Tafuta

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa niaba ya Papa Francisko, Siku ya kwanza ya Wazee na Wajukuu Duniani. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa niaba ya Papa Francisko, Siku ya kwanza ya Wazee na Wajukuu Duniani. 

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani 2021: Mahubiri ya Papa Francisko!

Hata leo hii Yesu anataka kuzima njaa ya maisha, upendo na furaha ya kweli. Anaangalia kwa makini na kuchunguza yale ambayo waja wake wameyabeba nyoyoni mwao: mateso, uchovu na matumaini. Mbele ya Mungu, kila mtu anayo thamani ya pekee na wala hakuna mkutano mkuu. Kristo Yesu analo jicho la tafakuri linaloweza kuzama katika undani wa maisha ya mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 umenogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria ambayo yanaadhimishwa tarehe 26 Julai 2021. Hii ni ahadi ya uwepo endelevu na fungamani wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Sehemu kubwa ya waamini waliohudhuria Ibada hii ya Misa takatifu ni kutoka Jimbo kuu la Roma, hasa wale wanaojishughulisha kwa karibu zaidi na huduma kwa wazee. Kundi la pili, ni wazee waliokuwa wameandama na wajukuu wao kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya Injili ya uhai, inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa walimwengu dhidi ya utamaduni wa kifo unaowabeza na kuwatweza wazee katika jamii.

Kwa mara ya kwanza kabisa, wazee ambao kwa miaka mingi wamekaa katika nyumba za kutunzia wazee, wamepata “mtoko na kwenda kuosha macho” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Vijana wa kizazi kipya wanaohamasishwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na wazee kwani wazee wana ndoto na vijana wana unabii nao wamehudhuria! Ibada ya Misa takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya ambaye amewaambia waamini waliohudhuria katika Ibada hii ya Misa takatifu kwamba, kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu bado anaendelea na mapumziko baada ya kufanyiwa operesheni kubwa. Kumbe, bado anahitaji muda wa kupumzika ili aweze kupona vizuri zaidi na hatimaye, kurejea kwenye shughuli zake za kichungaji akiwa na afya tele kabisa! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yaliyosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, amekazia mambo makuu matatu: kuona, kushirikishana na kuhifadhi.

Baba Mtakatifu anasema, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 17 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa na kwa namna ya pekee katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, akimwonesha Kristo Yesu akiwashibisha mkutano mkuu kwa mikate mitano ya shayiri na samaki wawili na vipande vilivyobakia, vilikusanywa, ili kisipotee chochote. Rej. Yn 6:1-15. Kristo Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake. Hiki ni kielelezo makini cha Kristo Yesu anayeona na kuwahurumia watu hawa waliokuwa wamechoka pamoja na kuelemewa na njaa na kiu. Hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuzima njaa ya maisha, upendo na furaha ya kweli. Anaangalia kwa makini na kuchunguza yale ambayo waja wake wameyabeba nyoyoni mwao: mateso, uchovu na matumaini. Mbele ya Mwenyezi Mungu, kila mtu anayo nafasi na thamani ya pekee na wala hakuna mkutano mkuu. Kristo Yesu analo jicho la tafakuri linaloweza kuzama katika undani wa maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hili ndilo jicho ambalo wazee wanalo katika maisha ya mwanadamu. Tangu utotoni wamejizatiti kuwalinda watoto na wajukuu wao, kwa imani na upendo thabiti. Ni watu ambao walikuwa ni mwamba na ngome salama wakati ambapo wajukuu wao walipokuwa wanajisikia kutofahamika, wakiogopa changamoto za maisha! Wao wakawa wakwanza kuwakimbilia na kuwapokea kwa faraja, huku wakipangusa machozi yaliyokuwa yamefichika machoni na ndoto iliyokuwa imezama moyoni! Ni kwa njia ya huruma na upendo wa wazee, leo hii wale waliokuwa watoto sasa ni watu wazima na wanajitegemea wenyewe! Jambo la kujiuliza, mara ya mwisho kuonana, kuwatembelea au kuongea na bibi na babu ilikuwa ni wakati gani? Je, wajukuu wameweza kuonesha ukaribu na ujirani mwema? Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, anaumia sana moyoni mwake kuona jinsi watu wanavyofanya mambo kwa haraka, kiasi kwamba, hawana hata muda wa kusimama kidogo, kuangalia, kusalimia na kufariji kwa upendo. Inaogofya kuona jamii ambayo watu wote wanaonekana kama mkutano mkuu na wala watu hawana nafasi tena ya kutaka kufahamiana.

