Tafuta

Tarehe 19 Agosti ya Kila mwaka Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani: Athari za mabadiliko ya tabianchi kwa binadamu! Tarehe 19 Agosti ya Kila mwaka Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani: Athari za mabadiliko ya tabianchi kwa binadamu! 

Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani 19-8- 2021

Maadhimisho ya Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani Papa anasema, athari za mabadiliko ya tabianchi, daima zimekuwa zikisababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu na waathirika wakuu ni maskini. Kumbe, kuna dharura ya kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na umoja wa familia ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 19 Agosti inaadhimisha Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani iliyoridhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2009. Hii ni kumbukumbu endelevu ya shambulio la kigaidi lililotokea kwenye Hotel ya Canal mjini Baghdad, nchini Iraq kunako mwaka 2003 na hivyo kupelekea watu 22 kupoteza maisha, akiwemo Bwana Sergio Vieira de Mello, aliyekuwa Mkurugenzi wa huduma ya kibinadamu nchini Iraq. Maadhimisho ya Mwaka 2021 yanalenga kuragibisha zaidi kuhusu gharama ya binadamu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuokoa maisha ya watu maskini zaidi ulimwenguni. Katika ulimwengu mamboleo, kampeni za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote zinaendelea kupamba moto!

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2021 zaidi ya watu milioni 235 wanahitaji msaada wa kibinadamu kutokana na athari mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani anasema, athari za mabadiliko ya tabianchi, daima zimekuwa zikisababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu na waathirika wakuu ni maskini, “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Kumbe, kuna dharura ya kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika haki, amani na umoja wa familia ya binadamu!

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres katika maadhimisho haya anasema, wahudumu wa masuala ya kibinadamu wako mstari wa mbele katika mchakato wa kusaidia kuokoa maisha ya watu ambao wako hatarini sehemu mbalimbali za dunia, majanga yanapozuka. Hawa ni watu wanaohatarisha na wakati mwingine kusadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hawa ni watu wanaokabiliwa na ongezeko kubwa la vistisho. Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, matukio ya wafanyakazi hawa kupigwa risasi, kutekwa nyara na hata kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi yameongezeka maradufu. Katika kipindi cha Mwaka 2021, zaidi ya wafanyakazi 72 tayari wamekwisha kupoteza maisha, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, wanalindwa, ili waweze kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa watu wanaohitaji msaada wa dharura.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatishia usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Waathirika wakuu wa majanga asilia ni maskini. Kumbe, ni wajibu wa kila mtu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kadiri ya nafasi, uwezo na dhamana yake! Baba Mtakatifu anasema, binadamu ni sehemu ya Kazi ya Uumbaji, changamoto ni kutenda na kuwajibika kama watunzaji bora wa mazingira na wala si kama wakwapuaji wa rasilimali za dunia, jambo linalohatarisha msingi unaotegemeza maisha ya mwanadamu. Matokeo yake ni athari za mabadiliko ya tabianchi zinazojionesha kwa mafuriko, baa la njaa linalowapekenya watu wengi duniani; mambo yanayohatarisha ustawi na maendeleo kwa sasa na kwa siku zijazo kama wanavyobainisha wanasayansi. Familia ya watu wa Mungu inapaswa kusaidiana na kuwajibikiana, kwa kuheshimu na kufuata dhamiri nyofu inayowadai utunzaji bora wa mazingira na wala si uharibifu na ulaji wa kupindukia. Jumuiya ya Kimataifa inao wajibu wa kutunza mazingira ili kuhakikisha kwamba inakiachia kizazi kijacho mazingira bora zaidi ya kuishi.

Umoja, mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa yanahitajika sana na ni sehemu muhimu sana ya maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (Cop26) utakaofanyika mjini Glasgow nchini Uingereza. Baba Mtakatifu anasema, bayianuai ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya ikolojia. Kumbe, kuna haja ya kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa kwa kulinda asilimia 30% ya dunia kama hifadhi maalum hadi kufikia mwaka 2030, ili kuondokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na kupotea kwa bayoanuai. Ni wakati muafaka wa kuragibisha umuhimu wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Ni wakati wa kurekebisha mfumo wa uchumi na malengo yake; mfumo wa maendeleo ili hatimaye, kufanya marekebisho katika mifumo ambayo inahatarisha na kuharibu mazingira. Binadamu anapaswa kuchukua hatua ya kwanza kwa kufanya wongofu wa kiikolojia na kwamba, kipindi hiki kisaidie kujenga huruma kwa kujikita katika kipaji cha ubunifu na ujasiri.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, linawataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanajipanga kikamilifu ili kukabiliana na athari za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika umaskini wa hali na kipato! Machafuko ya kisiasa nchini Afghanstan na Lebanon; maafa ya tetemeko la ardhi nchini Haiti ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa kwa sababu wanaoathirika ni maskini na wanyonge zaidi katika jamii. Caritas Internationalis inawataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na watunga sera duniani, kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula. Watu wanajenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kibinadamu katika kukabiliana na maafa asilia. Jumuiya ya Kimataifa iendelee kutekeleza sera na mikakati ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kujikita katika mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na teknolojia rafiki kwa mazingira. Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (Cop26) unapaswa kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi kama jambo tete sana kwa binadamu!

Papa Wahudumu
19 August 2021, 16:13