Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani unanogeshwa na kauli mbiu "Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote" Mt 28:20. Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani unanogeshwa na kauli mbiu "Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote" Mt 28:20. 

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya Kwanza ya Wazee na Wajukuu 2021

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani ni fursa kwa wao kudemka kwani maisha yataka matao! Papa anagusia kuhusu: Upweke hasi, janga la UVIKO-19; faraja kutoka kwa vijana na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na waja wake. Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema. Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii husika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Wazee ni amana na utajiri wa jamii, wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii. Wazee wamapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa mwaka 2021 anasema, Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani ni fursa kwa mababu, mabibi na wajukuu wao kudemka kwani maisha yataka matao! Upweke hasi, janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; faraja kutoka kwa vijana na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na waja wake.

Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii ili kuweza kuurithisha kwa kizazi kipya pamoja na kuwalinda vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani ili wasijikwae na hatimaye kukengeuka! Wazee hata katika uzee wao, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi kieleweke kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Wazee na vijana wanahitajiana, ili kukamilishana katika hija ya maisha yao na hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake. Baba Mtakatifu anawataka mababu, mabibi na wazee katika ujumla wao kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono” Yoe 2: 28-32.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wazee kwamba, Kanisa liko karibu na pamoja nao! Kanisa linawapenda, linawalinda na kuwatunza na kamwe halitaki kuwaacha wazee kutumbukia katika upweke hasi. Janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limepukutisha maisha ya wazee wengi sehemu mbalimbali za dunia. Wengine wamewapoteza wapendwa wao, kiasi kwamba kufumba na kufumbua wakajikuta wako pweke! Baadhi ya wazee imewabidi kukaa karantini kwa muda mrefu sana. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa akina Joakim na Anna ambao hawakubahatika kupata mtoto mapema, kiasi cha kuonekana kama wageni na watu wasiofaa kwa majirani zao. Lakini hatimaye, Mwenyezi Mungu akasikia sala yao ya muda mrefu. Malaika wa Bwana akaja na kuwafariji na kuwahakikishia kwamba, “Daima yuko pamoja nao”. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 litapita na watu wataanza kuwatembelea na kuwafariji na maisha yatarejea katika hali yake ya kawaida.

Kwa wakati huo, Malaika watakuwa na nyuso za wajuu wao, ndugu, jamaa na majirani. Huu ndio umuhimu wa upendo wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Hata hivyo, kutokana na maambukizi makubwa ya UVIKO-19 kuna nchi ambazo wananchi wake hawaruhusiwi kuwatembelea wazee kwenye nyumba za wazee. Kumbe, Baba Mtakatifu anawahimiza wazee kusali na kutafakari Neno la Mungu ili kufahamu mpango wa Mungu katika maisha yao. Wazee waendelee kusali kwa ajili ya kuombea watenda kazi katika shamba lake. Wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu ni wa milele na yuko daima pamoja nao na wala hawezi kwenda kula pensheni. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu waliotumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, hata wazee nao wamepewa dhamana na wajibu wa kulinda na kutunza mizizi ya imani, ili kuwarithisha vijana wa kizazi kipya pamoja na kuwatunza. Wazee wakumbuke kwamba, wakati wote wa maisha yao wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, wawakabidhi na kuwarithisha wajukuu wao mila za wazee zilizo njema. Bila shaka wazee watakuwa na maswali mengi ya kujiuliza, lakini watambue kwamba, Roho Mtakatifu atawapatia majibu muafaka.

Watu wa Mungu wanapaswa kupita janga la maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 wakiwa wamebadilika na kamwe wasibaki katika ile hali ya kwanza. Watu wanahitajiana ili kukamilishana na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kujiokoa mwenyewe, kwani wote ni ndugu! Wazee ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, ili kupambana kikamilifu na changamoto kwa sasa na kwa siku za usoni. Wazee wanaweza kusaidia kufikia lengo hili kwa kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha yaani: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono” Yoe 2: 28-32. Matumaini ya ulimwengu ujao yanasimikwa katika Agano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Vijana wanapaswa kutekeleza ndoto ya wazee. Hii ni ndoto inayosimikwa katika misingi ya: haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mwelekeo huu unawawezesha vijana wa kizazi kipya kuwa na dira ili kwa pamoja kuweza kujenga ulimwengu ujao, kwa kuunganisha uzoefu, mang’amuzi na magumu ya maisha. Wazee wamekula chumvi nyingi na wamepitia mengi katika maisha, kumbe, wanaweza kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya ili kuweka msingi thabiti kwa siku za usoni!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndoto hizi zinafumbatwa katika Kumbukumbu, kwa kutambua madhara na machungu ya vita, ili vijana wa kizazi kipya waweze kujifunza kulinda, na kudumisha tunu ya amani duniani. Wazee waendelee kupyaisha kumbukumbu zao sanjari na kuwashirikisha wengine kama sehemu ya utume wa wazee, kwani kumbukumbu ni sehemu ya maisha. Kuna wazee ambao walilazimika kuyakimbia makazi na nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Hata leo hii bado kubwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wanaotamani kuona leo na kesho iliyo bora zaidi. Baadhi ya watu hawa leo hii wanaendelea kutoa huduma kwa wazee sehemu mbalimbali za dunia. Kumbukumbu safi za namna hii, zinaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa ulimwengu wa kibinadamu unaosimikwa katika fadhila ya ukarimu. Kumbe, kumbukumbu inahitajika katika ujenzi, lakini bila msingi imara hakuna kitakachoweza kufanikiwa. Msingi wa maisha ni kumbukumbu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema nguzo ya tatu ni Sala na kwamba, Sala ya wazee ina nguvu kiasi hata cha kuweza kuulinda ulimwengu. Ni maneno yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, ambaye hata katika uzee wake, bado anaendelea kusali na kuliombea Kanisa. Wazee wanapaswa kukumbuka kwamba, sala yao ni rasilimali muhimu sana katika maisha na kwamba, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, unahitaji sala ya wazee, ili kuweza kupata msukumo mpya wa kimisionari. Yaani vipindi vya kuabudu, kutafakari na sala kwa kuondokana na ubinafsi hasa katika nyakati hizi ngumu ambamo bado janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona linaendelea kutishia maisha. Sala za wazee ni muhimu sana, ili kuleta amani na utulivu ili watu wote waweze kufika bandarini salama salimini. Ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika huduma kama ilivyokuwa kwa Charles de Foucald, ambaye anatarajiwa kutangazwa kuwa ni Mtakatifu hivi karibuni. Watu wa Mungu wajenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, ili wote katika ukweli waweze kuwa ni ndugu wamoja! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake katika maadhimisho ya Siku ya kwanza ya wazee na wajukuu kwa kusema: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20.

Papa Wazee

 

 

22 July 2021, 15:20