Tafuta

Papa Francisko ametuma ujumbe kwa washiriki wa Jukwaa la Furaha ya Upendo ndani ya familia. Papa Francisko ametuma ujumbe kwa washiriki wa Jukwaa la Furaha ya Upendo ndani ya familia. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Jukwaa la Amoris Laetitia

Jukwaa hili ni mahali muafaka pa majadiliano kati ya Vatican, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, vyama vya kitume pamoja na utume wa familia. Kanisa linajiaminisha chini ya maongozi na nguvu za Roho Mtakatifu, ili jukwaa hili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Ni muda kwa Kanisa na viongozi wake pamoja na waamini walei, kukaa kwa pamoja ili kusikiliza mahitaji msingi ya familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia Jumatano tarehe 9 Juni 2021 hadi Jumamosi tarehe 12 Juni 2021 linaendesha Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Forum Amoris Laetitia” ili kutathimini mahali ambapo hadi sasa Kanisa limefikia katika mchakato wa utekelezaji wa Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko takribani miaka mitano iliyopita. Hii ni fursa ya kuangalia utekelezaji wa Wosia huu wa Kitume kwa kuzama na kuangalia maisha na malezi endelevu ya ukatekumeni katika maisha ya ndoa na familia. Ni wakati wa kusikiliza shuhuda kutoka kwa wanandoa ili kupata: uzoefu, mang’amuzi, matatizo, fursa na changamoto katika maisha ya ndoa na familia. Ni wakati wa kuendelea kukazia majiundo makini na endelevu kwa wale wote ambao wamepewa dhamana na wajibu wa kuwasindikiza wanandoa katika maisha yao. Jukwaa hili linawahusisha wawakilishi kutoka katika Mabaraza 60 ya Maaskofu Katoliki na zaidi ya vyama vya utume wa familia 30 kutoka sehemu mbalimbali za dunia vinashiriki katika mkutano huu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Jukwaa hili ni mahali muafaka pa majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya Vatican, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, vyama vya kitume pamoja na utume wa familia. Kanisa linajiaminisha chini ya maongozi na nguvu za Roho Mtakatifu, ili jukwaa hili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Ni muda muafaka kwa Kanisa na viongozi wake pamoja na waamini walei, kukaa kwa pamoja ili kusikiliza mahitaji msingi ya familia, changamoto na fursa zilizopo, tayari kupyaisha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika maisha na utume wa Kanisa. Jambo la msingi wanalipaswa kujiuliza, Je, mchakato wa utekelezaji wa Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” umefikia wapi? Huu ni wakati wa kufanya mang’amuzi ya Kikanisa mintarafu mtindo wa maisha ya ndoa na familia na hatima yake kadiri ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda makini wenye mvuto na mashiko! Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” ni matunda ya tafakari ya kina iliyofanywa wakati wa maadhimisho ya Sinodi kuhusu maisha ya ndoa na familia. Wosia huu unahitaji uvumilivu mkubwa ili kuweza kuumwilisha katika maisha na vipaumbele vya Kanisa.

Huu ni wongofu wa kimisionari. Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Forum Amoris Laetitia” ni mchakato wa mwendelezo wa hija ya Sinodi juu ya maisha ya ndoa na familia ambayo kwa sasa inapaswa kuzamisha mizizi yake kwenye Makanisa mahalia. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kukuza: ushirikishaji na ushirikiano, ili kung’amua na hatimaye, kujenga mazingira yatakayoliwezesha Kanisa mahalia kuwa karibu zaidi na familia. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko uliotolewa tarehe 9 Juni 2021 kwa wajumbe wanaoshiriki kwenye Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Forum Amoris Laetitia” ili kutathimini mahali ambapo hadi sasa Kanisa limefikia katika mchakato wa utekelezaji wa Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limeendeleza maumivu, uovu na ukatili, vitu ambavyo vinapelekea familia nyingi kuvunjika na hivyo kupoteza ushirikiano wa maisha na upendo. Huu ni muda muafaka kwa Mama Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha familia, kwa kuwashirikisha wadau wote wa familia katika mpango mkakati wa utume wa ndoa na familia.

