Tafuta

Baba Mtakatifu ametunga sala maalum kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wazee. Baba Mtakatifu ametunga sala maalum kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wazee. 

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani 2021: Sala Maalum Kwa Wazee!

Baba Mtakatifu Francisko katika video ya sala kwa ajili ya Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani yumo pia Askofu Laurent Noèl, mwenye umri wa miaka 101 na historia inaonesha kwamba, huyu ndiye Askofu mwenye umri mkubwa zaidi duniani! Hii ni sala ya kusifu, kushukuru na kuomba tena ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu katika safari ya maisha ya hapa duniani kwa imani zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Ujumbe wa Baba Mtakarifu katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Wazee ni amana na utajiri wa jamii, wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii. Wazee wamapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko katika video ya sala kwa ajili ya Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani yumo pia Askofu Laurent Noèl, mwenye umri wa miaka 101 na historia inaonesha kwamba, huyu ndiye Askofu mwenye umri mkubwa zaidi duniani!  

SALA YENYEWE: Ninakushukuru Ee Mungu Baba Mwenyezi kwa faraja na uwepo wako wa daima; hata katika kipindi cha upweke, kwa sababu wewe ni tumaini na tegemeo langu, mwamba na ngome ya maisha yangu tangu ujana wangu. Ninakushukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia familia sanjari na kunikirimia maisha marefu. Ninakushukuru kwa nyakati zile za furaha na ugumu wa maisha; ninakushukuru kwa ndoto ambazo zimetekelezeka katika maisha yangu na zile ambazo bado ziko mbele yangu. Ee Mungu Mwenyezi ninakushukuru kwa muda huu ambao unapyaisha matunda ya wito wangu.

Ninakuomba Ee Mungu Baba Mwenyezi uniongezee imani, unifanye niwe chombo chako cha amani; unifundishe kuwapokea na kuwakumbatia wale wote wanaoteseka zaidi yangu na kamwe nisiache kuota ndoto na kuwasilimulia vijana wa kizazi kipya matendo yako makuu. Mlinde na kumwongoza Baba Mtakatifu Francisko na Kanisa, ili mwanga wa Injili uweze kufika hadi miisho ya dunia. Mpeleke Roho wako Mtakatifu ili aweze kuigeuza sura ya dunia; ili dhoruba ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 liweze kutulia, maskini wafarijike na vita ikome! Ee Mungu wangu uniinue katika unyonge na udhaifu wangu; unisaidie niweze kuishi katika ukamilifu wake, kila dakika unayonijalia katika maisha, nikiwa na uhakika kwamba, wewe upo pamoja nami siku zote, hata ukamilifu wa dahari. Amina.

Sala Maalum
23 July 2021, 16:00