Tafuta

Afya ya Papa Francisko inaendelea kuimarika baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa kwenye utumbo mpana Jumapili tarehe 4 Julai 2021. Afya ya Papa Francisko inaendelea kuimarika baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa kwenye utumbo mpana Jumapili tarehe 4 Julai 2021. 

Afya ya Papa Francisko Inaendelea Kuimarika Baada ya Operesheni

Taarifa ya madaktari kutoka Hospitalini Gemelli inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu amefanikiwa kupata usingizi mwanana wakati wa usiku na Jumanne, asubuhi tarehe 6 Julai 2021 baada ya masifu ya asubuhi, alipata kifungua kinywa na baadaye alipata nafasi ya kupitia baadhi ya magazeti waliyomletea chumbani mwake hapo Hospitalini kwenye Ghorofa ya 10. Ameanza mazoezi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tangu alipolazwa kwenye Hospitali ya Gemelli iliyoko mjini Roma na hatimaye kufanyiwa upasuaji mkubwa kwenye utumbo mpana, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 anaendelea vyema. Taarifa ya madaktari kutoka Hospitalini Gemelli inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu amefanikiwa kupata usingizi mwanana wakati wa usiku na Jumanne, asubuhi tarehe 6 Julai 2021 baada ya masifu ya asubuhi, alipata kifungua kinywa na baadaye alipata nafasi ya kupitia baadhi ya magazeti waliyomletea chumbani mwake hapo Hospitalini kwenye Ghorofa ya 10. Ameanza kufanya mazoezi ya kutembea kidogo kidogo hospitalini hapo. Madaktari wanaendelea kufuatilia mwenendo wa afya yake na kwamba, hadi sasa inaendelea vyema. Huu ni ufafanuzi uliotolewa tarehe 6 Julai 2021 na Dr. Matteo Bruni, Msemaji mkuuu wa Vatican. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kupata salam na matashi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kati ya salam hizi ni kutoka kwa: Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM pamoja Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri.

Waamini na watu wenye mapenzi mema wanaendelea kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea kwenye maisha na utume wake, tayari kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kupitia kwa Askofu mkuu Georg Ganswein, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, anaendelea kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kupona haraka. Kwa sasa Baba Mtakatifu anasaidiwa na wauguzi wawili kutoka Vatican na kwamba, atalazimika kukaa hospitalini walau kwa muda wa siku saba kama hakutakuwa na mabadiliko makubwa mintarafu mwenendo wa afya yake. Kwa upande wake, Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anapenda kumhakikishia Baba Mtakatifu Francisko uwepo wake wa kiroho kwa njia ya sala, ili aweze kupona haraka na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, changamoto na wito kutoka kwa Kristo Yesu.

Anasema, “Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu; na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya mwanadamu” 1 Kor 1:25. Fumbo la Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu linajionesha na kuendelezwa hata katika maisha, udhaifu na mateso ya mwanadamu, ili kwamba, Injili ya Kristo Yesu, iweze kumwilishwa kikamilifu katika maisha ya waja wake! Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali nchini Italia, wanamtakia heri, baraka na uponywaji wa haraka. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe tarehe 11 Julai, Siku ya Utume wa Bahari, ataweza kusali na kuwasalimia waamini kutoka Hospitalini Gemelli. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM kwa upande wake, linamshukuru Mungu kwa kufanikisha upasuaji mkubwa aliofanyiwa Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Julai 2021.

Maaskofu pamoja na watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini wanapenda kumwonesha uwepo wao wa karibu kwa njia ya sala, wakati huu anapoendelea kupata matibabu. Dhamana na wajibu wa Shirikisho la Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini ni kunogesha umoja na mshikamano wa kidugu, ili aweze kuinuka tena na kuendeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani.

Papa Francisko Afya

 

06 July 2021, 15:12