Tafuta

Tarehe 30 Julai 2021 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Tarehe 30 Julai 2021 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. 

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara ya Binadamu 2021

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu tarehe 30 Julai 2021, anapenda kutoa wito kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya mageuzi makubwa kutoka katika uchumi wa biashara ya binadamu na kuingia katika uchumi wa huduma kwa waathirika. Mtandao wa "Talita Kum" unaendesha kampeni nzito sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2021 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo duniani. Siku hii ilianzishwa na Umoja wa Mataifa ili kusaidia juhudi za kimataifa za kuragibisha athari za biashara hii katika maisha na utu wa binadamu. Maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Waathirika, sauti inayoonesha njia.” Hapa kuna umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kujibu kilio cha waathirika. Hawa ni watu muhimu sana katika mapambano dhidi ya biashara na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza katika kuzuia, kutambua na kuwasaidia waathirika, katika mchakato wa maboreso ya afya na maisha yao. Waathirika hawana budi kuvuka kiwango cha ujinga na hali ya kutoeleweka ili waweze kupatiwa msaada zaidi. Historia na mang’amuzi ya waathirika ni muhimu sana katika kutengeneza sera na mbinu mkakati wa kupambana na janga hili linaloendelea kusababisha maafa makubwa ya watu sehemu mbalimbali za dunia! Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya viungo vya binadamu.

Watoto wanafanyishwa kazi ngumu majumbani na hata wakati mwingine kuolewa wakiwa na umri mdogo, yaani kutumbukizwa kwenye ndoa za shuruti! Kuna watoto wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo wakati wa vita na machafuko ya kisiasa na kijamii! Wote hawa ni waathirika wa utumwa mamboleo unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Kutokana na changamoto zote hizi, kunako mwaka 2015, Kanisa lilianzisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu Duniani, changamoto iliyovaliwa njuga kwa namna ya pekee na Mtandao wa “Talita Kum”. Huu ni mtandao wa Mashirika ya Kitawa Kimataifa unaoshirikiana bega kwa bega na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Unashirikiana na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Wadau wengine ni Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, lililoanzishwa kunako mwaka 1910, pamoja na Tume ya Haki na Amani ya Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, nchini Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu kwa mwaka 2021, anapenda kutoa wito kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya mageuzi makubwa kutoka katika uchumi wa biashara ya binadamu na kuingia katika uchumi wa huduma kwa waathirika. Mtandao wa “Talita Kum” unatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 70 duniani. Mtandao ukipewa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu; kwa kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na hivyo sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema haya ni mapambano ya kiuchumi, lakini vita hii zaidi ni ya kimaadili, kwani wafanyabiashara hawa wanatumia umaskini kunyanyasa utu na heshima ya binadamu! Huu ni wakati wa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa wale wote wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuunganisha nguvu ili kupambana na uhalifu huu dhidi ya ubinadamu, kwani unatishia tunu msingi za maisha ya kijamii, ulinzi na usalama; uchumi pamoja na mafungamano ya kijamii! Mtandao wa “Talita Kum” katika mchakato wa maadhimisho haya, umechapisha shuhuda mbalimbali zinazoonesha umuhimu wa kujielekeza zaidi katika uchumi wa huduma kwa waathirika akama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika elimu bora; kutengeneza fursa za ajira pamoja na kuwapatia watu vibali vya kusafiria. Jamii iendelee kuwekeza zaidi katika sekta ya afya, pamoja na kuwasaidia kisaikolojia waathirika wa biashara na mifumbo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Mtandao wa “Talita Kum” umeendelea kuwa ni msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya biashara na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB katika maadhimisho haya linasema kwamba, maisha ya binadamu yana thamani kubwa. Kwa muda wa juma zima, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kwa kushirikiana na “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM.), Chama cha Kutetea Wanawake, Watoto na Vijana (ASBRAD) limeendesha kampeni ya juma zima na kilele chake ni tarehe 30 Julai 2021. Kampeni hii imeingia katika awamu ya tano na imeendeshwa kwa njia ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii nchini Brazil. Wajumbe wamepembua kwa kina na mapana dhana ya biashara ya binadamu na viungo vyake. Waathirika wakubwa wa biashara hii ni wanawake, wasichana na watoto. Takwimu kutoka Brazil zinaonesha kwamba kumekuwepo na ongezeko la waathirika wa biashara ya binadamu nchini Brazil kutokana na athari kubwa za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Na waathirika wakuu ni watoto. Hii ni kutokana na kupungua kwa shughuli za uzalishaji, huduma pamoja na watu kulazimika kukaa karantini kwa muda mrefu. Makundi ya uhalifu kitaifa na kimataifa yakatumia mwanya huu kujitafutia mapato haramu!

Biashara ya Binadamu
30 July 2021, 16:10