Tafuta

Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inaadhimishwa tarehe 25 Julai 2021: Wahusika wakuu ni wazee, wajukuu na vijana wa kizazi kipya. Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inaadhimishwa tarehe 25 Julai 2021: Wahusika wakuu ni wazee, wajukuu na vijana wa kizazi kipya. 

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani 2021: Ibada ya Misa Mjini Vatican!

Sehemu kubwa ya waamini ni wale wana wanaojishughulisha kwa karibu zaidi na huduma kwa wazee. Kundi la pili, ni wazee watakaokuwa wameandama na wajukuu wao kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya Injili ya uhai, inayopaswa kushuhudiwa kwa walimwengu dhidi ya utamaduni wa kifo unaowabeza na kuwatweza wazee katika jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani Jumapili tarehe 25 Julai 2021, unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika taarifa yake kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii linabainisha kwamba, Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho haya itaanza Jumapili saa 4:00 Asubuhi kwa Saa za Ulaya, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Sehemu kubwa ya waamini ni wale wanaotoka Jimbo kuu la Roma na wanaojishughulisha kwa karibu zaidi na huduma kwa wazee. Kundi la pili, ni wazee watakaokuwa wameandama na wajukuu wao kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya Injili ya uhai, inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa walimwengu dhidi ya utamaduni wa kifo unaowabeza na kuwatweza wazee katika jamii. Kwa mara ya kwanza kabisa, wazee ambao kwa miaka mingi wamekaa katika nyumba za kutunzia wazee, watapata nafasi ya “kuosha macho” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Ibada hii inahudhuriwa pia na vijana wa kizazi kipya wanaohamasishwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na wazee kwani wazee wana ndoto na vijana wana unabii kama ambavyo anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Wazee Duniani iwe ni fursa ya kuboresha mahusiano haya ya kifamilia, kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wazee, ambao wanayo mengi ya kuwafundisha na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazee ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, ili kupambana kikamilifu na changamoto kwa sasa na kwa siku za usoni.

Wazee wanaweza kusaidia kufikia lengo hili kwa kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha yaani: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. Matumaini ya ulimwengu ujao yanasimikwa katika Agano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Vijana wanapaswa kutekeleza ndoto ya wazee. Hii ni ndoto inayosimikwa katika misingi ya: haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mwelekeo huu unawawezesha vijana wa kizazi kipya kuwa na dira ili kwa pamoja kuweza kujenga ulimwengu ujao, kwa kuunganisha uzoefu, mang’amuzi na magumu ya maisha. Wazee wamekula chumvi nyingi na wamepitia mengi katika maisha, kumbe, wanaweza kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya ili kuweka msingi thabiti kwa siku za usoni! Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndoto hizi zinafumbatwa katika Kumbukumbu, kwa kutambua madhara na machungu ya vita, ili vijana wa kizazi kipya waweze kujifunza kulinda, na kudumisha tunu ya amani duniani. Wazee waendelee kupyaisha kumbukumbu zao sanjari na kuwashirikisha wengine kama sehemu ya utume wa wazee, kwani kumbukumbu ni sehemu ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema nguzo ya tatu ni Sala na kwamba, Sala ya wazee ina nguvu kiasi hata cha kuweza kuulinda ulimwengu.

Ni maneno yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, ambaye hata katika uzee wake, bado anaendelea kusali na kuliombea Kanisa. Wazee wanapaswa kukumbuka kwamba, sala yao ni rasilimali muhimu sana katika maisha na kwamba, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, unahitaji sala ya wazee, ili kuweza kupata msukumo mpya wa kimisionari. Yaani vipindi vya kuabudu, kutafakari na sala kwa kuondokana na ubinafsi hasa katika nyakati hizi ngumu ambamo bado janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona linaendelea kutishia maisha. Sala za wazee ni muhimu sana, ili kuleta amani na utulivu ili watu wote waweze kufika bandarini salama salimini. Ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika huduma. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linayahimiza Majimbo, Parokia na Vigango na Taasisi mbalimbali kuhakikisha kwamba, zinaadhimisha Siku hii kwa kishindo kama sehemu mwendelezo wa sera na mikakati ya Mama Kanisa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Siku ya Wazee Duniani
23 July 2021, 15:35