Tafuta

Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2021 Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2021 

Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2021: UVIKO-19

Umoja wa Mataifa, tarehe 20 Juni 2021 unaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko”. Huu ni mwaliko wa kufungua akili na nyoyo, ili kuonja mateso na magumu wanayokabiliana nayo wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Watu waguswe na furaha, matumaini na majonzi yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 20 Juni 2021, amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Umoja wa Mataifa, tarehe 20 Juni 2021 unaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko”. Huu ni mwaliko wa kufungua akili na nyoyo, ili kuonja mateso na magumu wanayokabiliana nayo wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Watu waguswe na furaha, matumaini na majonzi yao. Wenyeji wajifunze kutoka kwa wakimbizi na wahamiaji kuwa walinzi wajasiri, ili kwa pamoja, waweze kukua na kukomaa kama kielelezo cha Jumuiya ya binadamu inayounda na kujenga familia kubwa ya binadamu! Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2021 ni kumbukumbu ya Miaka 21 tangu Siku ya Wakimbizi Duniani ilipoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2000, kama kumbukumbu ya Mkataba wa Wakimbizi Duniani uliotiwa mkwaju na Jumuiya ya Kimataifa kunako mwaka 1951.

Kwa mara ya kwanza Siku hii imeadhimishwa Mwaka 2020. Jumuiya ya Kimataifa inahamasisha watu kutekeleza vyema dhamana na nyajibu zao na kila mtu kadiri ya nafasi yake. Lengo ni kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanachangia pia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mahali walipo, ikiwa kama sera na mikakati itawashirikisha kikamilifu. Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa pia kupata fursa za elimu, afya na michezo. Kwa kutekeleza haya mambo msingi, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuanza kujikwamua kutoka katika janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni chachu katika mchakato wa uponyaji na kujifunza, ili hatimaye, kuweza kung’ara kwa pamoja. Hakutakuwepo na uhakika wa usalama hadi pale hata wakimbizi na wahamiaji watakapokuwa wamehudumiwa vyema! Kuna umati mkubwa wa wakimbizi kutoka Siria kutokana na vita iliyofumuka kunako mwaka 2011.

Kuna wananchi wa Siria milioni 5.6 wanaoishi kama wakimbizi na wahamiaji. Vita na mauaji nchini Afghanistan imepelekea watu zaidi ya milioni mbili kukosa fursa za ajira na hivyo kuikimbia nchi yao. Kuna wakimbizi Rohingya zaidi ya 742, 000 wanaoishi nchini Bangladesh, lakini wanakumbana na hali ngumu sana ya maisha! Bwana Fillipo Grandi, Kamishna wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, katika taarifa yake anasema kwamba, idadi ya wakimbizi na wahamiaji kutokana na: vita, migogoro, kinzaji na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu imeongezeka hadi kufikia watu milioni 82.4, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4% ikilinganishwa na takwimu zilizotolewa mwishoni mwa mwaka 2019. Bwana Grandi amesema wakimbizi wanastahili msaada wa kimataifa sio tu kupitia misaada ya dharura ya kibinadamu bali kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhisho la kudumu litakalomaliza shida na changamoto za wakimbizi duniani. Bwana Grandi pia ameitaja migogoro ya muda mrefu katika nchi za Siria, Afghanistan, Somalia na Yemen kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwani, nchi hizi zimekuwa ni chimbuko la watu wengi kuyakimbia makazi yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antònio Guterres katika maadhimisho haya anasema, Umoja wa Mataifa hauna budi kujizatiti zaidi ili kukomesha vita, kinzani na migogoro ya kijamii, kidini na kitamaduni. Hii inatokana na ukweli kwamba, migogoro hii inasababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi na nchi zao ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na mateso makubwa kwa maskini na watu wenye kipato cha chini. Taarifa hii imebainisha kuwa janga la UVIKO-19 lilipofika kileleni mnamo mwaka 2020, zaidi ya nchi 160 zilifunga mipaka yake, wakati nchi 99 hazikuwashughulikia kabisa watu waliotafuta hifadhi na usalama wa maisha kwenye nchi mbalimbali duniani. Hata hivyo pamoja na kuwekwa hatua zilizoboreshwa kama vile uchunguzi wa matibabu kwenye mipaka, vyeti vya afya au karantini za muda mfupi mara tu wakimbizi walipowasili, taratibu za usajili zilizorahisishwa na kusikilizwa wakimbizi kwa njia video, nchi nyingi ziliweza kufaulu kuwawezesha wakimbizi hao kupata hifadhi na wakati huohuo hatua za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa UVIKO-19 zilizingatiwa.

