Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano 109 wa Shirika la Kazi Duniani, ILO Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano 109 wa Shirika la Kazi Duniani, ILO 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mkutano wa 109 wa ILO, Juni 2021

Jumuiya ya Kimataifa inapopambana na athari za Ugonjwa wa UVIKO-19 kuna haja ya kutoa kipaumbele kwa mafao ya wengi; kuangalia Ddhamana na Utume wa ILO na Utume wa Kanisa katika Ulimwengu wa wafanyakazi Kukuza majadiliano, haki za wafanyakazi na mshikamano kati ya Vatican na ILO kwa kulinda mifumo mbalimbali ya kazi inayosimikwa katika: uhuru, haki na usawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Rais Moon Jae-in wa Korea, Rais Fèlix Antoine Tshisekedi Tshilombo wa DRC, Waziri mkuu Antònio Costa wa Ureno pamoja na Rais Joe Biden wa Marekani ni kati ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa ambao wameshirikisha hotuba zao katika mkutano wa 109 wa Shirika la Kazi Duniani ILO. Baba Mtakatifu katika hotuba yake elekezi wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapopambana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kuhakikisha kwamba, inatoa kipaumbele kwa mafao ya wengi. Kuendelea kukazia dhamana na Utume wa ILO; Dhamana na Utume wa Kanisa katika Ulimwengu wa wafanyakazi: majadiliano, haki msingi za wafanyakazi, majadiliano na mshikamano kati ya Vatican na ILO kwa kulinda mifumo mbalimbali ya kazi inayosimikwa katika: uhuru, haki, fursa sawa kwa watu wote na huduma msingi kwa wafanyakazi. Changamoto za ulimwengu wa wafanyakazi zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu kama sehemu ya upendo wa kisiasa, kwa kukazia unabii na ubunifu. Shirika la Kazi Duniani ILO, kuanzia tarehe 17 hadi 18 Juni 2021 linafanya Mkutano wa Kimataifa wa 109 kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru Bwana Guy Ryder, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani, kwa kumpatia nafasi ya kuweza kuchangia mawazo yake katika mkutano huu. Amelipongeza Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa utekelezaji wa majukumu yake sanjari na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza. Jambo la msingi kwa wakati huu ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi kwa kufanya maamuzi makini, ili kuokoa nafasi na muda wa kazi, kwani kwa sasa kuna kazi na biashara nyingi ambazo zimefungwa au zinakaribia kufungwa. Mwaka 2020 umeshuhudia wafanyakazi wengi wakipoteza fursa za kazi kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumbe, kuna haja ya kuondokana na tabia ya kujenga kuta za utengano kwa kisingizio cha utaifa hali ambayo itapelekea watu wengi kukosa fursa za ajira. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutafuta mbinu mkakati utakaoendeleza fursa za ajira zinazosimikwa katika kazi nzuri zinazoheshimu utu na haki msingi za wafanyakazi; ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, tayari kulinda na kudumisha jamii sanjari na kujielekeza zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, haina budi kuzingatia utu wa binadamu kama kigezo msingi.

Shirika la Kazi Duniani, ILO linayo dhamana kubwa katika mchakato wa majadiliano, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wafanyakazi ambao wengi wao bado wameathirika kutoka na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna wafanyakazi wanaolipwa kwa kutwa, wengi wao hawana fursa za ajira tena, bila kuwasahau wakimbizi na wahamiaji na wale wote wanaofanya kazi katika sekta zisizo rasmi. Hawa ndio wale wanaoorodheshwa kwenye kundi la wafanyakazi lililoko hatarini, wafanyakazi wachafu na wasio na hadhi. Wengi wa wale wanaofanya kazi katika makundi haya hawana hata bima ya afya kwa familia zao na wengi wao wanajikuta wakisukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii na matokeo yake, wengi wao wamepoteza maisha na fursa za ajira kutokana na UVIKO-19. Ukosefu wa hifadhi na usalama wa kijamii utapelekea watu wengi kuendelea kuathirika kutokana na UVIKO-19. Matokeo yake ni kuongezeka kwa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na kushamiri kwa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Yote haya yanaongeza hatari ya maambukizi UVIKO-19 kwa wazee na wagonjwa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema ni dhamana na wajibu wa Mama Kanisa kutoa mwaliko kwa wadau mbalimbali kujizatiti katika kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuhakikisha ushiriki wa watu wengi zaidi katika utekelezaji wa dhamana na wajibu huu mtakatifu. Lengo kuu ni ujenzi na uimarishaji wa amani pamoja na hali ya watu kuaminiana na kuthaminiana. Wahanga wakuu ni vijana, wahamiaji na Jumuiya za watu mahalia pamoja na maskini, ambao wanaweza kujikuta kwamba, wametengwa na kuachwa pembezoni mwa majadiliano haya. Ni wajibu wa dini na madhehebu mbalimbali kushiriki katika mchakato huu, ili hatimaye, kujenga jukwaa la majadiliano ili kukuza ustawi wa wengi, ujenzi wa umoja na mshikamano wa kibinadamu pamoja na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote mambo yanayopaswa kutekelezwa katika ngazi mbalimbali za maisha ya watu, kwa kukazia haki na wajibu, ili kuweza kuwa na majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi! Ni wajibu na dhamana ya Kanisa kuhakikisha kwamba, wanafanyakazi wote wanalindwa dhidi ya mambo yale ambayo yanaweza kuathiri ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hawa ni watu wanaopaswa kupewa huduma bora za afya; kuhakikishiwa lishe bora pamoja na mahitaji yao msingi. Mifuko ya hifadhi ya jamii inahamasishwa kujiwekea sera na mikakati itakayohakikisha kwamba changamoto za majanga kama haya zinapatiwa ufumbuzi mapema kwa kuzingatia haki msingi za wafanyakazi pamoja na kuwaruhusu washiriki kwenye vyama vya wafanyakazi kwa kutambua kwamba, hii ni haki yao na wala si huruma. Jitihada zote hizi hazina budi kwenda sanjari na mabadiliko ya mfumo wa uchumi Kimataifa, ili uweze kuwa ni uchumi shirikishi zaidi na hasa baada ya kutikiswa na kuanza kuchechemea kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi, kwa kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu hasa na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya Jumuiya ya Kimataifa, ili hata wao nao waweze kupanda katika ngazi ya maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa, badala ya kutengeneza na kuunda kikundi kidogo cha wasomi!

