Tafuta

Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kigaidi yaliyotokea kwenye soko la al Wuhailat mjini Baghdad. Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kigaidi yaliyotokea kwenye soko la al Wuhailat mjini Baghdad. 

Papa Asikitishwa na Mauaji Kwenye Soko la Al Wuhailat, Iraq!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, hakuna vitendo vyovyote vya kigaidi na ghasia zitakazofifisha juhudi na jitihada za kutaka kujikita katika upatanisho wa kitaifa, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu nchini Iraq. Anawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na shambulizi hili la kigaidi kwenye soko la Al Wuhailat.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Waamini wa dini ya Kiislam hutumia Eid ul-Adha kusherehekea utiifu kamili wa Nabii Ibrahimu kwa Amri ya Mwenyezi Mungu na kuwakumbusha wenyewe kuwa tayari kutoa kafara chochote ili kutimiza maagizo ya Mwenyezi Mungu katika mchakato wa kumfuasa! Hii ni siku ile Nabii Ibrahimu alipotaka kumtoa kafara mwanaye Ishmael kama alivyokuwa amemriwa na Allah, lakini badala yake akapewa kondoo na Mwenyezi Mungu ili amtoe kafara badala yake! Sikukuu ya Eid ul-Adha huadhimishwa kuanzia siku ya 10 tangu kuonekana kwa mwezi wa Dhul Hijjah. Ni katika hali na mazingira haya ya wananchi wa Iraq kujiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Sikukuu ya Eid ul-Adha, wakiwa kwenye Soku kuu al-Wuhailat mjini Baghdad, wakati bomu la kujitoa mhanga lililolipuka na kusababisha zaidi ya watu 30 kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa, Jumatatu tarehe 19 Julai 2021.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na vitendo hivi vya kigaidi vinavyohatarisha amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Mitja Leskovar, Balozi wa Vatican nchini Iraq anasema, anapenda kutoa salam zake za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huu mzito. Anawaombea kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awajalie moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi. Wale waliofariki dunia, wapate usingizi wa amani na pumziko la milele. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, hakuna vitendo vyovyote vya kigaidi na ghasia zitakazofifisha juhudi na jitihada za kutaka kujikita katika upatanisho wa kitaifa, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu nchini Iraq.

Wakati huo huo, Bwana António Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameshutumu na kulaani vikali mashambulizi haya ya kigaidi. Anapenda kuchukua nafasi hii, kutoa salam zake za rambirambi kwa Serikali na wananchi wa Iraq katika ujumla wake. Anawaombea wale waliojeruhiwa katika shambulio hili waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao kama kawaida. Shambulizi hili la kigaidi katika makesha ya Sikukuu ya Eid ul-Adha ni angalisho kwa watu wote kwamba, vitendo vya kigaidi havina mpaka. Ni matumaini ya Umoja wa Mataifa kwamba, wahusika watasakwa kwa ud ina uvumba, ili hatimaye waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama nchini Iraq na hivyo sheria kuchukua mkondo wake. Watu wengi waliopoteza maisha ni wanawake na watoto. Hii ni changamoto kwa watu wote wa Mungu nchini Iraq kushirikiana na kushikamana kwa pamoja katika kulinda, kudumisha na kujenga misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Rambirambi

 

 

21 July 2021, 15:16