Tafuta

Tarehe Mosi Julai 2021 Gazeti la L'Osservatore Romano linaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 160 tangu kuanzishwa kwake. Tarehe Mosi Julai 2021 Gazeti la L'Osservatore Romano linaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 160 tangu kuanzishwa kwake. 

Gazeti la L'Osservatore Romano Kumbukizi ya Miaka 160 Utume!

Gazeti la L’Osservatore Romano, tarehe 1 Julai 2021 linaadhimisha rasmi kumbukumbu ya Miaka 160 tangu kuanzishwa kwake. Hili ni gazeti linalomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, kama chombo cha mawasiliano ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu aliwatakia heri na baraka wafanyakazi wote na waendelee kujikita katika fadhila ya uaminifu na ubunifu kwa mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, Jumanne tarehe 29 Juni 2021 alisema kwamba, Gazeti la L’Osservatore Romano, tarehe 1 Julai 2021 linaadhimisha rasmi kumbukumbu ya Miaka 160 tangu kuanzishwa kwake. Hili ni gazeti linalomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, kama chombo cha mawasiliano ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu aliwatakia heri na baraka wafanyakazi wote wa L’Osservatore Romano na kuwataka kuendelea kujikita katika fadhila ya uaminifu na ubunifu, ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na huduma inayotolewa na gazeti hili. Baba Mtakatifu mwenyewe anakiri kwamba, anapenda kulisoma kwa sababu ni gazeti ambalo limesheheni habari za maisha na utume wa Kanisa katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya “Inter Mirifica” yaani “Njia za Mawasiliano ya Jamii” wanakazia umuhimu wa mawasiliano ya jamii unaoweza kumsaidia au kumwangamiza mwanadamu, pale ambapo kanuni maadili, utu wema, ustawi na maendeleo ya wengi havitazingatiwa.

Vyombo vya mawasiliano ya jamii havina budi kusaidia kutangaza na kushuhudia ukweli; kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kati ya watu. Visaidie kukuza na kuendeleza uhuru unaowawajibisha watu kimaadili sanjari na kusaidia mchakato wa watu kupyaisha maisha yao ya kiroho na kiutu! Kimsingi njia za mawasiliano ya jamii hazina budi kuhakikisha kwamba, zinasaidia kutoa huduma makini ya mawasiliano katika medani mbalimbali za mawasiliano ya kijamii ili kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linatumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya habari kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Njia za mawasiliano zisaidie katika shughuli mbalimbali za kichungaji zinazofanywa na kutekelezwa na Mama Kanisa. Mawasiliano ya Jamii ni sekta ambayo inakua na kupanuka kwa haraka sana, kiasi cha kubeba changamoto, matatizo na fursa ambazo, zinaweza kuvaliwa njuga na Mama Kanisa katika maisha na utume wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Miaka 160 tangu kuanzishwa kwa Gazeti la L’Osservatore Romano na Miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Radio Vatican, Jumatatu tarehe 24 Mei 2021 alitembelea Jumba la Mawasiliano ya Vatican. Akafanya mahojiano maalum na Radio Vatican na hatimaye, akazungumza na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Baba Mtakatifu alitumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kazi kubwa wanayofanya katika maisha na utume wa Kanisa. Hata hivyo, Baba Mtakatifu alionesha wasiwasi kuhusu idadi ya watu wanaosoma Gazeti la L’Osservatore Romano, wale wanaosikiliza Radio Vatican pamoja na kusoma habari mbalimbali zinazoandikwa na kutundikwa kwenye mitandao ya kijamii inayoendeshwa na Vatican, yaani: Vatican News. Lengo kubwa la Kanisa kuwekeza katika tasnia ya mawasiliano ya jamii ni kuhakikisha kwamba, ujumbe unawafikia watu wa Mungu popote pale walipo.

Ni rahisi sana kuwa na taasisi nzuri na yenye vifaa bora lakini kama ujumbe wake hauwafikii walengwa, hii ni hatari sana. Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano kujiuliza kila siku, Je, ni watu wangapi wanasikiliza na kusoma ujumbe wao. Habari Njema ya Wokovu inapaswa kuwafikia watu wote wa Mungu mahali walipo! Je, ni watu wangapi wanapata Habari Njema ya Injili kutoka kwenye Gazeti la L’osservatore Romano na Radio Vatican? Baba Mtakatifu anakaza kusema hili ni swali msingi sana. Kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, matunda yake yameanza kuonekana. Vatican News imekuwa ni msaada mkubwa kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Licha ya mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, radio bado inaendelea kuchukua kipaumbele cha kwanza. Kuna watu wengi wanasikiliza kwa hakika.

Ukiritimba na urasimu ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya taasisi yoyote ile. Watu wajenge utamaduni wa kufanya kazi kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ubunifu, daima wakipania kuboresha zaidi shughuli zao. Ikiwa kama juhudi zote hizi zinafanywa, lakini walengwa hawapati Habari Njema ya Wokovu, anasema Baba Mtakatifu hapo kuna kasoro kubwa! Watu wawe huru kutekeleza vyema shughuli zao, kiasi hata cha kuthubutu kukosea, hali inayohitaji: moyo mkuu na ujasiri wa kutosha!

Romano 160 Yrs
01 July 2021, 15:43