Tafuta

Jubilei ya Miaka 50 ya "Caritas Italiana" mashuhuda na wahudumu wa Injili ya upendo Jubilei ya Miaka 50 ya "Caritas Italiana" mashuhuda na wahudumu wa Injili ya upendo 

Miaka 50 ya Caritas Italiana: Injili ya Huduma ya Upendo Kwa Maskini

Upendo ni huruma ya Mungu inayowatafuta na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi. Mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo, wawe na ujasiri wa kujifunza kutoka katika shule ya maskini, kwani hawa ni kielelezo cha Madonda Matakatifu ya Yesu! Kuwahudumia kwa ari na moyo mkuu ni sawa na kukutana na Kristo Yesu kati pamoja na waja wake! Maskini ni amana ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Hawa ni walengwa wa kwanza wa mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Umoja, upendo na mshikamano wa utu na udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Katika muktadha huu mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani sanjari na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa upendo na katika maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayowatenga na kuwanyanyasa maskini.  Kwa sasa tofauti kati ya watu inakuwa ni chanzo cha kinzani, uhasama na vita. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma; wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa binadamu, kati ya watu wa mataifa, familia na tamaduni zao.

Mtakatifu Paulo VI aliwahi kusema, Injili ya upendo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu ambao kwa wakati wake, utashinda chuki, kinzani na vita. Huu ni ushuhuda wa mshikamano unaotekelezwa na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas katika ngazi mbalimbali. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Italia, “Caritas Italiana”, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. “Caritas Italiana” inaundwa na Mashirika ya Misaada kutoka katika Majimbo 220 ya Kanisa Katoliki nchini Italia. Haya ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaolitaka Kanisa kuwa ni Sakramenti ya wokovu na chombo cha mshikamano wa upendo na maskini. Iliundwa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1971. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe wa “Caritas Italiana” tarehe 26 Juni 2021 alikazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa “Caritas Italiana” kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu pasi na kutafuta makuu.

Upendo ni huruma ya Mungu inayowatafuta na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi. Mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo, wawe na ujasiri wa kujifunza kutoka katika shule ya maskini, kwani hawa ni kielelezo makini cha Madonda Matakatifu ya Yesu! Kuwahudumia kwa ari na moyo mkuu ni sawa na kukutana na Kristo Yesu kati pamoja na waja wake! Uwepo wa maskini, iwe ni chachu ya toba na wongofu wa ndani, tayari kutubu na kumwongokea Mungu ili kuachana na yale mambo yanayopelekea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mtindo na tunu msingi za Kiinjili ziwe ni dira na mwongozo wa huduma ya upendo kwa maskini, kama Mtakatifu Paulo Mtume, anavyofafanua maana ya upendo katika Utenzi wake katika Waraka wa Kwanza kwa Wakorintho 13:7. Huu ni upendo unaowaambata na kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi.

Ni upendo unaomshughulikia mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa sababu binadamu ndiye njia ya Kanisa kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II. Injili ya huduma ya upendo inapaswa kutolewa kwa kujikita katika kipaji cha ubunifu, uzoefu na weledi, daima kwa kusoma alama za nyakati, ili kutambua mifumo mipya ya umaskini na utumwa mamboleo inayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawaalika vijana kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini; huduma ambayo inapaswa kutolewa kwa furaha, ili kujenga na kudumisha utu, heshima na udugu wa kibinadamu. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika Ibada ya Liturujia ya Neno, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa “Caritas Italiana” aliwakumbusha wajumbe wa “Caritas Italiana” kwamba, huduma kwa maskini ni mchakato unaowawezesha kushiriki katika upendo wa Mungu unaookoa, unaoganga na kuponya!

Hii ni namna ya kufikiri na kutenda, kadiri ya mwanga na karama za Roho Mtakatifu anazolikirimia Kanisa lake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Karama za Roho Mtakatifu ziwasaidie waamini kujenga na kudumisha fadhila ya unyenyekevu katika huduma ya upendo. Watambue kwamba, wanahudumia kwa sababu wanapenda kuhudumia! Huu ni mwaliko kwa waamini wote kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo kwa jirani zao kama sehemu ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, “Caritas Internationalis”, anawataka waamini kuonesha uvumilivu, upole na upendo kwa maskini. Anawashukuru na kuwapongeza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waliojitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao pamoja na yale ya wapendwa wao! Hawa ni mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo ambao wametekeleza dhamana na utume wao kwa ujasiri, mshikamano na upendo wa dhati.

Injili ya Upendo

 

 

 

20 July 2021, 15:23