Tafuta

Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inaadhimishwa tarehe 25 Julai 2021 ili kuthamini mchango unaotolewa na wazee katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inaadhimishwa tarehe 25 Julai 2021 ili kuthamini mchango unaotolewa na wazee katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. 

Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani Jumapili 25 Julai 2021! Maandalizi

Siku ya Wazee Duniani itakuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani unanogeshwa na kauli mbiu “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20! Waamini wajiandae kikamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 31 Januari 2021 alitangaza kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 itaadhimishwa Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inayokaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Siku ya Wazee Duniani itakuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 22 Juni 2021 anatarajia kuwasilisha ujumbe wake kwa maadhimisho haya kwa waandishi wa habari mjini Vatican. Ujumbe huu unanogeshwa na kauli mbiu “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Hii ni ahadi ya uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Vijana wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujikita katika maisha ya sala, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wazee wanaweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kutekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, linawaalika waamini wote katika Makanisa mahalia kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho haya, ili kukoleza moyo wa uinjilishaji kwa kutambua kwamba, wazee wa ndoto na vijana wana unabii kama ambavyo anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Wazee Duniani iwe ni fursa ya kuboresha mahusiano haya ya kifamilia, kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wazee, ambao wanayo mengi ya kuwafundisha na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii.

Kwa upande wake, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, haya ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na utahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.  Utume wa Kanisa miongoni mwa wazee ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika shughuli za kichungaji zinazoendeshwa na Makanisa mahalia. Jamii inapaswa kuheshimu na kuthamini amana na utajiri unaobubujika kutoka kwa wazee kizazi kimoja hadi kingine. Hii ni changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine, ili kuendelea kuenzi na kuthamini karama, amana na utajiri wa wazee ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Siku ya Wazee Duniani itaadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili jioni tarehe 25 Julai 2021. Yote haya yatategemea itifaki ya kudhibiti maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Makanisa mahalia yanahimizwa kuadhimisha Siku hii kadiri inavyofaa mintarafu vipaumbele na shughuli zao za kichungaji.

Baba Mtakatifu Francisko, katika Waraka wake wa Kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” hususan ile Sura ya tatu: Mwelekeo kwa Yesu: Wito wa familia, anawaalika kwa namna ya pekee, wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na utume wao ndani ya Familia. Wazazi na walezi watambue kwamba, wao ni wadau wa kwanza wanaoshirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji, malezi na makuzi ya watoto wao kwa sasa na kwa siku za usoni. Wazazi wake Bikira Maria, wanaonesha na kushuhudia umuhimu wa familia kama shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha. Sikukuu hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Matukio kama haya ni fursa ya kukuza na kudumisha ndani ya nyoyo za watu: faraja, upendo, huruma, imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu aliye asili ya wema na utakatifu wa maisha.

Wazazi na walezi wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani miongoni mwa watoto wao. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, wazazi wawasaidie watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbali mbali za maisha ya uzeeni bado wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume, “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” anasifu heshima inayotolewa na familia ya Mungu Barani Afrika kwa wazee wao, kwani wao ni utajiri, hawatengwi wala kudharauliwa bali, wanabaki kama miamba na walezi wakuu wa mila, desturi na tamaduni njema katika jamii. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujifunza namna ya kuheshimu na kuwathamini wazee kutoka Afrika. Uzee, umaskini na magonjwa visiwe ni sababu ya kuwatenga na kuwakosea heshima wazee katika jamii. Anaichangamotisha jamii kwa ujumla kutambua kuwa wazee ni msingi wa uhai na maendeleo fungamani ya binadamu. Huu ndio mwongozo wa wongofu wa ikolojia ya binadamu, ili kufikiri na kutenda kiutu, kwa huruma na upendo; kwani mambo yote haya yanahusiana na kukamilishana. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wajifunze kuenzi, kuheshimu na kuthamini tamaduni zao. Hii ni changamoto muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya kupyaisha mizizi ya tamaduni zao, kama sehemu muhimu sana ya utambulisho wao. Vijana wa kizazi kipya wajenge na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi na wazee. Wazazi wajenge utamaduni wa kuzungumzana na watoto wao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazee wana ndoto za kinabii wakati vijana wana maono ya maisha. Ushuhuda ni mahali ambapo waamini wanaweza kugundua mpango wa Mungu katika maisha yao na kwamba, hii ndiyo ekolojia ya kibinadamu! Umuhimu wa Neno la Mungu, Maskini na Wazee ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Baba Mtakifu Francisko kwa wakati huu, lakini pia vina mwelekeo wa matumaini kwa sas ana kwa siku za usoni. Vijana na wazee wanategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha yao yak ila siku. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Vittorio Scelzo, Afisa wa Huduma za Kichungaji kwa Wazee, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Siku ya Wazee Duniani ni mwendelezo wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu: uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa pia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Maskini Duniani ambayo ni matunda ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa mara ya kwanza imeadhimishwa kunako mwaka 2017.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kumbukumbu endelevu ya huruma ya Mungu inayopaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa waamini katika ujumla wao. Siku hii ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini.  Hii ni alama ya kwanza ya huduma kwa maskini kutokana na utambuzi kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika udugu na mshikamano. Yesu mwenyewe aliwapatia maskini kipaumbele cha kwanza katika Heri za Mlimani kwa kusema, “Heri maskini, maana hao watairithi nchi”. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliuza mali na vitu vyake na kuwagawia watu kadiri ya mahitaji yao!

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao” ameanzisha Dominika ya Neno la Mungu itakayokuwa inaadhimishwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Tatu ya Mwaka wa Kanisa. Dominika hii itakuwa ni: kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani huu ni wakati wa kuombea Umoja wa Wakristo. Kristo Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” Lk. 24:45.

Siku ya Wazee Duniani
21 June 2021, 15:54