Tafuta

Papa Francisko Jumapili tarehe 11 Julai 2021 ataongoza Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Hospitali ya Gemelli mjini Roma. Papa Francisko Jumapili tarehe 11 Julai 2021 ataongoza Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Hospitali ya Gemelli mjini Roma. 

Papa Francisko Kuongoza Sala ya Malaika wa Bwana 11 Julai 2021

Taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa tarehe 9 Julai 2021, inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameanza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kufanya kazi taratibu na kwamba, Jumapili tarehe 11 Julai 2021, Jumapili ya Utume wa Bahari, anatarajia kusali Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Ghorofa ya 10, Hospitali ya Gemelli, iliyoko mjini Roma. Hii ni Jumapili ya Utume wa Bahari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema ugonjwa na mateso yamekuwa daima kati ya matatizo mazito sana yanayoyaweka maisha ya mwanadamu katika majaribu. Katika ugonjwa mtu anapata mang’amuzi ya kutokuwa na uwezo, ya mipaka yake na kikomo chake. Kila ugonjwa unaweza kumfanya mwanadamu achungulie kifo. Ugonjwa unaweza kumpeleka mtu katika uchungu kwa kujihangaisha wenyewe, pengine hata kukata na kujikatia tamaa na hatimaye kumwasi Mwenyezi Mungu. Ugonjwa pia waweza kumkomaza mtu zaidi, kumsaidia kupambanua katika maisha yake kile ambacho si cha lazima, ili kuelekea kile kilicho lazima na muhimu. Mara nyingi sana ugonjwa huchochea kumtafuta Mwenyezi Mungu kwa toba na wongofu wa ndani. Rej. KKK 1499- 1500. Baba Mtakatifu Francisko tangu alipofanyiwa upasuaji mkubwa hapo tarehe 4 Julai 2021, hali yake inaendelea kuimarika kila kukicha. Changamoto za ugonjwa na hali ya uzee anaendelea kuzipokea katika hali ya utulivu na unyenyekevu mkuu. Madaktari wanaoendelea kumpatia matibabu wanaonesha matumaini makubwa kwa mgonjwa wao. Anaendelea kupata chakula kama kawaida pamoja na kufanya mazoezi ya viungo.

Taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa tarehe 9 Julai 2021, inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameanza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kufanya kazi taratibu na kwamba, Jumapili tarehe 11 Julai 2021, Jumapili ya Utume wa Bahari, anatarajia kusali Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Ghorofa ya 10, Hospitali ya Gemelli, iliyoko mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema kwamba, ameguswa sana na sala na ujumbe wa matashi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Anapenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru wale wote wanaoendelea kumsindikiza kwa sala, salam na matashi mema wakati huu ambapo amelazwa kwenye Hospitali ya Gemelli iliyoko mjini Roma. Baba Mtakatifu amekwisha kupokea salam na matashi mema kutoka kwa wakuu wa Nchi wa: Croatia Taiwan, Palestina, Uturuki, Kuwait, Cyprus, Poland, Ujerumani pamoja na Cuba. Kwa upande wake, Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba, katika salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kwa hakika watu wa Mungu wanahitaji hekima na busara pamoja na madaraka yake ya kimaadili.

Viongozi mbalimbali wanamwombea Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea katika shughuli zake za kuwafundisha watu wa Mungu, kuwatakasa na kuwaongoza, daima akiendelea kunogesha: imani, matumaini na mapendo kati ya watu wa Mataifa. Wanamwombea ili aweze kupona haraka ili kuendeleza mchakato wa haki, amani, umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Viongozi wakuu wa Makanisa pamoja na Mabaraza mbalimbali ya Maaskofu Katoliki yameendelea pia kutuma salam zao. Ni matumaini ya watu wa Mungu kwamba, baada ya kutoka Hospitali, Baba Mtakatifu atakuwa na ari na mwamko mpya katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa upande wake Baba Mtakatifu Franciko anayaelekeza mawazo yake kwa wagonjwa na hasa zaidi wale wanaoshindwa kupata huduma ya matibabu kutokana na sababu mbalimbali katika maisha yao. Wote hawa anawaombea pia ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwaangalia na hatimaye, waweze kupata msaada na huduma ya matibabu wanayohitaji zaidi. Baba anaendelea kuwashukuru watu wote wanaosali kwa ajili yake pamoja na wale wote wanaoendelea kumtumia ujumbe wa matashi mema!

Papa Gemelli

 

 

09 July 2021, 15:24