Tafuta

Katekesi za Papa Francisko kwa Mwezi Julai Zimesitishwa hadi Jumatano tarehe 4 Agosti 2021. Katekesi za Papa Francisko kwa Mwezi Julai Zimesitishwa hadi Jumatano tarehe 4 Agosti 2021. 

Katekesi za Papa Zimesitishwa Kwa Mwezi Julai hadi 4 Agosti 2021

Katika kipindi chote cha Likizo ya Kiangazi kwa Mwaka 2021 yaani mwezi wa Julai, hakutakuwa na Katekesi kwa siku za jumatano kama ilivyozoeleka. Baba Mtakatifu atarejea tena uringoni kwa ajili ya katekesi Jumatano tarehe 4 Agosti 2021. Kama kawaida ataendelea kutoa tafakari za Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican! Tupo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi chote cha Likizo ya Kiangazi kwa Mwaka 2021 yaani mwezi wa Julai, hakutakuwa na Katekesi kwa siku za jumatano kama ilivyozoeleka. Baba Mtakatifu atarejea tena uringoni kwa ajili ya katekesi Jumatano tarehe 4 Agosti 2021. Kama kawaida ataendelea kutoa tafakari za Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu, baada ya kumaliza Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, hivi karibuni ameanza Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Waraka Wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Ni Waraka unaowawezesha waamini kumfahamu zaidi Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa na tema msingi katika maisha na utume wake, zinazoremba uzuri wa Injili. Katika Waraka huu, Mtume Paulo anakazia toba na wongofu wa ndani na jinsi alivyoyasadaka maisha yake kwa ajili ya huduma ya Injili na Kristo Yesu. Anazungumzia mambo msingi katika imani kwa kujikita zaidi kuhusu: uhuru na neema ya kuishi kikamilifu kama Mkristo. Huu ni Waraka unaogusa mambo tete na nyeti hata katika nyakati hizi, kana kwamba, ni Waraka ulioandikwa kwa ajili ya waamini katika mapambazuko ya Millenia na Tatu ya Ukristo.

Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anatoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu uliomwezesha kutembelea Jumuiya ya Wagalatia walau mara mbili, wakati wa safari zake za kimisionari. Kuna mambo mengi ambayo hayana majibu ya moja kwa moja. Paulo alikuwa ni Mtume kweli kweli na wala si “Mtume wa Kuchonga” au “Feki”. Anuani, msingi na muhtasari wa Injili ya Paulo unabubujika kutoka katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu: “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia; Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu… Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba nililitesa Kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu… Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake…” Gal 1:1.13.15-16.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Likizo ya Kipindi cha Kiangazi kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia ni muda muafaka wa kujipatia nafasi ya kupumzika: kimwili na kisaikolojia, ili kujipatia tena nguvu za kuweza kusonga mbele katika mapambano ya maisha ya kila siku. Ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani, ukuu na uweza wake kutokana na kazi kubwa ya uumbaji na ukomnbozi. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anayo kila sababu ya kulinda, kutunza na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwani kimsingi, mazingira bora na safi ni ufunuo wa: nguvu, wema, ukuu na utakatifu wa Mungu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani: “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiikolojia. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu kwa sababu mazingira bora ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya maisha ya binadamu.

Huu ndio ule muda uliokubalika wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kumfuasa Kristo Yesu bila woga! Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Likizo ni muda muafaka wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Likizo ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Likizo si wakati wa kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu kwani hii, ni hatari kubwa sana!

Likizo ya Kiangazi
03 July 2021, 15:32