Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Ni walengwa wakuu katika mchakato wa uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Ni walengwa wakuu katika mchakato wa uinjilishaji. 

Papa Francisko Maskini ni Amana, Utajiri na Walengwa wa Uinjilishaji

Papa Francisko ametuma ujumbe wa video kwa wafanyakazi wa kujitolea wa “Huduma ya Upendo wa Usiku pamoja na Nyumba ya Nazareti, “Noche de Caridad e dell’Hogar de Nazareth” Jimbo Katoliki la Mar del Plata nchini Argentina. Hili ni kundi maalum linaloendelea kujisadaka kwa ajili ya maskini, watu wasiokuwa na makazi na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu. Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati ya watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 24 Juni 2021 ametuma ujumbe wa video kwa wafanyakazi wa kujitolea wa “Huduma ya Upendo wa Usiku pamoja na Nyumba ya Nazareti, “Noche de Caridad e dell’Hogar de Nazareth” Jimbo Katoliki la Mar del Plata nchini Argentina. Hili ni kundi maalum linaloendelea kujisadaka kwa ajili ya maskini, watu wasiokuwa na makazi maalum na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa huduma makini kwa maskini. Kuanzia tarehe 21 Juni hadi tarehe 21 Septemba 2021, Jimbo Katoliki la Mar del Plata nchini Argentina limekodi hoteli kwa ajili ya kutoa huduma kwa watu 75, ili kuwakinga na kipindi cha baridi kali.

Huu ni ushuhuda uliotolewa na Askofu Gabriel Antonio Mestre wa Jimbo Katoliki la Mar del Plata nchini Argentina. Ni kwa njia ya huduma ya usiku wa upendo, Kanisa limeweza kuokoa maisha ya maskini, ambao mara nyingi wanaathirika na hatimaye kufariki dunia kwa sababu ya baridi kali. Huduma ya usiku wa upendo inatoa fedha, mavazi, dawa na mahitaji msingi kwa maskini. Maskini hawa ni matokeo ya athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; ni watu wenye mgogoro wa afya ya akili au baadhi yao wameathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia. Baadhi yao ni wazee na wagonjwa wa muda mrefu, wote hawa wanapewa huduma makini inayopania usalama wa maisha yao! Baba Mtakatifu kwa moyo wa upendo na shukrani, anawapongeza waamini walei, wakleri na wafadhili wa Kanisa kwa kumsaidia Kristo Yesu, anayejifunua kwa njia ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na hawa ndiyo wale wanaopatikana huko pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Argentina
01 July 2021, 15:06