Tafuta

Papa Francisko Ujumbe: Jubilei ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Mt. Andrea Kim Taegon. Papa Francisko Ujumbe: Jubilei ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Mt. Andrea Kim Taegon. 

Papa: Jubilei ya Miaka 200 ya Kuzaliwa Mt. Andrea Kim Taegon

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyelijalia Kanisa Mtakatifu Andrea Kim Taegon mfano bora na ushuhuda wa imani thabiti na mwamba katika mchakato wa uinjilishaji katika nyakati ngumu za historia ya Korea, iliyopambwa kwa madhulumu na nyanyaso. Ni mfano wa furaha ya matumaini juu ya upendo wa Mungu unaoshinda ubaya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Mama Kanisa tarehe 21 Agosti 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbukizi la Miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon kutoka Korea. Mtakatifu Andrea Kim Taegon, alikuwa ni Padre wa kwanza Mzalendo kuwekwa wakfu nchini Korea. Aliuwawa kikatili tarehe 16 Septemba 1846 wakati wa madhulumu nchini Korea kati ya Mwaka 1839-1846. Papa Pio XI tarehe 5 Mei 1925 akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 6 Mei 1984. Mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Andrea Kim Taegon na wenzake 102 kila mwaka ifikapo tarehe 16 Septemba. Kilele cha Jubilei ya Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Andrea Kim Taegon ni tarehe 27 Novemba 2021. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wa matashi mema, watu wa Mungu kutoka Korea wanaoishi mjini Roma, waliohudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyelijalia Kanisa Mtakatifu Andrea Kim Taegon mfano bora na ushuhuda wa imani thabiti na mwamba katika mchakato wa uinjilishaji katika nyakati ngumu za historia ya Korea, iliyopambwa kwa madhulumu na nyanyaso. Mtakatifu Andrea Kim Taegon na wenzake 102 ni mfano wa furaha ya matumaini inayoonesha kwamba, upendo wa Mungu daima unashinda ubaya, chuki na uhasama! Hata leo hii kuna ubaya unaoendelea kusababisha mateso kwa binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Kumbe, hapa kuna haja ya kugundua tena umuhimu wa utume na dhamana ya kila Mkristo mbatizwa, anayepaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha amani na matumaini, kielelezo cha Msamaria mwema, tayari kupiga magoti na kuinama ili kufunga majeraha ya watu wenye kiu ya upendo, msaada au wale wanaotamani walau kuona ufunuo wa uso wa udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kulipongeza Kanisa nchini Korea kwa kuonesha na kushuhudia ukarimu kwa kuenzi kampeni ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa ajili ya nchi maskini zaidi duniani. Huu ni ushuhuda unaowachangamotisha watu wa Mungu kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya maskini na wangonge zaidi katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Huu ni mwaliko wa kuendelea kujisadaka kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini. Mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano ni dhamana na wajibu wa watu wote wa Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, wataendelea kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ujenzi wa Korea inayong’aa zaidi kwa siku za usoni! Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka watu wote wa Mungu nchini Korea chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, mashuhuda na wafiadini wa Korea na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Papa Korea
21 August 2021, 16:42