Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani waliokolewa na Kristo Yesu na sasa ni mashuhuda wa Injili. Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani waliokolewa na Kristo Yesu na sasa ni mashuhuda wa Injili. 

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Waliokolewa na Kristo Yesu

Papa Francisko: Watakatifu Petro na Paulo Mitume, ni mashuhuda wa imani waliobahatika kukutana mubashara na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, akawa ni chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha yao. Wakaonja huruma na upendo wa Kristo Yesu; akawaponya na kuwaokoa; leo hii wamekuwa ni Mitume na vyombo vya kuokoa wengine kwa ushuhuda wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 29 Juni ya kila mwaka anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani na Mashuhuda wa Upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni siku ambamo Maaskofu wakuu wa Majimbo makuu pamoja na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki wamepewa Pallio Takatifu watakazovishwa majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika. Kwa Mwaka 2021, Baba Mtakatifu Francisko ametoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu 12. Kanisa Barani Afrika linawakilishwa na Askofu mkuu Fulgenze Muteba Mugali wa Jimbo kuu la Lubumbashi nchini DRC. Hii ni siku pia ya kunogesha majadiliano ya kiekumene katika ushuhuda wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa uwepo na ushiriki wa ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol.

Ni siku ya mshikamano kwa kuonesha upendo kwa Baba Mtakatifu kwa njia ya sala, lakini kwa kuchangia katika Mfuko maalum wa huduma ya mshikamano na upendo unaotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, sehemu mbali mbali za dunia. Majimbo mengi wameiadhimisha Siku ya Upendo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumapili tarehe 27 Juni 2021, ili kuwapatia waamini wengi nafasi ya kuchangia katika mfuko kuu: “The Pence of Saint Peter” (L’Obolo di San Pietro). Simoni Petro alikuwa ni mvuvi kutoka Bethsaida na ni kati ya Mitume walioitwa kwanza kabisa na Kristo Yesu. Rej. Mk 1:16-20. Akateuliwa kuwa Mtume wa kwanza kati ya Mitume 12 wa Yesu. Rej. Mt 10:2 na Kristo Yesu akambadilishia na hatimaye akampatia jina jipya, Petro, yaani “Mwamba” na hivyo akapewa dhamana ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani sanjari na kuchunga Kondoo wa wa Kristo! Rej. Mk 16:13-19; Lk 22:31-32; Yn 21:15-19.

Kwa upande wake, Sauli aliyekuwa analitesa na kulinyanyasa Kanisa, akakutana na Kristo Mfufuka mubashara akiwa njiani kuelekea Dameski “kutembeza mkong’oto” na hapo akatubu na kumwongokea Mungu, leo hii anaitwa Mtume Paulo, Mwalimu wa mataifa! Rej. Mdo 9:1-19; Fil 3:12, akaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri ya miamba na mashuhuda wa Injili yaani Watakatifu Petro na Paulo Mitume, amekazia kwamba, hawa ni mashuhuda wa imani waliobahatika kukutana mubashara na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, akawa ni chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha yao. Wakaonja huruma na upendo wa Kristo Yesu; akawaponya na kuwaokoa; leo hii wamekuwa ni: Mitume na vyombo vya kuokoa wengine.

Ni wafuasi huru waliokombolewa na Kristo Yesu; wakaonja mang’amuzi ya Fumbo la Pasaka, changamoto na wito wa Kanisa ni kuwaokoa walimwengu kutoka katika dhambi na mauti; ukosefu wa haki msingi; sanjari na hali ya kukata na kujikatia tamaa! Mtakatifu Petro, Mtume, aliokolewa na Kristo Yesu kutokana na mapungufu yake ya kibinadamu pamoja na kujikatia tamaa baada ya kufanya kazi ya kuchosha usiku kucha, wasipate kitu! Lk 5:5; Yn 21:5. Ni huyu Petro aliyemwona Kristo Yesu akitembea juu ya maji ya bahari akataka naye pia kumwendea akitembea juu ya maji, lakini alipouona upepo, akaogopa akaanza kuzama! Rej. Mt 14:30. Licha ya kuwa ni mwanafunzi mwaminifu wa Kristo Yesu aliendelea kufikiri na kutenda kama walimwengu, bila kufanikiwa kutambua maana ya Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu. Rej. Mt 16:22. Mtakatifu Petro aliyekuwa anajidai kuwa tayari kuyasadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo wakati wa mateso, akaishia kumkana Kristo Yesu mara tatu. Rej. MK 14: 66 – 72.

Hata katika yote haya, bado Kristo Yesu aliendelea kumpenda na kumthamini Mtakatifu Petro sanjari na kuwekeza kwake. Akimtia shime ili atupe nyavu baharini; asimame na kumfuata juu ya Bahari, achunguze na kuangalia kwa umakini mkubwa kuhusu udhaifu wake wa binadamu na baadaye, abebe Msalaba wake kisha aanze kumfuata, akiwa tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya ndugu zake pamoja na kuwachunga Kondoo wa Kristo. Kristo Yesu alimkomboa Mtakatifu Petro na woga, usalama na uhakika potofu wa maisha; hofu na mashaka ya malimwenguna hatimaye, akampatia ujasiri na furaha ya kweli kwa kujikisia kuwa ni mvuvi wa watu, akiwa na dhamana ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Kristo Yesu akampatia funguo za Ufalme wa mbinguni; ili kufunga na kufungua minyororo ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, yote haya yamewezekana kwa sababu ameokolewa kutoka gerezani kama ilivyokuwa hata kwa Waisraeli walipokombolewa kutoka utumwani Misri. Petro Mtume aliambiwa ajifunge mshipi, avae viatu, tayari kutoka nje! Kristo Yesu akamfungulia malango mbele yake, mwanzo wa historia mpya ya maisha: Haya ni mang’amuzi ya Pasaka ya Bwana kwa kutambua kwamba, kwa hakika amekombolewa na Kristo Yesu.

