Tafuta

Papa Francisko amekishukuru Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha  Agostino Gemelli kwa huduma fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Papa Francisko amekishukuru Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli kwa huduma fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. 

Papa Akishukuru Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Cha Agostino Gemelli

Baba Mtakatifu ameona nyuso za madaktari na wauguzi kiasi cha kuvutiwa na utendaji wao wa kazi unaosimikwa katika weledi, wakati walipokuwa wanamhudumia kama mgonjwa hospitalini hapo. Huduma ya matibabu anasema Baba Mtakatifu ni kielelezo cha moyo. Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli kinabeba ndani mwake jina la wito wa huduma ya binadamu! Asante!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 28 Novemba 2019 alizindua Mwaka wa Masomo wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli “Sacro Cuore” sanjari na uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 kwa mwaka 2020-2021 na kukazia umuhimu wa Chuo kikuu kujikita katika diplomasia kwa ajili ya ujenzi wa amani duniani. Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora, ujuzi na maarifa pamoja na kuhakikisha kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki, mara kwa mara kinapima mafanikio, matatizo na changamoto zinazojitokeza. Lengo ni kukiwezesha kuchangia katika mchakato wa maendeleo fungamani, ukuaji wa uchumi, majiundo makini pamoja na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu kinapaswa kujielekeza zaidi katika kutoa nadharia ambayo inamwilishwa katika vitendo.

Kwa kutambua changamoto zilizoko mbele yao na hivyo kutafuta nyenzo zitakazosaidia kupambana na matatizo pamoja na changamoto hizi ili hatimaye, suluhu ya kudumu iweze kupatikana kwa njia ya masomo yanayowapatia ujuzi, weledi na maarifa yanayotokana na tafiti makini za kisayansi. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli, Baba Mtakatifu Francisko, amemwandikia barua ya shukrani Professa Franco Anelli, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli, Roma kwa uwepo wao wa karibu wakati alipokuwa amelazwa hospitalini hapo. Ameona nyuso za madaktari na wauguzi kiasi cha kuvutiwa na utendaji wao wa kazi unaosimikwa katika weledi, wakati walipokuwa wanamhudumia kama mgonjwa hospitalini hapo. Huduma ya matibabu anasema Baba Mtakatifu ni kielelezo cha moyo. Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli kinabeba ndani mwake jina la wito wa huduma ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, amelazwa Hospitalini hapo, wakati huu Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya maisha na utume wake, kwa kujielekeza zaidi katika karne ijayo. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Chuo hiki kinajizatiti zaidi katika kunogesha elimu, utamaduni sanjari na huduma fungamani ya binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anasema, amegusa kwa maisha yake mwenyewe huduma yao, kumbe, hakuna sababu ya kulalama kwa yale yaliyopita. Kristo Yesu anayeteseka miongoni mwa wagonjwa wa kila rika, kuna hitaji jicho makini na lenye uwezo wa kutoa matumaini wakati wa shida na mahangaiko ya binadamui pamoja na kuangalia mbele zaidi. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kuona hayo yote wakati alipokuwa amelazwa Hospitalini hapo. Amekutana na kuonana na nyuso nyingi za watu wa Mungu Hospitalini hapo, amana na utajiri ambao ameuhifadhi moyoni mwake. Baba Mtakatifu anapenda kuwashukuru watu wa Mungu wote walioko kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli. Mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume!

Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” inaadhimishwa wakati ambapo dunia imepigishwa magoti kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni mwaliko wa kuadhimisha Jubilei hii katika hali ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, tayari kumpokea Kristo Yesu, ili aweze kuwa ni mwandani wa maisha, huku wakiendelea kuchota amana na utajiri wa huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waswahili husema, “Moyo usio na shukrani hukausha mema yote.” Baba Mtakatifu Francisko baada ya kulazwa tarehe 4 Julai 2021 na kufanyiwa operesheni kubwa kwenye utumbo mpana; aliendelea kupata matibabu hadi aliporuhusiwa tarehe 14 Julai 2021, akawashukuru wale wote waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao.

Siku hiyo hiyo alikwenda moja kwa moja kumshukuru Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Popoli Romani” kwa sala, maombezi na tunza yake ya kimama wakati wote alipokuwa amelazwa Hospitali ya Gemelli. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Julai 2021 amemwandikia Wakili Carlo Fratta Pasini, Rais wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS “Fondazione Policlinico Universitario Agostino Gemelli IRCCS” kumshukuru kwa niaba ya Familia kubwa ya watu wa Mungu Hospitali ya Gemelli, Roma, kwa ukarimu na udugu wao wa kibinadamu, ambao ameuonja wakati wote alipokuwa amelazwa hospitalini hapo, kiasi cha kumfanya ajisikie kuwa yuko nyumbani! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya afya, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Huduma hii imenogeshwa kwa weledi wa kisayansi. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ndani ya moyo wake, anabeba nyuso, historia na mahangaiko ya watu mbalimbali.

Hospitali ya Gemelli ni sawa na mji mdogo ndani ya Jiji kuu la Roma. Hapa ni mahali ambapo kila siku kuna maelfu ya watu wanaofika wakiwa na matumaini pamoja na wasiwasi mbalimbali kutokana na mahangaiko yao. Hospitalini hapo, licha ya kutoa huduma ya tiba, wagonjwa wanapata pia huduma ya kiroho na hivyo Hospitali inamhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; daima utu na heshima yake vikipewa msukumo wa pekee. Huduma hii anasema Baba Mtakatifu inakuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini wakati wa mateso na majaribu katika maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kazi nyeti na ngumu wanayoitekeleza Hospitalini hapo! Hii ni huduma ya huruma ambayo kwa njia ya wagonjwa, wahudumu hao wanaweza kukutana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua kwamba, ameona kwa macho yake mwenyewe na akatunza hicho alichokiona na atakiwakilisha mbele ya Mwenyezi Mungu kama ushuhuda wa matendo ya huruma mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru tena Wakili Carlo Fratta Pasini, Rais wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS, wafanyakazi na wale wote wanaounda familia kubwa ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Wote hawa amewapatia baraka zake za kitume na kuwaomba kuendelea kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Shukrani
21 July 2021, 15:48