Kama ilivyo katika mchakato wa uinjilishaji kuwa ni wajibu na utume wa wabatizwa wote, hivi ndivyo inavyopaswa kufanyika hata kwenye utume wa ndoa na familia. Utume wa familia unapania kunogesha upendo wa Mungu katika maisha ya kifamilia, kwa kuwajengea vijana uwezo wa kuanzisha familia zao. Wanafamilia washirikiane bega kwa bega na viongozi wao wa Kanisa ili kutangaza na kushuhudia: utakatifu, ukuu, ukweli, uzuri na Changamoto za maisha ya ndoa na familia! Huu ni muda muafaka wa kusaidiana na kushikamana ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kwa kutambua kwamba, hata katika magumu na changamoto za maisha, Kristo Yesu bado anaendelea kuwepo katika Sakramenti ya Ndoa, ili kuwakirimia wanandoa: upendo, uvumilivu na matumaini kwa watu wote kila mtu kadiri ya hali yake ya maisha! Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanandoa na familia kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kwa vijana, ili hatimaye, vijana waweze kuona kwa macho yao wenyewe uhalisia wa maisha ya ndoa na familia na kwamba, kufunga ndoa ni jambo linalowezekana na wala si ndoto ya kufikirika.

Mama Kanisa anawahitaji wadau mbalimbali watakaoshirikiana naye katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Ikumbukwe kwamba, Ndoa ni Sakramenti ya huduma ya kitume inayowapatia wanandoa utume maalum wa ujenzi wa Kanisa. Wao wanatekeleza Ukuhani wa waamini wote katika Sakramenti. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, kumbe wazazi wanapaswa kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa imani kwa ajili ya watoto wao, kwa maneno, lakini zaidi kwa matendo, ili kuwasaidia na kuwaelekeza watoto katika miito mbalimbali ya maisha. Upendo wa dhati unaobubujika kutoka katika familia una nguvu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, wanandoa wote wanakuwa ni amana na utajiri wa Kanisa. Baba Mtakatifu anakazia utume unaotekelezwa na viongozi wa Kanisa. Anawaomba wajitahidi kujiaminisha chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, ili kushirikiana kikamilifu na wanandoa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Wapewe nafasi ya kushirikisha ujenzi wa umoja na mafungamano ya Kikanisa kwa kutambua kwamba, watu wote wa Mungu wanahitajiana ili kukamilishana ili kujenga na kuliimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Huu ni umoja katika tofauti unaotekelezwa kwa njia ya miito na hali mbalimbali za maisha ya waamini.

Wongofu wa kimisionari ni muhimu sana katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limekuwa ni fursa ya kuangalia vipaumbele katika maisha na mtindo wa utekelezaji wa vipaumbele hivi. Katika Waraka wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, furaha inayobubujika kutoka katika imani inaganga na kuponya madonda na changamoto za maisha na utume wa Kanisa, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya kueneza Furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Yesu katika: Neno lake, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kwa jirani. Wosia huu ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, unatoa mwelekeo wa Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.

Ni waraka unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka na kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao. Baba Mtakatifu anachambua kwa kina na mapana tasaufi ya maisha ya ndoa na familia zawadi kubwa ambayo watu wa ndoa wamebahatika kuipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanayopaswa pia kuwashirikisha jirani zao. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia yameibua matatizo, changamoto na fursa katika maisha na utume wa familia. Kanisa limegundua sera kandamizi zinazokwamisha mchakato wa malezi na makuzi bora ya watoto ndani ya familia; matatizo na changamoto ya mahusiano na mafungamano ya kifamilia; umaskini wa hali na kipato pamoja na upweke hasi unaowapelekea wanandoa wengi kushindwa kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao.

Changamoto zote hizi zinahitaji mwamko mpya wa shughuli za kichungaji hususan: maandalizi makini kwa ajili ya wanandoa wapya; umuhimu wa kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wao; huduma makini kwa wazee; ukaribu wa Mama Kanisa kwa familia zenye makovu na machungu ya maisha; au watu wa ndoa waliotengana na hatimaye kuoa au kuolewa tena, wote hawa wanahitaji kupewa mwamko mpya katika maisha na mang’amuzi yao ya Kikristo! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Forum Amoris Laetitia” ni muda muafaka wa kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji. Ni fursa ya kujenga na kudumisha mtandao wa miito ili kukamilishana na hatimaye, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, kwa ufanisi mkubwa sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Papa Jukwaa la Upendo
10 June 2021, 16:33