Tafuta

Papa Francisko katika Ujumbe wake kwa Globsec Bratislava anakazia: Umuhimu wa kuona, kuamua na kutenda. Papa Francisko katika Ujumbe wake kwa Globsec Bratislava anakazia: Umuhimu wa kuona, kuamua na kutenda. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Jukwaa la GLOBSEC Bratislava!

Papa Francisko amekazia kuhusu: Kuona, Kuamua na Kutenda. Haya ni mambo msingi katika mchakato wa ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi baada ya janga la UVIKO-19. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya upembuzi yakinifu mintarafu masuala ya uchumi na jamii; Ikolojia sanjari na Sera na Mikakati ya Ulinzi na Usalama kwa sababu mambo yote haya yameungana na kutegemeana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

GLOBSEC Bratislava Forum ni Jukwaa lililoibuliwa na wanafunzi takribani miaka kumi na sita iliyopita kama mahali ambapo vijana kutoka sehemu mbalimbali za Umoja wa Ulaya wangeweza kushirikisha mawazo yao kwa uhuru mpana zaidi. Ni jukwaa ambalo linatoa fursa kwa wataalamu vijana kujadili changamoto mamboleo; kuboresha mfumo wa utungaji wa sera na mikakati kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, tayari kuboresha mwelekeo wa maisha yao kwa siku za usoni. “GLOBSEC Bratislava Forum” kwa Mwaka 2021 limezinduliwa tarehe 15 na linatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 17 Juni 2021. Pamoja na mambo mengine “GLOBSEC Bratislava Forum” linajikita zaidi katika kuchambua athari za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Ufufuaji na ukuzaji wa uchumi; mchakato wa maboresho ya demokrasia, usalama, biashara na afya. Uhusiano wa Kisiasa kati ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU na Marekani. Jukwaa hili linanogeshwa na kauli mbiu “Ujenzi wa Dunia Iliyo Bora Zaidi”.

Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa: Kupyaisha mchakato wa demokrasia kwa kuaminiana na kushikamana; Kuboresha na kukuza uchumi fungamani sanjari na maboresho ya sekta ya afya baada Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mambo mengine ni utawala bora katika ulimwengu wa kidigitali; Ulinzi na Usalama kwa Karne 21 pamoja na uthabiti katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa walioalikwa kwenye “GLOBSEC Bratislava Forum” kwa Mwaka 2021. Katika hotuba yake kwa njia ya video amekazia kwa namna ya pekee kabisa mambo makuu matatu: Kuona, Kuamua na Kutenda. Haya ni mambo msingi katika mchakato wa ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya upembuzi yakinifu mintarafu masuala ya uchumi na jamii; Ikolojia sanjari na Sera na Mikakati ya Ulinzi na Usalama kwa sababu mambo yote haya yameungana kwa pamoja, kwani yanategemeana na kukamilishana.

Baba Mtakatifu anawaka wajumbe wa “GLOBSEC Bratislava Forum” kwa Mwaka 2021 kufanya upembuzi wa kina na mapana; katika ukweli na uaminifu, ili kuangalia yaliyopita kwa jicho makini zaidi. Hii ni pamoja na mapungufu yaliyojitokeza katika mifumo mbalimbali; makosa yaliyotendeka pamoja na ukosefu wa uwajibikaji kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mapungufu yaliyopelekea utengano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, ili kusahihisha na kurekebisha pale “palipo pinda” pamoja na kuangalia mambo yaliyopelekea kuzuka kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ili kuweza tena kusimama na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya tathmini ili kubaini mambo msingi yaliyopelekea kuanguka kwa misingi hiyo pamoja na kuwajibika. Kwa bahati mbaya sana, walimwengu walidanganyika na kuhadaika kwa mifumo ya uhakika wa usalama wao uliojikita kwa namna ya pekee kabisa katika umaarufu na uwezo wao kifedha. Huu ni mtindo wa maisha, mfumo wa uchumi na kijamii unaotengeneza uchoyo na ubinafsi; pamoja na ukosefu wa misingi ya usawa. Kuna idadi ndogo sana ya watu wanaomiliki na kuendesha rasilimali na utajiri wa dunia hii, wakati umati mkubwa wa watu ukiteseka.

Hii ni jamii ambayo haijishughulishi sana na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni jamii ambayo imejidekeza kwa kula kupita kiasi na kuharibu mazingira bila ya kukumbuka kwamba, hata wengine wanapaswa kufaidika na rasilimali hii ambayo inapaswa kulindwa, kutunza na kuendelezwa. Vijana wa kizazji kijacho wasitwike mizigo ya madeni ya ikolojia kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa “GLOBSEC Bratislava Forum” kuthamini kile ambacho wamekiona. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umepelekea changamoto mpya na zenye majaribu makubwa zinazohitaji maamuzi thabiti. Hapa watu wanapaswa kuamua na kuchagua: mahali pema au pabaya; kusuka au kunyoa! Hapa watu kamwe hawawezi kutoka jinsi walivyoingia katika janga hili. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kuboresha hali ya maisha na hatimaye, kusonga mbele, kwa kutambua kwamba, hakuna hata mtu mmoja anayeweza kujiokoa mwenyewe. Watu wanapaswa kutambua kwamba, binadamu wote ni sawa wanaopaswa kupata fursa na haki sawa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa sasa kutenda bila kuchelewa ili kupambana na ukosefu wa usawa wa kijamii na mambo yanayopelekea watu kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Changamoto ya UVIKO-19 inawataka watu kujielekeza zaidi katika mfumo wa maendeleo fungamani ya binadamu, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika utu na mahitaji yake msingi: Huyu ni binadamu anayepaswa kulindwa, kutunza na kuendelezwa kwa kuzingatia kanuni maadili ya mshikamano wa binadamu na siasa ya upendo, ili kuwatangazia na kuwashuhudia wengine Injili ya matumaini. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutenda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, changamoto inayohitaji toba na wongofu wa ndani. Maamuzi makini yatakayogeuza utamaduni wa kifo kuwa ni Injili ya maisha; maamuzi yatakayogeuza silaha kuwa ni chakula kwa ajili ya watu wanaopekenyuliwa na baa la njaa duniani. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katika wongofu wa Kiikolojia, ili kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wajumbe wa “GLOBSEC Bratislava Forum” kwa Mwaka 2021wataweza kushirikishana mfumo wa maisha wenye uwezo wa kutoa majibu sahihi; kwa kujikita katika ushirikishwaji; sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu yanayosimikwa katika msingi wa haki, amani na maridhiano. Kumbe, kuna haja ya kuwa na amani na utulivu na Fumbo la Kazi ya Uumbaji.

Globsec

 

 

 

15 June 2021, 14:58