Tafuta

Papa Francisko asema  Prof. Edgar Morin ni Msomi anayejisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Francisko asema Prof. Edgar Morin ni Msomi anayejisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Prof. Edgar Morin, Anajisadaka Kwa Utu na Mafao ya Wengi!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Prof. Edgar Morin amekuwa akijipambanua katika kunogesha sera na siasa za kistaarabu zinazotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Anahamasisha umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa Mataifa, ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na utu wa binadamu sanjari na upyaishaji wa demokrasia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Profesa Edgar Morin, ambaye pia anajulikana kama Edgar Nahoum alizaliwa tarehe 8 Julai 1921 na mwaka 2021 anasherehekea Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwake. Ni mwanafalsafa na mwanajamii kutoka Ufaransa, maarufu sana sehemu mbalimbali za dunia kutokana na mchango wake wa mawazo kimataifa. Ni mwanazuoni ambaye amechangia sana katika uringo wa siasa, sayansi jamii, ikolojia; antholopolojia ya kuona, elimu na bayolojia. Amekwisha kuandika vitabu zaidi ya 60 ambavyo vinapatikana kwa lugha ya Kifaransa zaidi. Ni katika muktadha huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni, UNESCO, tarehe 2 Julai 2021 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Prof. Edgar Morin na kilele chake kitakuwa ni hapo tarehe 8 Julai 2021. UNESCO imeamua kumuenzi Bwana Edgar Morin kutokana na mchango wake mkubwa katika elimu, sayansi na utamaduni na kwamba ameendelea kujipambanua kuwa ni mwanazuoni mahiri na moja ya watu wa rejea kutoka UNESCO.

Ujumbe wa Baba Mtakatifru Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro, Katibu mkuu wa Vatican na umesomwa na Monsinyo Francesco Follo, Mwakilishi wa wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO. Na kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Prof. Edgar Morin katika sekta ya elimu na utamaduni. Amejitahidi kuyamimina maisha yake kwa ajili ya mchakato wa maboresho ya maisha ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Daima amekuwa ni msomi aliyeongozwa na dhamiri nyofu, akakazia kanuni maadili na utu wema katika masuala ya sayansi, ili kamwe sayansi isisababishe majanga katika maisha ya familia kubwa ya binadamu. Wanasayansi hawana budi kukumbuka kwamba, wanao wajibu wa kuwasaidia watu kutumia vyema maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala sayansi isiwe ni chanzo cha maafa kwa binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Prof. Edgar Morin amekuwa akijipambanua katika kunogesha sera na siasa za kistaarabu zinazotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu na wala si uchu wa mali na madaraka! Prof. Edgar Morin ni Msomi anayejipambanua katika kuhamasisha umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa Mataifa, ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na utu wa binadamu sanjari na upyaishaji wa demokrasia inayokita mizizi yake katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya maridhiano, haki, amani na ukarimu. Alimpongeza na kumsifu Baba Mtakatifu Francisko kwa umakini wake katika mafundisho jamii ya Kanisa. Ni Msoni aliyeshiriki katika mchakato wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” kuanzia tarehe 11-18 Oktoba 2020 na kutiwa mkwaju hapo tarehe 15 Oktoba 2020. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano huu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran kilichoko mjini Roma alikazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Janga la elimu duniani, maana ya elimu, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu duniani na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu duniani!

Baba Mtakatifu alisema lengo kuu ni kuanzisha Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” utakaotekelezwa kwenye nchi mbali mbali, kwa kuwekeza nguvu zaidi na vipaji ili kuanzisha mchakato wa ushirikiano na vyama vya kiraia ili kuleta mageuzi. Mafundisho Jamii ya Kanisa kadiri ya Ufunuo wa utu mpya ndani ya Kristo Yesu unaiwezesha jamii kujenga msingi thabiti pamoja na kuwa na rejea makini zinazonesha dira na mwongozo wa kufuata wakati wa dharura. Uwekezaji huu unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika mafungamano ya udugu wa kibinadamu, ambayo ni wazi, ili kuhakikisha kwamba watoto na vijana wanapata elimu bora kadiri ya utu na heshima ya binadamu, ili kutekeleza wito wake wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Tarehe 27 Juni 2019, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kuzungumza na Prof. Edgar Morin. Alimpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, uliozinduliwa tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu.

Katika Waraka huu, Baba Mtakatifu anapembua kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira, umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia na kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira. Anazungumzia kuhusu haki ya maji safi na salama. Mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, urithi unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utunzaji wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na uwajibikaji na wala maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasitumike kama nguvu ya kiuchumi kwa ajili ya kunyonya Mataifa mengine wala kuyatumbukiza katika utamaduni wa kifo. Nguvu ya fedha iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa ijenge utamaduni wa kujadiliana, kuamua na kutenda kwa pamoja. Mapambano ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni muhimu, ili kujenga mtandao wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote ni mchakato unaokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Papa UNESCO

 

 

03 July 2021, 14:52