Tafuta

Papa Francisko asema mashemasi wa kudumu wanayo nafasi muhimu sana katika huduma kwa watu wa Mungu. Papa Francisko asema mashemasi wa kudumu wanayo nafasi muhimu sana katika huduma kwa watu wa Mungu. 

Wito na Wajibu wa Mashemasi wa Kudumu Ndani ya Kanisa Katoliki

Huduma ya Daraja Takatifu ya Ushemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuliwezesha Kanisa kupenda na hivyo kuweza kuhudumia na kuwaongoza watu wa Mungu. Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma makini kwa watu wa Mungu. Kumbe, Mashemasi wa Kudumu wapo kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, utume unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. HUDUMA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Daraja Takatifu ya Upadre imegawanyika katika madaraja makuu matatu: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Daraja yenyewe, Upadre na Ushemasi ambao pia umegawanyika katika makundi makuu mawili, yaani: Ushemasi wa Mpito kwa wale wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu ya Upadre pamoja na Ushemasi wa Kudumu. Kimsingi, Mashemasi wamewekewa mikono siyo kwa ajili ya ukuhani, bali ni kwa ajili ya huduma ya utumishi. Kwa maana, wakiwa wamethibitika kwa neema ya Sakramenti wanalitumikia taifa la Mungu katika ushirika na Askofu na umoja wa Mapadre wake, katika huduma, “diakonia” ya: Liturujia ya Kanisa, Neno la Mungu na Upendo kwa Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mashemasi wanaweza kutoa Ubatizo rasmi, kuitunza na kuigawa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kusimamia na kuibariki Ndoa Takatifu kwa niaba ya Kanisa. Kuwapelekea Komunyopamba walio katika hatari ya kufa; kuwasomea waamini Maandiko Matakatifu; kuwafundisha na kuwaonya watu. Huduma nyingine ni kuongoza Ibada na Sala za waamini; kugawa visakramenti, kuongoza Ibada ya maziko na mazishi. Kimsingi Mashemasi wanapaswa kuwa na huruma, wenye bidii, wakienenda katika ukweli wa Bwana, aliyejifanya mtumishi wa wote. Kuna baadhi ya nchi duniani ambazo zina Mashemasi wa Kudumu. Hawa ni wanaume wenye umri wa kukomaa na wanaoishi katika Ndoa Takatifu. Rej. LG 29.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Jimbo kuu la Roma, Kardinali Angelo De Donatis, Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Roma, amemteuwa Shemasi wa Kudumu Giustino Trincia kuwa Mkurugenzi wa Caritas Roma na Don Paolo Salvin, atakuwa ni Mkurugenzi Msaidizi. Uongozi huu mpya utaanza kushika madaraka mwezi Septemba 2021. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 19 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na Mashemasi wa Kudumu Jimbo kuu la Roma, waliokuwa wameambatana na familia zao. Jimbo kuu la Roma, kwa kufuata Mapokeo ya tangu Kale, limetoa pia Parokia moja inayohudumiwa na Shemasi wa Kudumu. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kujikita zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu, kwa ari na moyo mkuu, kwa unyenyekevu na sadaka! Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amefafanua maana ya Huduma ya Daraja Takatifu ya Ushemasi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuliwezesha Kanisa kupenda na hivyo kuweza kuhudumia na kuwaongoza watu wa Mungu.

Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma makini kwa watu wa Mungu. Kuna baadhi ya nchi ambazo zina uhaba mkubwa wa Mapadre kutokana na kupungua kwa idadi ya miito ya Daraja Takatifu, kumbe, Mashemasi wa Kudumu wapo kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, utume unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. Mashemasi wa Kudumu wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya Ndoa na Familia. Mashemasi wa Kudumu wawasaidie waamini kumtambua Kristo Yesu na Kanisa lake katika huduma kwa maskini wa hali na kipato! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwapongeza Mashemasi wa Kudumu pamoja na familia zao. Baba Mtakatifu anasema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wameelezea kwa kina Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa kusema kwamba, kimsingi, Mashemasi wamewekewa mikono siyo kwa ajili ya ukuhani, bali ni kwa ajili ya huduma ya utumishi. Katika maisha na utume wa Kanisa fadhila ya unyenyekevu katika huduma inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kufuata mfano bora wa Kristo Yesu aliyejinyenyekesha na kuwa mdogo kuliko wote kwa ajili ya kutoa huduma.

Ushemasi yaani huduma ni dhana inayobaki katika maisha ya Wakleri. Mitume na wafuasi wa Kristo Yesu wanapaswa kutambua kwamba, kupenda ni kuhudumia na kuhudumia ni kuongoza na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma makini kwa watu wa Mungu. Dhana ya Ushemasi katika maisha na utume wa Kanisa inakita mizizi yake katika Umisionari, kwani kimsingi Kanisa ni la kimisionari linalopaswa kuishi na kudumu katika huduma. Bila huduma makini kwa watu wa Mungu, Kanisa litakengeuka na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Kanisa halina budi kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya upendo kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyemtumikia Mwenyezi Mungu pamoja na jirani kwa furaha, amani na utulivu wa ndani. Huo ndio msukumo wa unyenyekevu wa Mungu, kuwaendea hata wale ambao watu wamewageuzia kisogo na “kuwaangalia kama nyanya mbichi”. Kupungua kwa idadi ya miito ya Daraja Takatifu ya Upadre, huduma mbalimbali zinazotolewa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake, zinaweza kutekelezwa vyema kabisa na Mashemasi wa Kudumu.

Kwa maana, wakiwa wamethibitika kwa neema ya Sakramenti wanalitumikia taifa la Mungu katika ushirika na Askofu na umoja wa Mapadre wake, katika huduma, “diakonia” ya: Liturujia ya Kanisa, Neno la Mungu na Upendo kwa Maskini, Wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Roma ilibahatika kupata Mashemasi hodari katika huduma na leo hii wamekuwa ni mifano bora ya kuigwa na watu wote wa Mungu katika huduma kwa jirani kama Mama Kanisa anavyokazia katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Mashemasi wa Kudumu Jimbo kuu la Roma wanaendelea kutoa ushuhuda wenye mvuto katika huduma kwa watu wa Mungu na maskini katika ujumla wake. Kimsingi tasaufi ya Ushemasi inakita mizizi yake katika huduma ya unyenyekevu; ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya maskini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mashemasi wa Kudumu watajenga na kukuza ndani mwao fadhila ya unyenyekvu na yote yale watakayotenda, iwe ni siri sirini kati yao na Mwenyezi Mungu na wala wasijitafutie umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Mashemasi wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, ili kuleta faraja na matumaini kwa wale wote wanaochechemea katika shida na magumu ya maisha. Mashemasi wa Kudumu wajenge mahusiano na mafungamano ya kijamii na wadau mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Hapa, jambo la msingi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mashemasi wa Kudumu wawe ni walinzi waaminifu si tu kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; bali wasaidie Jumuiya za Kikristo kumwezesha Kristo Yesu kutembelea maskini na wale wote ambao wako mbali zaidi na maisha pamoja na utume wa Kanisa, ili kwa kuwaona Mashemasi wa Kudumu, waamini wenye shida na mahangaiko yao: kiroho na kimwili waweze kumtambua Kristo Yesu kati yao katika huduma.

Mashemasi wa Kudumu
19 June 2021, 16:18