Tafuta

Papa Francisko anawakumbuka na kuwaombea wale waliokumbwa na mafuriko nchini China. Papa Francisko anawakumbuka na kuwaombea wale waliokumbwa na mafuriko nchini China. 

Mshikamano wa Papa Francisko kwa Waathirika wa Mafuriko China

Papa Francisko anapenda kuungana na watu wa Familia ya Mungu nchini China ambao wamekumbwa na maafa makubwa baada ya mvua kubwa kunyeesha na hivyo kusababisha mafuriko makubwa kwenye mkoa wa Henan na Manispaa ya jiji la Zhengzhou ndiyo iliyoathirika vibaya. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika siku za hivi karibuni mvua kubwa imenyeesha kwenye mkoa wa Henan na Manispaa ya jiji la Zhengzhou ndiyo iliyoathirika vibaya nchini China kutokana na mafuriko makubwa yaliyosababisha zaidi ya watu 58 kupoteza maisha na wengine wengi hawajulikani mahali walipo! Mvua kubwa imesababisha kingo za mito kuvunjika pamoja na maporomoko ya udongo ambayo pia yamesababisha makazi ya watu kubomoka. Mabwawa ya kuhifadhi maji, mengi yamebomoka na hivyo kutishia usalama wa maisha ya watu na mali zao. Tayari vikosi vya ulinzi na usalama vimepelekwa kwenye eneo la tukio, ili kusaidia juhudi za kuokoa maisha ya watu na mali zao. Mafuriko ni jambo la kawaida nchini China, lakini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kutokana na athari za uchafuzi mkubwa wa mazingira sanjari na mabadiliko ya tabianchi, mafuriko nchini China yamepelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao kwanza kabisa mijini na kwa sasa athari hizi zinaendelea kusambaa hata vijijini.

Ni katika muktadha huu wa maafa makubwa yaliyosababishwa na mafuriko makubwa huko nchini China, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alipenda kuungana na watu wa Familia ya Mungu nchini China ambao wamekumbwa na maafa makubwa baada ya mvua kubwa kunyeesha na hivyo kusababisha mafuriko makubwa kwenye mkoa wa Henan na Manispaa ya jiji la Zhengzhou. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya makubwa pamoja na familia zao. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake wa udugu wa kibinadamu na uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa wale wote walioathirika.

Mafuriko China

 

26 July 2021, 14:16