Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kikao cha 42 cha FAO: Sera na mikakati makini dhidi ya baa la njaa duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kikao cha 42 cha FAO: Sera na mikakati makini dhidi ya baa la njaa duniani. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mkutano wa 42 wa FAO 2021

Baba Mtakatifu Francisko anaipongeza na kuendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kuhakikisha uzalishaji mkubwa wa chakula kwa kutumia kilimo bora na cha kisasa; utunzaji bora wa mazingira na uoto wa asili; kwa kukuza na kudumisha uchumi wa mizani sanjari na maboresho ya soko la mazao ya wakulima kutoka vijijini, bila kusahau uhuru wa kiuchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Umepelekea kuyumba na hatimaye, kuchechemea kwa huduma ya afya na ukuaji wa uchumi. Ni ugonjwa ambao umevuruga mahusiano na mafungamano ya kijamii kutokana na kiwango chake kikubwa cha maambukizi. Hali hii imechochea pia uhaba wa chakula; ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula kwa mamilioni ya watu! Bado kuna watu wanaopata lishe duni na isiyotosheleza hata kidogo mahitaji ya binadamu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita idadi ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa duniani imeongezeka maradufu. Kiwango hiki kinawezekana kuongezeka zaidi kutokana na: athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuyumba kwa uchumi wa kitaifa na Kimataifa. Ili kuweza kuwahudumia watu wote hawa kuna haja ya kuibua sera na mbinu mkakati zitakazosaidia maboresho ya mfumo wa chakula duniani pamoja na kuwaunganisha watu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuanzisha mfumo wa uchumi shirikishi, utakaowawezesha watu wengi zaidi kunufaika na rasilimali pamoja na utajiri wa nchi husika; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili ya nishati rafiki kwa maendeleo yanayokita mizizi yake kwa mahitaji msingi ya binadamu, utu, heshima na haki zake msingi. Mfumo wa uhakika na usalama wa chakula duniani, hauna budi kuhakikisha kwamba, baa la njaa linadhibitiwa kikamilifu, kwa kuwekeza katika kilimo cha familia pamoja na kuwajengea uwezo wakulima vijijini. Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula na biashara hao ndio wahanga wa kwanza wa baa la njaa duniani. Kuna mamilioni ya watu wanaoishi vijijini na sehemu kubwa ya maisha yao kwa kiasi kikubwa yanategemea sekta ya kilimo. Lakini kutokana na uhaba wa soko; ukosefu wa ardhi bora kwa kilimo; ukosefu wa mitaji ya kilimo kikubwa; miundo mbinu na teknolojia. Katika muktadha kama huu, watu wanaoishi vijijini wako kwenye hatari kubwa ya kupekenywa na baala njaa na utapiamlo. Hii ni sehemu ya ujumbe alioandika Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Bwana Michał Tadeusz Kurtyka, Waziri wa Mazingira kutoka Poland ambaye kwa sasa ndiye Rais wa Mkutano 42 wa FAO uliofunguliwa tarehe 14 na unatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 18 Juni 2021 hapa mjini Roma.

Baba Mtakatifu anaipongeza na kuendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kuhakikisha uzalishaji mkubwa wa chakula kwa kutumia kilimo bora na cha kisasa; utunzaji bora wa mazingira na uoto wa asili; kwa kukuza na kudumisha uchumi wa mizani sanjari na maboresho ya soko la mazao ya wakulima kutoka vijijini, bila kusahau uhuru wa kiuchumi. Pasipokuwepo na shinikizo linalotoka kwa wananchi na taasisi za kiraia, mamlaka za kisiasa zitashindwa kufanya utekelezaji wa sera hizo wakati ambapo mambo muhimu yanahitaji kutekelezwa haraka. Utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni muhimu sana katika kupambana na tabia ya uchoyo na ubinafsi inayojionesha katika jamii ya mwanadamu. Watu wote wa familia ya Mungu wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani, kwa kuheshimu zawadi ya maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuondokana na Virusi vya kutojali wala kuguswa na mahitaji ya wengine.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, sera na mikakati ya kilimo bora si mali kitu, ikiwa kama sera hizi hazifanyiwi kazi ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kupata matokeo chanya. Ni wakati wa kuendeleza mchakato wa ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, kujenga jamii inayokita mizizi yake katika mchakato wa maboresho ya elimu, majadiliano na haki sawa kwa wote! Huu unapaswa kuwa ni uwajibikaji wa mtu binafsi na familia ya binadamu katika ujumla wake. Ni changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya “kuchakazwa na tabia ya uchoyo na ubinafsi”. Huu ni mwaliko wa kushirikiana na kushikamana na kamwe asiwepo mtu awaye yote anayebaki nyuma katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawatakia wajumbe wote mkutano mwema na kwamba, anatambua mchango wao katika mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Papa Francisko FAO 2021
15 June 2021, 15:47