Tafuta

Mvua kubwa imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Zaidi ya watu 150 wamefariki dunia na wengine 1, 300 hawajulikani mahali walipo! Mvua kubwa imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Zaidi ya watu 150 wamefariki dunia na wengine 1, 300 hawajulikani mahali walipo! 

Mafuriko Ulaya: 150 Wamefariki dunia, 1300 Hawajulikani Walipo!

Mvua kubwa iliyonyeesha Alhamisi, tarehe 15 Julai 2021 imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao nchini: Ujerumani, Ubelgiji, Luxembourg na Uholanzi. Hadi kufikia Ijumaa, tarehe 16 Julai 2021 zaidi ya watu 150 walikuwa wamekwisha fariki dunia na wengine zaidi ya 1, 300 hawajulikani mahali waliko. Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambirambia na faraja kwa wote

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mvua kubwa iliyonyeesha na hivyo kusababisha mafuriko makubwa Alhamisi, tarehe 15 Julai 2021 imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao nchini: Ujerumani, Ubelgiji, Luxembourg na Uholanzi. Hadi kufikia Ijumaa, tarehe 16 Julai 2021 zaidi ya watu 150 walikuwa wamekwisha fariki dunia na wengine zaidi ya 1, 300 hawajulikani mahali waliko. Mvua kubwa iliyonyeesha imesababisha kingo za mito mingi kubomoka na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu pamoja na miundo mbinu. Utabiri wa hali ya hewa unaonesha kwamba, bado mvua kubwa inatarajiwa kunyeesha hadi kufikia mwishoni mwa juma. Majimbo ya Rhineland-Palatinate na North Rhine-Westphalia (NRW) ndiyo yaliyoathirika zaidi nchini Ujerumani.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani ameonesha masikitiko yake makubwa kwa wote waliopoteza maisha na kuathirika na mafuriko haya. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambirambi anawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili awakirimie moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya. Anawaombea wote ambao bado hawajulikani waliko baada ya kukumbwa na mafuriko pamoja na kuangukiwa na vifusi vya nyumba walimokuwa wanaishi. Neno la matumaini na faraja liwaendelee watu wote walioguswa na maafa haya asilia.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na kwamba, anapenda kuwatia shime wafanyakazi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwaokoa watu waliokumbwa na mafuriko Ujerumani, Ubelgiji, Luxembourg na Uholanzi. Viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Kimataifa wameonesha kusitikishwa kwao na maafa yaliyojitokeza katika nchi hizi. Kuna hofu kubwa kwamba idadi ya watu waliopoteza maisha yao, huenda ingaongezeka maradufu. Serikali ya Ujerumani inaendelea kuwatafuta kwa udi na uvumba wale ambao bado hawajaonekana. Watu wengi wamelazimika kuhama makazi yao ili kutafuta hifadhi mahali pa salama zaidi. Wachunguzi wa mambo wanasema, hizi ni athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kuongezeka kwa joto duniani. Itakumbukwa kwamba, mvua kubwa pamoja na mafuriko yaliyotokea kwenye nchi kadhaa Barani Ulaya katika kipindi cha mwaka 2002 yalipelekea watu zaidi ya 121 kupoteza maisha.

Mafuriko Ulaya

 

17 July 2021, 08:51