Tafuta

Vatican News

Papa Francisko: Mtafuteni kwa Upendo Yesu Azime Njaa ya Maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anasema waamini wanapaswa kutambua jambo gani linalowasukuma kumtafuta Yesu! Huu ni mchakato wa kumpokea na kumkaribisha Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha, ili kujenga na kudumisha historia ya upendo wa dhati, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza. Ni kwa njia hii, Kristo Yesu ataweza kuitakasa imani na kuimarisha mafungamano ya upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili 18 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inakita ujumbe wake kwa Kristo Yesu kuwa ndiye “Chakula cha uzima.” Mkutano ulikuwa unamtafuta Yesu na walipomkosa, wakaamua kupanda mashua na kuelekea Kapernaumu, ng’ambo ya bahari na walipomwona, wakamwambia, “Rabi, wewe umekuja lini hapa?” Kwa haraka haraka, watu wanaweza kudhani kwamba, mkutano huu ulikuwa na hoja ya msingi kiasi hata cha kujitaabisha kumtafuta Kristo Yesu! Kumbe, haitoshi kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha, jambo la msingi ni kutambua, ni sababu gani inayomsukuma mtu kiasi cha kumtafuta Mwenyezi Mungu kwa udi na uvumba? Ndiyo maana Kristo Yesu anawajibu akisema: “Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa mhuri na Baba, yaani, Mungu.” Yn 6:26-27. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 1 Agosti 2021.

Ule umati baada ya kula na kushiba, haukuwa umetambua maana halisi ya ishara ile ya kugeuza mikate ile mitano na samaki wawili. Walibaki wakiwa wameshikilia mambo ya nje bila kuzama katika undani wake. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza, Je, wanamtafuta Kristo Yesu kwa sababu gani msingi inayobubujika kutoka katika imani? Mwamini asipofanya mang’amuzi ya kutosha anaweza kujikuta akitumbukia katika kishawishi cha kuabudu vitu na malimwengu. Pengine, hii ndiyo sababu msingi inayowasukuma waamini wengi kumtafuta Mwenyezi Mungu, ili aweze kutosheleza tamaa na mahitaji yao; awasaidie kutatua matatizo yanayowasonga. Awapatie neema na baraka ambazo kwa nguvu zao wenyewe kamwe hawawezi kuzipata. Katika hali na mazingira kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko imani inabaki ikielea juu kwenye ombwe bila ya kuzama katika uhalisia wa maisha ya mwamini. Hii ndiyo imani ya miujiza wanayoitafuta waamini wengi katika hija ya maisha yao hapa duniani! Lakini, waamini hawa hawa mambo yao yanapowanyookea wakati wa “kula bata kwa mrija” kamwe hawawezi kumkumbuka Mwenyezi Mungu na matokeo yake, “wanamtundika pembezoni mwa vipaumbele vyao kama Kinubi.”

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni vyema na haki kwa waamini kumpelekea Mwenyezi Mungu shida na mahangaiko yao ya ndani! Lakini, ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu anayetenda kwa haki na busara anataka kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati na waja wake katika upendo. Huu ni upendo wa kweli na wala si “Upendo wa ndoana, yaani nipe nikupe.” Upendo wa kweli kamwe haufungwi na ubinafsi, bali ni bure kabisa! Si vyema kumpenda mtu ili uweze kupata kitu kutoka kwake! Baada ya mkutano kuambiwa ukweli wa ishara iliyotendwa na Kristo Yesu, umati ukamuuliza tena Kristo Yesu: “Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.” Yn 6:28-29. Kwa maneno mengine, watu walitaka kufahamu watende kitu gani ili kutakasa mchakato wao wa kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha’ Yaani safari ya kutoka katika imani inayokita mizizi yake katika miujiza ili kutosheleza mahitaji binafsi hadi imani inayosimikwa katika upendo kwa Mwenyezi Mungu, aliye asili ya wema na utakatifu wote? Jibu la Kristo Yesu ni makini kabisa, yaani imani kwake aliyetumwa na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ni mchakato wa kumpokea na kumkaribisha Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha, ili kujenga na kudumisha historia ya upendo wa dhati, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza. Ni kwa njia hii, Kristo Yesu ataweza kuitakasa imani na kuimarisha mafungamano ya upendo. Waamini wajifunze kwanza kumpenda Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, kuliko mambo mengine yote anayoweza kuwakirimia katika hija ya maisha yao hapa duniani. Huu ndio mwelekeo sahihi katika ujenzi wa mahusiano na Mwenyezi Mungu na hata kati ya mtu na mtu na hata katika mahusiano ya kijamii. Kuna hatari kubwa ya kumtumia Mungu na watu kwa ajili ya kutosheleza matamanio ya kibinadamu na mafao binafsi. Jamii inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa vitu badala ya utu, heshima na haki msingi za binadamu, hiyo ni jamii ambayo kamwe haiwezi kuwa ni chemchemi ya Injili ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake kwa kusema wito na mwaliko wa Injili ya Jumapili ya 18 ya Mwaka B wa Kanisa ni waamini wasikitendee kazi chakula kiharibikacho, au chakula kinachozima njaa ya mwili peke yake! Waamini wajitahidi kumpokea na kumkaribisha Kristo Yesu kama chakula cha uzima wa milele; kwa kujenga na kudumisha urafiki na waamini wenyewe wakijitahidi kupendana kati yao, bila ya kujitafuta wala kutafuta mafao yao binafsi. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa ni kielelezo na mfano bora wa upendo kwa Mwenyezi Mungu, awaombee waamini ili kwamba, Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia neema na baraka za kuweza kuwa wazi ili hatimaye, kukutana na Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai!

Papa Upendo
01 August 2021, 14:36

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >