Kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu! Matumaini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Tarehe 22 Agosti, kila Mwaka, Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia wa mbingu, Sikukuu iliyoanzishwa na Papa Pio wa XII kunako mwaka 1954 kama alama ya matumaini kwa watu wa Mungu. Ni Sikukuu inayomwonesha Bikira Maria aliyepewa upendeleo wa pekee, ili kushiriki ukuu wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu: Kuhani, Mfalme na Nabii. Hii ni dhamana ambayo Wakristo wabatizwa wanaishiriki kikamilifu mintarafu Sakramenti ya Ubatizo. Papa Pio XII katika Waraka wake wa kitume “Ad Caeli Reginam” anabainisha kwamba, ingawa Sikukuu inaonekana kana kwamba, ni mpya, lakini inachota utajiri wake katika Maandiko Matakatifu, Liturujia ya Kanisa, Sanaa ya mambo matakatifu pamoja na Ibada ya watu wa Mungu kwa Bikira Maria. Kwa mara ya kwanza Sikukuu hii iliadhimishwa tarehe 31 Mei, lakini baada ya mageuzi ya Liturujia yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Sikukuu hii ikapangwa iadhimishwe tarehe 22 Agosti ya kila mwaka. Hii ni kumbukumbu inayoadhimishwa na Mama Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria, siku chache tu baada ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, hapo tarehe 15 Agosti.
Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio XII katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”. Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae”.
Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 alitangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Bikira Maria Malkia wa Mbingu anashiriki utukufu wa ufalme wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, alama na mfano wazi kabisa ya matumaini ya Wakristo ambao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo nao pia wanashiriki: ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo. Papa Pio XII, tarehe 1 Novemba 1954 aliwaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika shida na mahangaiko yao. Bikira Maria ni kikao cha hekima na faraja kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo.
Hii ni faraja inayobubujika kutoka katika msingi wa imani, matumaini na mapendo, kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Bikira Maria alishiriki hatua kwa hatua mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani na hatimaye, kushirikishwa utukufu wa Mwanaye mpendwa kwa kupalizwa mbinguni mwili na roho. Kwa waamini walioko huku bondeni kwenye machozi, wasisite kukimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Bikira Maria anashiriki kwa namna ya pekee upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya walimwengu. Ni kielelezo cha unyenyekevu na huduma ya upendo, inayofumbatwa katika kuhudumia, kusaidia na kupenda kwa dhati. Kristo Yesu aliposulubiwa pale mlimani Golgota, palikuwa na anuani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, “Mfalme wa Wayahudi”. Huu ni ufalme unaokita mizizi yake katika unyenyekevu, mateso na upendo wa dhati. Ni kwa njia hii, Ufalme wa Kristo Yesu unakuwa ni chemchemi ya ukweli, upendo, haki na amani. Ni ufalme unaofumbatwa katika huduma, kama ambavyo Bikira Maria alivyomjibu Malaika Gabrieli kwamba, yeye ni mjakazi wa Bwana na katika mwanga huu, Kanisa linamwona Malkia aliyezama katika huduma, sala na upendo.
Katika Litania ya Bikira Maria, waamini wanamsifu Bikira Maria kuwa ni Malkia wa Malaika, Malkia wa Mababu, Malkia wa Manabii, Malkia wa Mitume, Malkia wa Mashahidi na Waungama dini; Malkia wa Watakatifu wote na mwishoni anatajwa kuwa ni Malkia wa familia. Waamini wanamkimbilia Maria kwa sala na salam, wakisema, Salam Malkia wa mbingu! Heshima ya Bikira Maria kuitwa Malkia ni kielelezo cha imani, furaha, mapendo na msaada wa daima. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Ibada kwa Bikira Maria ni sehemu muhimu sana katika maisha ya kiroho. Hata katika shida na mahangaiko yao ya kiroho na kimwili, waamini wawe na ujasiri wa kumkimbilia Bikira Maria Malkia wa mbingu, anayewapenda, kuwasikiliza na kuwaombea kwa Mwanae mpendwa Kristo Yesu! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Bikira Maria asiye na doa, aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, akishamaliza mwendo wa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni pamoja na mwili na roho yake, akatukuzwa na Bwana kama Malkia wa ulimwengu, ili afananishwe kikamilifu zaidi na Mwanawe, aliye Bwana wa mabwana. Rej. LG. 59.
Waamini wanataka kuungana na Bikira Maria katika maisha na utume wake, huku wakijitahidi kufuata nyayo zake katika Njia ya Msalaba wa Mwanaye Kristo Yesu hadi pale Mlimani Kalvari, huku wakisali na kusema: “Salamu Malkia, Mama mwenye huruma, uzima, tulizo na matumaini yetu salam. Tunakusihi hapa ugenini sisi wana wa Eva, tunakulilia tukilalamika na kuhuzunika bondeni kwenye machozi. Haya basi mwombezi wetu, utuangalie kwa macho yako yenye huruma na mwisho wa ugeni huu, utuoneshe Yesu mzao mbarikiwa wa tumbo lako, Ee mpole, Ee mwema, Ee mpendelevu Bikira Maria.” Mtakatifu Paulo wa VI anasema kwamba, waamini ni sehemu muhimu sana ya umoja wa Fumbo wa Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, wanapaswa kuwa na mwono mpana zaidi kuhusu kazi ya Ukombozi na mchakato wa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha; kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu.