Tafuta

Papa Francisko ameidhinisha matumizi ya Qurbana Takatifu katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu kwa Makanisa ya Mashariki. Papa Francisko ameidhinisha matumizi ya Qurbana Takatifu katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu kwa Makanisa ya Mashariki. 

Waraka wa Papa Francisko Kuhusu Qurbana Takatifu: Ekaristi Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko, amewaandikia Waraka watu wa Mungu wa Kanisa la Syro-Malabar kuhusu maadhimisho ya Qurbana Takatifu, “The Holy Qurbana” akiwa ameridhia kwamba, yaanze kutumika baada ya maamuzi haya kupitishwa kwenye Sinodi ya Maaskofu wa Syro-Malabar iliyoadhimishwa kunako mwaka 1999 kama kielelezo makini cha ujenzi wa umoja wa Kikanisa! Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Qurbana Takatifu, “The Holy Qurbana (ܩܘܼܪܒܵܢܵܐ ܩܲܕܝܫܵܐ‎, Qurbānā Qaddišā ni mtindo wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanayotumiwa na Wakristo huko Siria ya Mashariki. Ni maadhimisho ambayo ni mkusanyiko wa zamani wa madhehebu ya Wakristo kutoka Asiria, Babilonia pamoja na Chaldea. Yote haya yanapata chimbuko lake kutoka katika mafundisho ya Mtakatifu Thomas Mtume. Makanisa ya Syro-Malabar, Wakatoliki wa Chaldea pamoja na Makanisa ya Mashariki yana umoja kamili na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni katika mukadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, amewaandikia Waraka watu wa Mungu wa Kanisa la Syro-Malabar kuhusu maadhimisho ya Qurbana Takatifu, “The Holy Qurbana” akiwa ameridhia kwamba, yaanze kutumika baada ya maamuzi haya kupitishwa kwenye Sinodi ya Maaskofu wa Syro-Malabar iliyoadhimishwa kunako mwaka 1999 kama kielelezo makini cha ujenzi wa umoja wa Kikanisa. Yote haya ni matunda ya maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo na juhudi za kichungaji zilizotekelezwa na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema katika Waraka huu kwamba, matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa zinahitaji mang’amuzi. Kumbe, kupitishwa kwa Madhehebu ya Qurbana Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanalenga kusaidia mchakato wa uinjilishaji hasa kwa waamini wanaoishi nje ya nchi na Makanisa yao ya asili. Kwa njia hii, waamini mbalimbali wataweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa amani na utulivu wa ndani na kama matunda ya kazi za Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, wakati ni mkubwa kuliko mahali, mwaliko ni kukubali mvutano kati ya utimilifu na mapungufu na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wakati.

Maaskofu wanapaswa kutembea hatua kwa hatua na kushirikiana bega kwa bega na watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, umoja na mshikamano hushinda vurugu. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kutambua “Raza Qurbana Taksa” na anawahimiza wakleri, watawa na waamini walei kuwa tayari kuunganisha maadhimisho ya Qurbana Takatifu kwa ajili ya: udugu, mafao, ustawi na umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu anamwomba Roho Mtakatifu ili apende kuimarisha umoja kati ya Makanisa yote ya Mashariki kama sehemu ya utekelezaji wa Maazimio ya Sinodi.

Qurbana Takatifu

 

06 July 2021, 14:59