Tafuta

Wadau wa tasnia ya mawasiliano duniani wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho na umoja wa kitaifa. Wadau wa tasnia ya mawasiliano duniani wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho na umoja wa kitaifa. 

Waandishi Wa Habari: Vyombo Vya Upatanisho na Umoja wa Kitaifa!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la 12 la Mawasiliano nchini Brazil linalowaunganisha wadau mbalimbali kutoka katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho na umoja wa Kitaifa katika nchi ya Brazil ambayo imegawanyika sana kutokana na sababu mbalimbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, kuna uwezekano mkubwa wa kukumbana na habari za kughushi na kupotosha. Lakini, kwa wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa, wanapaswa kujizatiti kutafuta: ukweli na kuufanya ufahamike, huku ukinogeshwa zaidi na kauli mbiu: haki, uaminifu na habari. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa vinapaswa kuwa ni jukwaa la majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa linahitaji vyombo vya mawasiliano vitakavyowasaidia watu na hasa vijana wa kizazi kipya kujenga na kukuza dhamiri nyofu, ili kutambua mema ya kufuata na mabaya ya kuyaacha. Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie kukomaza maamuzi makini yanayokita mizizi yake katika ukweli sanjari na kutambua umuhimu wa kuendelea kufanya kazi ili kudumisha haki, maridhiano ya kijamii, kwa kuheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wadau wa tasnia ya mawasiliano waendelee kutekeleza huduma yao katika ukweli, unyenyekevu na uwajibikaji mkubwa kwa sababu wao ni kioo cha jamii!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la 12 la Mawasiliano nchini Brazil “Mutirão de Comunicação” linalowaunganisha wadau mbalimbali kutoka katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho na umoja wa Kitaifa katika nchi ya Brazil ambayo imegawanyika sana kutokana na sababu mbalimbali. Kongamano hili limenogeshwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya mawasiliano fungamani, binadamu katika njia mpya za mawasiliano ya mazingira”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Waamini wanaalikwa kuwa ni alama ya matumaini na mshikamano wa kibinadamu. Kristo Yesu amewahakikishia wafuasi wake akisema, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28: 20. Dhamana na utume wa Wakrisro nchini Brazil ni kuhakikisha kwamba, kwa hakika wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja wa kitaifa sanjari na upatanisho.

Ni katika muktadha huu, Wakristo katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwa mstari wa mbele kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu. Wajitahidi kuwa kweli ni vyombo vya majadiliano vinavyokita mizizi yake katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu aliwahi kusema kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wana uwezo wa kushirikisha kile kilicho: kweli, chema na kizuri ili kuweza kuunda kumbukumbu ya kihistoria pamoja na kuelewa matukio mbalimbali yanayomzunguka mwanadamu. Lakini kutokana na ubinafsi, mwanadamu amejikuta akiharibu uwezo wake wa kuwasiliana na wengine, hali ambayo inapata chimbuko lake hata kutoka katika Maandiko Matakatifu. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, leo hii mwanadamu anakumbana na bahari ya habari za kughushi, dhana ambayo imetendewa kazi hata na Mapapa waliotangulia ambao wamewataka wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kusimama kidete kupinga habari za kughushi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na weledi wa uandishi wa habari kwa wanahabari wenyewe kuwajibika kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia ukweli!

Habari za kughushi anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni habari tenge inayojikita katika takwimu zilizochakachuliwa au hata zile ambazo hazipo kabisa, ili kumwadaa msomaji au mtazamaji. Lengo ni kutoa ushawishi katika maamuzi ya kisiasa ili kulinda na kudumisha zaidi mafao ya kiuchumi. Kwa haraka haraka habari za kughushi zinaonekana kuvutia sana na kugusa hisia za watu wengi kwani zinajikita katika maamuzi mbele yanayotolewa na jamii kutokana na chuki, hasira na hali ya kuchanganyikiwa. Habari za kughushi husambaa kwa haraka sana kama moto wa mabua, kiasi hata uwezo wa vyombo husika kukanusha, vinakuwa haviwezi kufua tena dafu! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuwa makini dhidi ya habari za kughushi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani ndiyo habari ya kweli inayomlenga mtu mzima ili kumjengea uwezo wa kusikiliza, kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa kuvutwa na: ukweli, wema na uzuri ili hatimaye, kuwajibika barabara.

Wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanao wajibu na utume mzito wa kulinda ukweli wa habari kwa kutambua kwamba, mlengwa mkuu ni binadamu. Habari inalenga kuwaunda watu wengine katika jamii, kugusa maisha yao ili kudumisha wema na uaminifu unaofungua njia ya umoja na amani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kongamano hili umesomwa na Askofu mkuu Walmor Oliveira de Azevedo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil. Washiriki wa kongamano hili, pamoja na mambo mengine, wamejadili kuhusu mahusiano ya kidigitali na hali halisi ya maisha ya mwanadamu; changamoto za ulimwengu wa kidigitali katika maisha na utume wa Kanisa nchini Brazil. Ushawishi wa njia za mawasiliano ya kidigitali katika maisha ya waamini katika mwanga wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Imekuwa ni fursa kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ndani ya Kanisa kupyaisha tena sera na mikakati ya mawasiliano ndani ya Kanisa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wajumbe kwa namna ya pekee kabisa wamekazia umuhimu wa vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa visimamie: ukweli, uwazi, ubora, maadili na utu wema kama sehemu ya utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo!

Mawasiliano Brazil
27 July 2021, 14:57