Kulingana na taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi, watoto ndio wanaathirika zaidi hasa wakati familia zinapolazimika kuhama makazi yao na kuendelea kuishi uhamishoni kwa miaka mingi inayofuata. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba, takribani watoto millioni moja walizaliwa kama wakimbizi na wahamiaji kati ya mwaka 2018 na mwaka 2020. Taarifa hiyo imesema asilimia 42% ya wakimbizi ni wasichana na wavulana walio chini ya umri wa miaka 18. Wengi wao wako katika hatari ya kuendelea kuishi uhamishoni kwa miaka ijayo na kwa wengine huenda wakaishi uhamishoni maisha yao yote. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, kwa muda wa mwaka mmoja, watu wengi wamejikuta wakiwa wamejifunia majumbani mwao kwa karantini kama sehemu ya itifaki ya kudhibiti maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Watu wamejifunza mbinu na mifumo mipya ya maisha, ili kukabiliana na changamoto ya gonjwa hili ambalo hadi sasa halina tiba! Umoja wa Mataifa unawashukuru na kuwapongeza wale wote waliosimama kidete kulinda, kutetea na kueneza ukweli kuhusu Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kundi hili limewawezesha watu kufuata ushauri sahihi unaotolewa na wanasayansi kama njia ya kuokoa maisha ya watu.

Umoja wa Mataifa utaendelea kuhimiza chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili kuokoa maisha ya watu na kuwasaidia wale wote ambao wameelemewa na mzigo wa gonjwa hili hatari. Hawa ni wanawake na watoto; makundi ya watu wachache ndani za jamii; wazee, walemavu, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum bila kuwasahau watu mahalia! Kwa njia ya chanjo makini dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kuna matumaini ya kuweza kuona mwanga mpya baada ya maafa makubwa kutokea sehemu mbalimbali za dunia. COVAX inapania kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na usawa katika mchakato wa kutoa chanjo, ili hata Nchi zinazoendelea duniani ziweze kupata fursa hii. Jambo la kusikitisha anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ni kuona kwamba, Nchi change zaidi duniani bado hazijafaulu kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19. Hii ni hatari sana kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa.

Kampeni ya Chanjo Kimataifa ni kipimo cha uwajibikaji wa kimaadili duniani, ili kufufua uchumi na kuwawezesha watu kusonga mbele katika maisha. Chanjo ya UVIKO-19 inapaswa kuangaliwa kama sehemu ya mafao ya wengi. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inaunganisha nguvu zake ili kuzalisha chanjo hii na jitihada hizi zinapaswa kuanza mara moja. Kwa njia ya umoja na mshikamano wa kidugu, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kudhibiti maafa makubwa yanayosababishwa na UVIKO-19. Ni kwa njia ya ushirikiano, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufufua uchumi unaoendelea kuchechemea na katika umoja, watu wanaweza kurejea tena katika shughuli na mambo wanayoyapenda!

Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko kuhusu wakimbizi anasema kwamba, hawa si wakimbizi peke yao, bali ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kielelezo cha maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wanyonge, maskini na wagonjwa wanapaswa kusaidiwa na wenye nguvu, ambao watakuwa kama wale Malaika waliokuwa wanapanda na kushuka, vinginevyo maskini hawa wataendelea kubaki nyuma na kudidimia katika umaskini na utupu wao. Huu ni wajibu na dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanashirikiana ili kuleta wokovu na ukombozi kwa watu hawa. Jambo hili linawezekana kwa njia ya umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma, ulinzi na ustawi wa wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni alama ya utu, shukrani na mshikamano wa dhati!

Siku ya Wakimbizi Duniani
20 June 2021, 15:04

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >