Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete dhidi ya kashfa ya baa la njaa, ukosefu wa maji safi na salama pamoja na tiba bora hasa kwa maskini duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete dhidi ya kashfa ya baa la njaa, ukosefu wa maji safi na salama pamoja na tiba bora hasa kwa maskini duniani. 

Papa Francisko Kashfa ya Baa la Njaa, Ukosefu wa Maji Safi na Tiba!

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yameendelea kusababisha uharibifu kwa mazingira na ukame kwa maisha ya kiroho. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuzalisha chakula kingi na cha kutosha mahitaji ya watu, lakini kwa bahati mbaya bado kuna umati mkubwa wa watu unaopekenywa kwa baa la njaa duniani. Hii ni kashfa inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora ili kupambana na mazingira yao, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani. Ni wajibu kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza sauti ya viongozi wa kidini kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema amana na utajiri wao wa maisha ya kiroho kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii inatokana na ukweli kwamba, mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu unategemea na kufungamana na masuala kama: Udugu wa kibinadamu, haki na uaminifu kati ya watu.

Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa unakazia mambo makuu matano: Watu, Mazingira, Ustawi, Maendeleo na Ushirikishwaji! Malengo ya kiuchumi na kisiasa hayana budi kufumbatwa katika kanuni maadili na utu wema; wongofu wa kiikolojia na kwamba, dini zina mchango wa pekee sana katika utekelezaji wa sera na mikakati ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Serikali ya Italia kuanzia tarehe 26 hadi 28 Julai 2021 kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, inaendesha mkutano wa utangulizi wa Mifumo ya Chakula (UN Food Systems Summit, Unfss) kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Jijini New York, Marekani, mwezi Septemba 2021 kuhusu Maendeleo ya Mifumo ya Chakula mintarafu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Bwana António Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na kusomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, amekazia kuhusu changamo ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha wakati huu wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limeendelea kusababisha ukosefu wa haki na mipasuko kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kuna kilio kikubwa cha Dunia Mama kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na kilio cha maskini duniani, ambacho hakijasikilizwa kikamilifu; changamoto inayohitaji wongofu wa ndani. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yameendelea kusababisha uharibifu mkubwa kwa mazingira na ukame kwa maisha ya kiroho. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuzalisha chakula kingi na cha kutosha mahitaji ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia, lakini kwa bahati mbaya bado kuna umati mkubwa wa watu unaopekenywa kwa baa la njaa duniani. Hii ni kashfa inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kung’oa baa la njaa na utapiamlo duniani, kuna haja ya kuweka sera na mikakati ya uzalishaji na ugavi wa chakula katika vitendo zaidi kwani maneno matupu kamwe hayawezi kuvunja mfupa. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba kuna kuwepo na mabadiliko makubwa katika mifumo ya chakula duniani.

Lengo likiwa ni kudumisha uchumi wa watu mahalia, kuboresha lishe, kupunguza chakula kinachotupwa taka pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanapata lishe bora kwa afya ya miili yao. Watu wajikite zaidi katika utunzaji bora na endelevu wa mazingira sanjari na kuheshimu tamaduni za watu mahalia! Mchakato huu unapaswa kwenda sanjari na maboresho ya hali ya maisha, ili kung’oa kabisa baa la njaa duniani. Ili kuondokana na baa la njaa duniani, kuna haja kabisa kwa kuwa na mifumo mipya ya chakula, kulinda mazingira nyumba ya wote sanjari na kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu; mtu na mahitaji yake akipewa kipaumbele cha kwanza. Jumuiya ya Kimataifa ihakikishe kwamba, kunakuwepo na chakula cha kutosha, kwa kukuza kazi nzuri. Baba Mtakatifu anasema kuna haja kwa sekta ya kilimo vijijini kupewa msukumo wa pekee, ili kiweze kutosheleza mahitaji msingi ya wananchi husika. Sekta ya kilimo vijijini, ipewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati kisiasa na kiuchumi, kama njia ya kuanza kujipanga upya baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Msukumo wa pekee uwe ni kuwajengea uwezo wakulima wadogo wadogo na familia zao; sanjari na kuheshimu mila, tamaduni na desturi zao njema. Sera za uzalishaji, soko na matumizi ya pembejeo za kilimo ni muhimu katika mchakato wa maboresho ya mifumo ya chakula duniani, ili hata familia ziweze kufurahia maisha. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kuwajengea uwezo wanawake vijijini; pamoja na kuhakikisha kwamba, vijana wanapata ajira na kunakuwepo na maboresho katika sekta ya kilimo vijijini. Sera na mikakati ya kilimo itungwe ili kunogesha tunu msingi za kijamii zinazofumbatwa katika: Mafao ya wengi, mshikamano wa udugu wa kibinadamu pamoja na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana. Lengo ni kukuza na kudumisha tabia ya kuwajibika; kwa kukuza na kudumisha msingi ya haki, amani; umoja na mshikamano wa familia ya binadamu. Changamoto ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni fursa ya kukuza na kudumisha ujasiri wa majadiliano kwa kupembua mizizi inayopelekea kukosekana kwa haki katika mifumo ya chakula duniani.

Ni vyema ikiwa katika mkutano huu, wadau watajadili pia kuhusu ndoto ya walimwengu kupata chakula na lishe ya kutosha; maji safi na salama; dawa na vifaa tiba, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Vatican na Kanisa katika ujumla wake, litaendelea kujielekeza katika huduma hii makini, ili malengo yaweze kufikiwa. Kanisa litaendelea kuchangia, kuunganisha mikono na utashi, matendo na maamuzi ya busara. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kila mtu ataweza kupata mahitaji yake msingi!

Kashfa ya Njaa

 

 

27 July 2021, 15:55