Kwa siku za usoni, Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa Vatican itaendelea kujielekeza zaidi katika kuragibisha dhidi mifumo yote inayopekenyua haki msingi za wafanyakazi pamoja na kubomoa misingi ya haki jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kunakosekana usawa na kila kitu kimewekwa chini ya sheria za usindani na kuishi kwa wenye uwezo zaidi, ambapo wenye nguvu hula walio wanyonge. Matokeo yake umati wa watu wanajikuta wametengwa na kusukumwa pembezoni, bila fursa za kazi, bila uwezekano na bila ya kuwa na njia yoyote ya kutoka. Rej. Evangelii gaudium no. 53. UVIKO-19 imewakumbusha wanadamu kwamba wate ni sawa na kwamba, kila mmoja wao ana mapungufu yake kama mwanadamu. Huu ni wakati wa kuondokana na mambo yote yanayosababisha ukosefu wa usawa, kwa kuganga na kutibu ukosefu wa haki msingi za binadamu kwa kuhakikisha kwamba, kila mfanyakazi anapata haki zake stahiki pamoja na kujiandalia maisha bora kwa siku za mbeleni pamoja na familia zao kuwa na uhakika wa usalama wa maisha pamoja na vitega uchumi vya familia. Kumbe, haki na wajibu ni sawa na chanda na pete kwa sababu vinakamilishana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kanisa Katoliki na Shirika la Kazi Duniani ILO, licha ya tofauti na shughuli zake msingi, yanaweza kushirikiana kwa kutambua na kuthamini “dhana ya kazi isiyo rasmi”; kwa kuwatambua wanawake wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi na kwamba, mara nyingi, hili ni kundi linalo tumbukizwa kwa urahisi katika baa la njaa, umaskini na magonjwa. Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu wanawake wasiokuwa kwenye orodha ya uchumi rasmi. Hawa ni wanawake wanaofanya kazi za majumbani na wengi wao ni “akina Mama Ntilie”. Wote hawa wanahitaji huduma ya hifadhi na usalama wa jamii. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limepelekea kilio kikubwa cha wanawake katika masuala ya: uhuru, haki, usawa na fursa kwa wote. Wanawake wamekumbana na nyanyaso, ukatili, vipigo vya majumbani pamoja na kutumbukizwa kwenye mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na mfumo dume. Wanawake hawana nafasi ya fursa na ujira sawa hata kama kazi ni ileile tu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kazi inapaswa kusaidia mchakato wa umoja na mafungamano ya kijamii kwa njia ya huduma makini kwa jirani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mambo yote haya yanahitaji utamaduni wa upendo, umoja na mshikamano wa kweli. Utandawazi usiowajali wengine ni hatari sana. Kumbe majiundo ya kiakili na kitamaduni ni vyema zaidi. Baba Mtakatifu anawakumbusha wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa 109 wa ILO, kuhusu dhamana na wajibu wao bil kusahau utekelezaji wao unaojikita katika uchumi shirikishi. Wanasiasa na viongozi wa Serikali wajitahidi kujenga upendo wa kisiasa ambao ni huduma msingi kwa siku za usoni, kwani inajihusisha na mwingiliano na mafungamano ya watu, tayari kuleta mabadiliko yanayokusudiwa. Dhana ya upendo katika siasa itasaidia kupambana na baa la njaa duniani, ujinga na umaskini kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na haki zake msingi. Kila binadamu anahamasishwa kuhakikisha kwamba, anashiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo binafsi na jamii katika ujumla wake. Ili kutekeleza dhamana na wajibu huu, watu hawana budi kujengewa uwezo wa kiuchumi na kiteknolojia.

Vyama vya wafanyakazi havina budi kujenga mshikamano na mafungamano ya kijamii, ili kukabiliana na changamoto mambaoleo. Viongozi wa wafanyakazi wanaitwa kutekeleza dhana na ushuhuda wa kinabii mahali pa kazi, kwa kusimamia haki, usawa, ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi wote kwa kuondokana kabisa na kishawishi cha rushwa na ufisadi. Vyama vya wafanyakazi licha ya kuwa nabii vinapaswa kuwa na ubunifu kwa kuwalinda wale ambao bado hawana haki, watu waliotengwa katika demokrasia pamoja na mambo mengine. Mwishoni mwa ujumbe wake kwa wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa 109 wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwahakikishia wajumbe wote uwepo wa Kanisa linalotembea pamoja nao bega kwa bega. Kanisa linapenda kutoa rasilimali zake msingi zinazobubujika kutoka katika: amana na utajiri wake wa maisha ya kiroho, sanjari na Mfundisho Jamii ya Kanisa. Binadamu wote wakumbuke kwamba, wamepanda mashua moja, wataweza kuokoka, ikiwa kama watakuwa wameungana na kushikamana kama binadamu!

Papa ILO 2021

 

 

17 June 2021, 16:29