Hivi ndivyo hata Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa alivyo okolewa na Kristo Yesu kutoka katika utumwa uliokuwa unamkandamizia chini katika ubinafsi wake. Kutoka kwa Saulo, jina la Mfalme wa kwanza wa Israeli hadi kuitwa Paulo, maana yake “Mtu mdogo”. Alikombolewa na Kristo Yesu kutoka katika hali, mtazamo na msimamo katika maisha yake. Ni kiongozi aliyejipambanua katika kuwatesa na kuwanyanyasa Wakristo wa nyakati zake. Akaokolewa na Kristo Yesu, badala ya kutumia ukatili wa upanga, akajielekeza zaidi katika upendo wa Mungu uliomwokoa kutoka katika msimamo mkali wa kidini na kiimani na kumkirimia neema ya kuwa ni chombo na shuhuda wa uinjilishaji wa watu wa Mataifa. Mtume Paulo akapambana na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali za maisha ya kitume; akaugua na kuonja kaburi; akateswa na kudhulumiwa; akazama baharini; akashikwa na njaa na kiu ya kufa mtu. Mtume Paulo anasema, “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. 1Kor 12:7-10.

Mtume Paulo akatambua kwamba, “Mwenyezi Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu.” 1Kor 1:27. Mtume Paulo akafanya mang’amuzi ya Fumbo la Pasaka, akaokolewa na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, Petro na Paulo Mitume, Miamba wa imani wameokolewa na Kristo Yesu kwa nguvu ya Injili, kwa sababu kwanza kabisa wameokolewa kwa kukutana mubashara na Kristo Yesu ambaye, hakuwahukumu, kuwadharau wala kuwabeza. Akashirikiana nao kwa upendo na uwepo wake wa karibu; akawaenzi kwa sala na sadaka yake takatifu; akawachangamotisha kutubu na kumwongokea Mungu; walipoteleza na kutopea katika dhambi, aliwaonya kwa moyo wa upendo na huruma; akawaombea na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa Wakristo wanapoteleza na kuanguka dhambini, wakimkimbilia Kristo Yesu, awashika mkono na kuwainua, ili kusonga mbele na hija ya maisha!

Waamini wanakumbushwa kwamba, kwa kuguswa na Kristo Yesu katika maisha yao hata wao pia wameokolewa. Ni katika muktadha huu, Kanisa huru, ni Kanisa linaloaminika. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro Mtume, hata waamini wa nyakati hizi katika ulimwengu mamboleo, wanaalikwa kuwa huru kutoka katika mapungufu na udhaifu wao wa kibinadamu, tayari kushikamana na Kristo Yesu anayewakirimia ujasiri wa kinabii. Kama ilivyokuwa kwa Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa, hata wakristo katika ulimwengu huu wanaalikwa kuachana na unafiki na hatimaye, kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi katika maisha; wamwombe Kristo Yesu, kuwaweka huru kutokana na hofu za kutofahamika na hatimaye, kushambuliwa. Waamini wawe waamni na wapole, kwa kutambua nguvu thabiti za uwepo wa Mungu kati yao. Kanisa Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, liwe huru, ili kuwaokoa watu kutoka katika dhambi na mauti; hali ya kukata na kujikatia tamaa; ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na ukosefu wa matumaini kwa watu wa kizazi hiki!

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, iwe ni fursa ya kuangalia kwa makini, Je, leo hii ulimwengu unataka kuokolewa kutoka katika hali gani? Ni minyororo ipi, inayoendelea kuufunga ulimwengu. Wakristo wanaweza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kazi hii ya ukombozi, lakini jambo la msingi kwanza, lazima waokolewe na upya wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kutembea katika uhuru wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Maaskofu wakuu wamepokea Pallio Takatifu, alama ya umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro; dhamana na utume wa Maaskofu wakuu kuwa ni wachungaji wema, tayari kujisadaka na kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Itakumbukwa kwamba, kuanzia mwaka 2015 Maaskofu wakuu walioteuliwa, pale inapowezekana wanashiriki Ibada ya Misa Takatifu na Baba Mtakatifu, lakini, Pallio Takatifu watavishwa majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika. Lengo ni kuwashirikisha watu wa Mungu wanaounda Jimbo kuu, wakiwa wameungana na Maaskofu mahalia, kushuhudia Askofu wao mkuu akivishwa Pallio Takatifu. Mkazo unawekwa kwenye umoja wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu, Maaskofu mahalia pamoja na waamini wote katika ujumla wao.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, kumekuwepo na utamaduni wa ujenzi wa umoja, ushirikiano na udugu wa kibinadamu na Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Makanisa haya mawili yanatambua kwamba, Petro na Andrea walikuwa ni ndugu wamoja. Huu ni ushuhuda wa uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mwaka 2021 unaongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia. Baba Mtakatifu ametambua, amekiri na kuwashukuru kwa uwepo wao katika maadhimisho haya. Hii ni alama ya umoja katika hija ya ukombozi wa umbali ambao ni kashfa inayowagawa bado Wakristo. Kanisa limesali kwa ajili ya Maaskofu wakuu wapya, viongozi wa Kanisa na waamini wote katika ujumla wao, ili wakiwa wameokolewa na Kristo Yesu, hata wao waweze kuwa ni Mitume wanaojizatiti kuuokoa ulimwengu.

Papa Mashuhuda wa Imani

 

29 June 2021, 15:44