Wazee waliorutubisha maisha ya watoto wao, wana kiu ya kuwaona wajukuu wao, wakiwatunza na kuwaonesha upendo wa dhati. Wazee wanataka kusikia uwepo wa vijana, changamoto kwao ni kuinua macho ili kuwaangalia wazee kama anavyofanya Kristo Yesu katika maisha yao! Kristo Yesu baada ya kugundua njaa na kiu waliyokuwa nayo, akaamua kuwalisha kwa mikate mitano na samaki wawili na wakala watu waume wapatao elfu tano. Kijana anawekwa mbele ya mkutano mkuu kama kielelezo cha wema, ukarimu na upendo wa Mungu. Kijana anayethubutu kuwashirikisha wengine ukarimu kwa kile kidogo alichokuwa nacho! Leo hii kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano mapya kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, ili kushirikishana amana na utajiri wa maisha, ili waweze kuota ndoto ya pamoja, kwa kuvuka kinzani na mipasuko kati ya kizazi na kizazi, tayari kujiandaa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Bila ya mwelekeo huu mpya wa maisha, matamanio hayo halali yatakufa kwa baa la njaa kutokana na kuongezeka kwa upweke hasi; uchoyo na ubinafsi, nguvu za ubaguzi na utengano. Ubinafsi ni hatari katika maisha ya kijamii. Injili inatoa mwaliko kwa waamini kushirikishana jinsi walivyo na kile walicho nacho; yaani vijana na wazee wanaweza kushikamana. Kwani wazee wana ndoto na vijana wana unabii. Vijana ni manabii wa siku za usoni, lakini wazee ni chimbuko la historia na kamwe hawezi kuchoka kuendelea kuota ndoto na kurithisha uzoefu na mang’amuzi yao kwa vijana wa kizazi kipya, bila kuwa ni kizingiti kwa maisha yao ya mbeleni! Kumbe, hii ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kushikamana na wazee na iwe hivyo pia kwa jamii na Kanisa katika ujumla wake. Injili inabainisha kwamba, nao waliposhiba, wanafunzi wa Yesu wakakusanya vipande vilivyobakia ili kisipotee chochote. Mwenyezi Mungu anawajalia waja wake mahitaji msingi ya maisha, lakini hapendi kuona kitu chochote kila kinapotea. Katika ulimwengu mamboleo asiwepo mtu awaye yote anayetelekezwa au kutwezwa.

Ni wakati wa kusimama kidete kukusanya, kutunza na kuhudumia kwa upendo. Wazee ni watu wanaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii kwani ni hazina, amana na utajiri mkubwa, kwa sababu ndani mwao wanatunza kumbukumbu! Bila mizizi ya kumbukumbu hii, mwanadamu si mali kitu! Ni wajibu wa jamii kulinda maisha ya wazee, kwa kuwarahisishia matatizo na changamoto za maisha. Ni wakati wa kusikiliza, kujibu na kuwatekelezea mahitaji yao msingi, ili kamwe wasielemewe na upweke hasi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiuliza ni lini wamewatembelea babu na bibi zao; wamejenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza, kujibu na kuwatimizia mahitaji yao? Wazee wanapaswa kulindwa ili maisha na ndoto zao, ziweze kuendelea, ili kwa siku za mbeleni, asiwepo mtu anayejuta kwa kuwa alishindwa kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kwa watu waliowapenda upendo na kuwakirimia zawadi ya maisha! Wazee ni sawa na chakula kinachotoa lishe ya maisha, kwa sababu wamewalea na kuwalinda; wakawaonjesha huruma na upendo. Katika magumu wakawa ni faraja kwao. Hawa ni watu wakuheshimiwa na kufurahi pamoja nao, changamoto na mwaliko wa kushirikishana muda uliopo. Vijana wa kizazi kipya na wazee kwa pamoja washirikiane na kushikamana, ili wote kwa pamoja waweze kuwa ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Papa Mahubiri
25 July 2021, 15:17