Tafuta

Siku ya Vijana Kimataifa Kwa Mwaka 2021 Kauli mbiu "Kubadilisha Mfumo wa Chakula: Vijana kwa Afya ya Binadamu na Sayari! Siku ya Vijana Kimataifa Kwa Mwaka 2021 Kauli mbiu "Kubadilisha Mfumo wa Chakula: Vijana kwa Afya ya Binadamu na Sayari! 

Papa Francisko: Ujumbe Siku ya Vijana Kimataifa Kwa Mwaka 2021

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa kwa Mwaka 2021 ni “Kubadilisha Mfumo wa Chakula: Vijana kwa Afya ya Binadamu na ya Sayari" Papa: Kwa msaada wa vijana na roho yao ya ubunifu Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufanikisha ndoto ya ulimwengu ambamo kuna chakula, maji, dawa na fursa za ajira zinapatikana kwa wingi na kuwafikia kwanza kabisa wahitaji zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1965 lilianza juhudi za kuwekeza katika vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha ya jamii inayowazunguka. Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa walitoa Tamko kuhusu vijana na kuwataka kujikita zaidi katika amani, heshima, maelewano na mafungamano kati ya watu wa Mataifa. Umoja wa Mataifa ukaanza kutenga rasilimali fedha na watu ili kuwaandaa vijana kutekeleza majukumu yao barabara kwa siku za usoni. Kunako tarehe 17 Desemba 1999 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliridhia wazo la kuanzisha Siku ya Kimataifa ya Vijana. Kwa mara ya kwanza Siku hii iliadhimishwa tarehe 12 Agosti 2000. Tangu wakati huo, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku hii ili kuwaelimisha vijana kuhusu umuhimu wao katika Jumuiya ya Kimataifa. Vijana wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuratibu matumizi sahihi ya rasilimali za dunia. Vijana wanahimizwa kushiriki katika siasa pamoja na kujielekeza zaidi katika kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake!

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa kwa Mwaka 2021 ni “Kubadilisha Mfumo wa Chakula: Vijana kwa Afya ya Binadamu na ya Sayari.” Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema kwamba, kwa msaada wa vijana na roho yao ya ubunifu Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufanikisha ndoto ya ulimwengu ambamo kuna chakula, maji safi na salama; dawa na fursa za ajira zinapatikana kwa wingi na kuwafikia kwanza kabisa wahitaji zaidi! Ndoto hii haitaweza kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa, ikiwa kama vijana wa kizazi kipya hawatashirikishwa kikamilifu. Vijana wanapaswa kujengewa uwezo katika ngazi ya mtu binafsi na vijana katika ujumla wao, ili waweze kushiriki kwenye mchakato wa marekebisho ya Sayari hii inayoendelea kukumbana na changamoto nyingi. Vijana hawana budi kusimama kidete kulinda na kudumisha uhai sanjari na unapatanishao wa bioanuwai katika mabadiliko ya mifumo ya chakula. Inakadiriwa kwamba, katika kipindi cha miaka thelathini ijayo, idadi ya watu duniani itakuwa imefikia watu bilioni mbili.

Kumbe, kuna haja ya kuweka mbinu mkakati utakaosaidia kuzalisha chakula bora ili kulisha ongezeko hili la watu duniani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Changamoto hii haina budi kwenda sanjari na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Kimataifa, ifikapo mwaka 2030. Itakumbukwa kwamba, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora na makini kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa kwa Mwaka 2020 yalitoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kila linalowezekana kuwawezesha vijana ulimwenguni kufurahia maisha yanayokita mizizi yake katika hali ya usalama, utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kupata fursa ya kuchangia katika hatua za pamoja za kimataifa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya yamehatarishwa kwa: hatua zao kuelekea utu uzima, utambulisho na kujitosheleza yamegeuziwa kisogo. Baadhi ya vijana wamechukua mizigo ya kulea au wanateswa na baa la njaa, unyanyasaji na hali ya kukata tamaa ya kusonga mbele na masomo. Vijana wa kizazi kipya wana nguvu na utashi wa kutaka kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni vijana ambao wameamka na wako makini katika kudai utekelezaji wa sera na mikakati dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Hiki ni kizazi cha vijana wanaotaka kuona jamii inasimikwa katika misingi ya haki, amani na usawa sanjari na kuambata mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu! Tema ya Mwaka 2019 ilikuwa ni kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu ili kuifanya elimu kuwa fungamanishi zaidi, rahisi kupatikana na inayokwenda na kasi ya ulimwengu mamboleo!

Papa Vijana Kimataifa
12 August 2021, 14:03