelezaji wa Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Pili, vijana wakitaka kuwa wakamilifu, wauze walivyo navyo na wawape maskini na watajiwekea hazina mbinguni. Tatu, wakishatekeleza yote hayo, wamfuase Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza vijana wanaothubutu kutenga muda wao kwa ajili ya kujitajirisha katika maisha ya kiroho, huku wakiwa na shauku ya kukutana na Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu, ili hatimaye, waweze kupata maisha na uzima wa milele! Kauli mbiu ya maadhimisho ya vijana kwa mwaka 2021 ni “Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?” (Mt 19:16). Hili ni swali msingi linalopata majibu muafaka kama kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa vijana wa kizazi kipya anayewapatia mwaliko kwa kusema, “Njoo unifuate!” Mt. 19:21. Mwinjili Mathayo hamtaji jina yule kijana aliyemwendea Kristo Yesu, kumbe, hapa kila kijana anaweza kuweka jina lake. Mwinjili anamwelezea kijana yule kwamba, alikuwa ni msomi na kubahatika kuwa na mali nyingi, kiasi cha kumsukuma kutafuta furaha ya kweli na utimilifu wa maisha.

Kijana tajiri akatia nia ya kumtafuta Mwalimu na Kiongozi atakayemsaidia kutimiza ndoto yake katika maisha. Kufumba na kufumbua, akakutana na Kristo Yesu anayesema kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye ukamilifu wa wema na utakatifu wote wa maisha na mengine yote yanabubujika kutoka kwake! Ili kijana aweze kujichotea wema na furaha ya kweli katika maisha; Mosi, ni kuwatendea mema jirani kama sehemu ya utekelezaji wa Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Mt 18:17. Kijana yule tajiri akamwambia Kristo Yesu kwamba, katika safari ya maisha yake, daima amewatendea mema jirani zake. Kristo Yesu akamwangalia na kumpenda kwa sababu aligundia nia thabiti ya yule kiajana ya kutaka kupata utimilifu wa maisha. Kristo Yesu alitambua pia udhaifu wa yule kijana tajiri na kumtaka kupiga hatua moja mbele kwa kujiondoa katika haki kwa sababu ya kutenda mema na kujikita katika sadaka ya maisha. “Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” Yn 19:21.

Njia ya uzima wa milele iko wazi kwa wale wanaomfuasa Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, kama kielelezo cha ukomavu wa ndani. Huu ni mchakato wa kuondokana na utekelezaji wa Amri za Mungu kama mazoea na kuanza mchakato wa unaosimikwa katika sadaka na upendo; kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Hapa Kristo Yesu anakazia uhuru kamili, mahusiano na mafungamano yenye mvuto na mashiko, ili kumpenda Mungu na jirani, ili hatimaye, kupata furaha ya kweli na kupenda kwa dhati! Hatua ya tatu katika hija ya kijana tajiri ni mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu ili aweze kufanana naye, na hatimaye ataweza kupata fursa ya kukutana na watu wengi zaidi. Rej. Yn 19: 21. Kumfuasa Kristo Yesu katika maisha ni chemchemi ya furaha ya kweli na sadaka inayotolewa inang’oa vikwazo vyote. Kwa bahati mbaya, kijana tajiri alikuwa ameelemewa sana, kiasi cha kutaka kuwahudumia Mabwana wawili, yaani Mungu na mali! Ndiyo maana yule kijana aliposikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi: Mt 19:22.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kijana hakuwa na ujasiri wa kuachilia mbali utajiri uliokua unamfunga, tayari kufuata nyayo za Kristo Yesu, ili hatimaye, kugundua furaha ya kweli na utimilifu wa maisha. Hata leo hii anasema Baba Mtakatifu, Kristo Yesu anaendelea kutoa mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kumfuasa. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha vijana kujiachia ili wavutwe na Uso wa huruma na upendo wa Kristo Yesu, unaowaokoa kutoka katika vishawishi vya uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka unaoweza kuwatumbukiza katika utamaduni wa kifo. Vijana wawe na ujasiri wa kupokea Neno la Wito kutoka kwa Kristo Yesu, bila ya kukata wala kukatishwa tamaa kama ilivyokuwa kwa yule kijana tajiri! Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano na kielelezo bora cha kuigwa. Maisha ya Bikira Maria tangu alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, alianza hija ya maisha na hitimisho lake ni pale Mlimani Kalvari, alipomwona Mwanaye wa pekee akiinama kichwa na kukata roho. Bikira Maria akawa ni Mama wote na chemchemi kwa ajili ya huduma ya upendo kwa binamu yake Elizabeth.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina kwa kusema “Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Yesu. Wale wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo, daima furaha inazaliwa upya.” EG 1. Baba Mtakatifu anapenda kuwaaminisha vijana chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, huku akiwaombea mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu. Uso wa Mwenyezi Mungu anayewapenda daima, uwaangazie na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili kwa njia ya mahusiano na mafungamano na jirani zao, waweze kuwa ni mashuhuda wa maisha mapya ambayo wameyapokea kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Itakumbukwa kwamba, Padre Slavko Barbarić (11 Machi 1946 – 24 Novemba 2000) ndiye muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina.

Papa Vijana 2021

 

 

03 August 2021, 15:21