Papa Francisko Aruhusiwa Kutoka Hospitalini, Amshukuru B. Maria!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko aliyelazwa Hospitali ya Gemelli tangu Jumapili jioni tarehe 4 Julai 2021 na kufanyiwa operesheni kubwa, hali yake imeendelea kuimarika zaidi na zaidi. Madaktari wanaomshughulia, tarehe 14 Julai 2021 wamemruhusu Baba Mtakatifu Francisko kutoka Hospitali ya Gemelli na hivyo kurejea tena kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican. Mara baada ya kutoka Hospitalini, Baba Mtakatifu amekwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, kusali na kumshukuru Bikira Maria, Afya ya Warumi, “Salus Popoli Romani” kwa sala, maombezi na tunza yake ya kimama wakati wote alipokuwa amelazwa Hospitali ya Gemelli.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kusali na kuwaombea wagonjwa wote waliolazwa hospitalini sehemu mbalimbali za dunia. Lakini kwa namna ya pekee, wale ambao amekutana nao wakati alipokuwa amelazwa Hospitali ya Gemelli na majira ya mchana kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa tayari kwenye maskani yake mjini Vatican. Baba Mtakatifu, Jumanne tarehe 13 Julai 2021 aliwatembelea watoto wagonjwa wa Saratani waliolazwa kwenye Hospitali ya Gemelli mjini Roma, ili kufarijiana pamoja nao! Amewashukuru kwa sala na sadaka yao wakati wote alipokuwa amelazwa pamoja nao Hospitalini hapo. Amewaomba waendelee kumkumbuka na kumwombea katika sala na sadaka zao. Amewaahidia sala zake kwao pia.