Tafuta

Papa Francisko anaungana na wale wote waliokumbwa na maafa ya mafuriko Barani Ulaya, anawaombea na kuwafariji wote walioguswa na kutikiswa na janga hili asilia. Papa Francisko anaungana na wale wote waliokumbwa na maafa ya mafuriko Barani Ulaya, anawaombea na kuwafariji wote walioguswa na kutikiswa na janga hili asilia. 

Mshikamano wa Papa Francisko Kwa Waathirika wa Mafuriko Barani Ulaya 2021

Baba Mtakatifu anawaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na maafa haya, ili waweze kupokelewa mbinguni. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aendelee kuwafariji, ndugu, jamaa na marafiki waliokumbwa na msiba huu mzito. Anawaombea baraka wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatafuta wale ambao hawajulikani waliko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kuanzia tarehe 12 Julai 2021, mvua kubwa imeendelea kunyeesha Barani Ulaya na hivyo kusababisha mafuriko makubwa na maporomoko ya udongo, hali ambayo imepelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wachunguzi wa mambo wanasema, haya ni madhara ya mabadiliko ya tabianchi kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani kutokana na uzalishaji wa hewa ya ukaa. Nchi ambazo zimeathirika kwa kiwango kikubwa ni pamoja na: Ujerumani, Ubelgiji, Luxembourg na Uholanzi. Nchi nyingine zilizopitiwa na mvua hizi ni pamoja na Uingereza, Italia na Austria ingawa kwa kiwango kidogo. Kuna baadhi ya vijiji na vitongoji vimefutwa kabisa kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo.

Hadi kufikia Jumatatu tarehe 19 Julai 2021 zaidi ya watu 192 walikuwa wamekwisha fariki dunia na maellfu wengine hawajulikani mahali waliko. Mvua kubwa iliyonyeesha imesababisha kingo za mito mingi kubomoka na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu pamoja na miundo mbinu. Majimbo ya Rhineland-Palatinate na North Rhine-Westphalia (NRW) ndiyo yaliyoathirika zaidi nchini Ujerumani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 18 Julai 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka zake. Amewakumbuka na kuwaombea watu wote waliokumbwa na maafa kutokana na mvua kubwa zilizonyeesha kwa siku za hivi karibuni.

Baba Mtakatifu anawaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na maafa haya, ili waweze kupokelewa mbinguni na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aendelee kuwafariji, ndugu, jamaa na marafiki waliokumbwa na msiba huu mzito. Anawaombea baraka wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatafuta wale ambao wanahofiwa kufunikwa kwa kifusi pamoja na kusombwa na maji. Nchi nyingi Barani Ulaya zimetangaza hali ya hatari kutokana na hofu ya mafuriko hayo kuendelea kusababisha maafa. Katika hali na mazingira haya, mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu unahitajika sana kama kikolezo cha faraja kwa wale walioathirika na maafa haya katika ujumla wao.

Papa Mafuriko Ulaya
19 July 2021, 14:41