Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni 2021. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni 2021. 

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya Mazingira Duniani 5 Juni 2021

Baba Mtakatifu anaunga mkono jitihada za UNEP na FAO kuhusu Mpango mkakati wa miaka kumi wa maboresho ya mazingira kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2030, kwa kusimama kidete: kuzuia, kudhibiti na kurekebisha ikolojia, ili kuweza kupata ufanisi zaidi. Binadamu ni sehemu ya Kazi ya Uumbaji, atende na kuwajibika kama mtunzaji na wala si mkwapuaji wa utajiri wa dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Tangu mwaka wa 1974, Siku ya Mazingira Duniani inaadhimishwa tarehe 5 Juni. Hili ni jukwaa la kimataifa la kuhamasisha na kuchukua hatua kuhusu masuala nyeti ya mazingira kuanzia kwa uchafuzi baharini, ongezeko la joto duniani hadi kwa matumizi ya bidhaa kwa njia endelevu na uhalifu dhidi ya wanyamapori.  Mamilioni ya watu wameshiriki katika miaka iliyopita, na kuleta mabadiliko jinsi ya kutumia bidhaa na kwenye sera za mazingira za Kitaifa na Kimataifa. Makundi ya kidini yana jukumu la kutekeleza ili kukomesha uharibifu wa bayoanuai na kutunza mazingira kwa manufaa ya familia ya binadamu. Viongozi wa kidini wa ngazi zote wanaweza kushawishi waamini wa dini zao, kuishi vizuri duniani na kutafuta ajira zisizochafua mazingira. Mwanzo, watu wanapaswa kujifunza kuhusu kile wanachoweza kufanya; kushiriki maarifa hayo na wanajamii wakati wa Siku ya Mazingira Duniani, na ikiwezekana kuchukua hatua za kubadili kile wanachostahili kubadili. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, “United Nations Environment Programme, UNEP” ndilo linaongoza duniani kwa kuweka ajenda za kimataifa za mazingira, linawezesha utekelezaji wa maendeleo endelevu kwenye nyanja ya mazingira kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa, na hufanya kazi kama mtetezi mkuu wa mazingira duniani.

Dhima ni kuongoza na kuwezesha ushirikiano katika utunzaji bora wa mazingira kwa kuhimiza, kuelimisha na kuwezesha Mataifa na watu kuimarisha hali yao ya maisha bila kuathiri yale ya vizazi vijavyo. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, tarehe 5 Juni 2021 Siku ya Mazingira Duniani linazundua Maadhimisho ya Miongo ya Hatua za Kutunza Mazingira. Hili kimsingi ni vuguvugu la Kimataifa la uboreshaji wa mifumo ya ekolojia kwa kutambua kwamba, hiki ni kizazi kichoweza kutengeza amani na mazingira nyumba ya wote! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa video aliowandikia Mrs Inger Anderson, Mkurugenzaji Mtendaji wa UNEP na Dr. Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na kusomwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa Mwaka 2021 anahimisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika kukabiliana na changamoto za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kujali na kutunza mazingira kunahitaji uhusiano na mshikamano wa upendo wa kidugu sanjari na kuwa na jitahada za kutafuta suluhisho la matatizo yanayoisonga jamii.

Baba Mtakatifu anaunga mkono jitihada za Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP na FAO kuhusu Mpango mkakati wa miaka kumi wa maboresho ya mazingira kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2030, kwa kusimama kidete: kuzuia, kudhibiti na kurekebisha ekolojia, ili kuweza kupata ufanisi zaidi. Baba Mtakatifu anasema, binadamu ni sehemu ya Kazi ya Uumbaji, changamoto ni kutenda na kuwajibika kama watunzaji bora wa mazingira na wala si kama wakwapuaji wa rasilimali za dunia, jambo linalohatarisha msingi unaotegemeza maisha ya mwanadamu. Matokeo yake ni athari za mabadiliko ya tabianchi zinazojionesha kwa mafuriko, baa la njaa linalowapekenya watu wengi duniani; mambo yanayohatarisha ustawi na maendeleo kwa sasa na kwa siku zijazo kama wanavyobainisha wanasayansi. Familia ya watu wa Mungu inapaswa kusaidiana na kuwajibikiana, kwa kuheshimu na kufuata dhamiri nyofu inayowadai utunzaji bora wa mazingira na wala si uharibifu na ulaji wa kupindukia. Jumuiya ya Kimataifa inao wajibu wa kutunza mazingira ili kuhakikisha kwamba inakiachia kizazi kijacho mazingira mazuri zaidi ya kuishi.

Kwa bahati mbaya sana, hali kwa sasa ni tete sana kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote sanjari na janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambapo limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumekuwepo na athari kubwa za myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa; majanga asilia; mambo ambayo yana athari sana kwa maisha ya binadamu pamoja na kuhatarisha baadhi ya viumbe hai kutoweka kabisa kutoka katika uso wa dunia. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kunahitajika uhuru wa kudhibiti na kusimamia teknolojia, ili iweze kutumika kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu, yanayozingatia utu, mahitaji msingi ya jamii na utimilifu wake. Wadau wengi wa utunzaji bora wa mazingira wanaendelea kujiunga katika mchakato wa maboresho ya mazingira. Hii inaonesha kwamba, si rahisi sana kuweza kutenganisha mazingira nyumba ya wote, haki kwa ajili ya maskini, majitoleo kwa jamii na amani ya ndani. Elimu ya utunzaji bora wa mazingira inapania pamoja na mambo mengine kukazia ikolojia linganifu, utulivu nyoyoni na viumbe wengine duniani; amani kati ya watu wa Mungu pamoja na Mwenyezi Mungu.

Hii ni ikolojia inayosimikwa katika kanuni maadili na utu wema. Wanasayansi wanasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kupambana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, sanjari na kurejesha mahusiano mema na mazingira. Tahadhari nyingi zimetolewa na kati ya hizi ni janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; na Ongezeko la kiwango cha joto duniani linalojitaji Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua zaidi. Umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unahitajika sana na kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (Cop26) utakaofanyika mjini Glasgow nchini Uingereza. Baba Mtakatifu anasema, bayianuai ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya ekolojia. Kumbe, kuna haja ya kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa kwa kulinda asilimia 30% ya dunia kama hifadhi maalum hadi kufikia mwaka 2030, ili kuondokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na kupotea kwa bayoanuai. Ni wakati muafaka wa kuragibisha umuhimu wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Ni wakati wa kurekebisha mfumo wa uchumi na malengo yake; mfumo wa maendeleo ili hatimaye, kufanya marekebisho katika mifumo ambayo inahatarisha na kuharibu mazingira. Binadamu anapaswa kuchukua hatua ya kwanza kwa kufanya wongofu wa kiikolojia na kwamba, kipindi hiki kisaidie kujenga huruma kwa kujikita katika kipaji cha ubunifu na ujasiri.

Papa Mazingira

 

04 June 2021, 15:36