Tafuta

Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kinyama huko Plymouth nchini Uingereza. Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kinyama huko Plymouth nchini Uingereza. 

Papa Francisko Asikitishwa na Mauaji ya Kinyama Uingereza!

Waamini Jumanne, tarehe 17 Agosti 2021 walikusanyika kwenye Kanisa la St. Thomas, huko Keyham katika mji wa Plymouth nchini Uingereza kusali kwa ajili ya kuwaombea watu 6 waliopoteza maisha yao kutokana na shambulizi la kinyama lililofanywa Alhamisi tarehe 12 Agosti 2021 na Bwana Jake Davison mwenye umri wa miaka 23 kabla ya kujifyatulia risasi na kupoteza maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Waamini wa Kanisa Katoliki, Jumanne jioni tarehe 17 Agosti 2021 walikusanyika kwenye Kanisa la St. Thomas, huko Keyham katika mji wa Plymouth nchini Uingereza kusali kwa ajili ya kuwaombea watu 6 waliopoteza maisha yao kutokana na shambulizi la kinyama lililofanywa Alhamisi tarehe 12 Agosti 2021 na Bwana Jake Davison mwenye umri wa miaka 23 kabla ya kujifyatulia risasi na kupoteza maisha! Ibada hii ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu Mark O' Toole wa Jimbo Katoliki la Plymouth nchini Uingereza.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa Kanisani hapo, amependa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu uzito! Baba Mtakatifu anaungana na watu wa Mungu ili kuwaombea Marehemu upendo wa huruma ya Mungu sanjari na uponyaji na faraja kwa wale waliojeruhiwa katika shambulio hizi. Baba Mtakatifu anasali ili Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu awajalie watu wote neema ili wasishindwe na ubaya, bali waushinde ubaya kwa wema! Rej. Rum 12:21. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia baraka zake za kitume, wote walioshiriki katika Ibada hii ya Misa takatifu.

Mauaji Uingereza
18 August 2021, 14:13