Tafuta

Papa Ondoeni Unafiki, Shuhudieni Imani ya Kweli Kutoka Moyoni!

Tatizo kwa Mafarisayo na Waandishi ni kukazia matendo ya nje kama kielelezo cha dini na hivyo kusahau kusafisha nyoyo zao. Kishawishi kikubwa ni kutaka kujionesha kwa nje mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini, Kristo Yesu, kamwe haridhishwi na mwonekano huo wa mambo ya nje, bali anataka imani inayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mtu mwenyewe! Unafiki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa na hususan Injili inaonesha majadiliano ya Mafaraisayo na Waandishi kuhusu mapokeo, baada ya kuona baadhi ya wanafunzi wa Kristo Yesu wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani isiyonawiwa! Wakakwazika sana kwa sababu wanafunzi wa Yesu walikuwa hawaendi kwa kufuata mapokeo ya wazee. Rej. Mk 7:2-5. Hata leo hii, baadhi ya waamini wanajiuliza, ilikuwaje, hata wanafunzi wa Kristo Yesu wakashindwa kufuata mapokeo ya wazee wao? Kimsingi huu ni ustaarabu, mapokeo na mila njema ya kunawa kabla ya kula chakula! Si kwamba, Kristo Yesu anapinga mila, desturi na mapokeo haya, bali anataka kuhakikisha kwamba, imani inapewa kipaumbele chake katika maisha ya waamini! Lengo ni kuondokana na unafiki kama ilivyokuwa kwa Mafarisayo na Waandishi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo yanayoonekana kwa nje na kusahau imani ya kweli inayopaswa kuwa ni kiini cha matendo yote ya nje. Tatizo kwa Mafarisayo na Waandishi ni kukazia matendo ya nje kama kielelezo cha dini na hivyo kusahau kabisa kusafisha nyoyo zao. Kishawishi kikubwa ni kutaka kujionesha kwa nje mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ibada. Lakini, Kristo Yesu, kamwe haridhishwi na mwonekano huo wa mambo ya nje, bali anataka imani inayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mwamini mwenyewe!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 29 Agosti 2021. Baada ya kukazia umuhimu wa kusafisha nyoyo zao, Kristo Yesu anakaza kwa kusema, “Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu… Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.” Mk 7:15, 21-23. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, maneno haya ya Kristo Yesu yalikuwa ni mapinduzi makubwa kwa sababu kadiri ya mapokeo ya wazee wao baadhi ya vyakula au mwingiliano na mambo ya nje yalimletea mtu unajisi. Mawazo kama haya bado yanaendelea kutawala hata katika ulimwengu mamboleo kwa kudhani kwamba, tabia. Mwenendo na mawazo ya watu wengine au jamii yanaweza kusababisha unajisi. Hivi ndivyo watu wanavyowahukumu wengine, jamii na ulimwengu katika ujumla wake.

Wakati mwingine, viongozi wa jamii wanatwishwa makosa na kutuhumiwa kwa kuwasababishia wengine unajisi. Tabia kama hii ni kupoteza wakati. Na kwa jinsi hii, watu wanakuwa kama “Mbogo” na wakali kushinda hata “Pilipili kichaa”, kiasi cha kumsukumizia Mwenyezi Mungu mbali kabisa na sakafu ya nyoyo zao! Mwelekeo kama huu ni sawa na wale watu waliosikika kwenye Injili wakilalamika na hatimaye, kuishia kwenye kashfa, kiasi hata cha kushindwa kumpokea Kristo Yesu katika maisha yao. Hakuna mwamini anayeweza kuwa kweli mchamungu na mtauwa wa kweli, ikiwa kama maisha yake yote yamejengeka katika “litania ya malalamiko tu”: hasira, chuki na uhasama; mambo yanayomfungia Mwenyezi Mungu lango la kuingia katika maisha. Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kuwakoa kutoka kwenye tabia ya kuwatuhumu wengine bila sababu. Katika sala, watu wa Mungu wajitahidi kumwomba Mungu awajalie neema ya kuokoa muda kwa kuondokana na uchafuzi wa ulimwengu kwa kulalamika, kwa sababu, kimsingi huu si Ukristo!

Kristo Yesu anawaalika waja wake kuuangalia ulimwengu kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Ikiwa kama, katika ukweli, waamini watamwomba Mwenyezi Mungu neema ya kusafisha na kutakasa nyoyo zao, hapo kweli, ulimwengu utaweza kuwa safi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna njia makini ya kushinda dhambi na ubaya wa moyo, kwa kuanza kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Mababa wa Kanisa wanasema, njia ya utakatifu wa maisha inaanza pale mwamini anapo chunguza dhamiri yake ili kugundua udhaifu na huo unakuwa ni mwanzo wa toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anawashauri waamini kuchunguza dhamiri zao, jambo ambalo litawasaidia katika kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewaelekeza waamini kwa Bikira Maria aliyeweza kubadili historia kwa njia ya usafi wake wa Moyo, awasaidie na kuwaombea ili waweze kusafisha na kutakasa nyoyo zao, kwa kuvuka kishawishi cha kuwatuhumu watu wengine na kulalama kwa kila jambo!

Papa Angelus

 

29 August 2021, 15:30

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >