Tafuta

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku ya Kuombea Toba, Wongofu na Utakatifu wa Mapadre Duniani. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku ya Kuombea Toba, Wongofu na Utakatifu wa Mapadre Duniani. 

Sherehe ya Moyo Mt. wa Yesu: Siku ya Kuwaombea Mapadre Duniani!

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku pia ya kuwaombea Mapadre: toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Mungu amependa kukutana na binadamu wote kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Mwaliko kwa waamini wote kuendelea kujiaminisha kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kusema “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mapadre kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu”. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele!  

Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta utakatifu wao, kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi wa amani; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na wakati wa majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye, kupata faraja na usalama wao! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 9 Juni 2021 amesema kwamba, Ijumaa tarehe 11 Juni 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hii pia ni Siku ya Kuwaombea Mapadre: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu amependa kukutana na binadamu wote kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini wote kuendelea kujiaminishwa kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kusema “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.”

Waamini wainogeshe sala hii hasa zaidi wakati wa Mwezi Juni, uliotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waamini wamwombe Kristo Yesu ili aweze kuwafundisha kumpenda Mungu na jirani. Kwa wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya, watambue kwamba, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kisima cha huruma na upendo wa Mungu unaopaswa kuwashwa duniani. Hapa ni mahali ambapo, waamini wanaweza kujichotea imani, matumaini na mapendo thabiti. Baba Mtakatifu anawashauri waamini wasione woga kumtolea Kristo Yesu shida na mahangaiko, wasiwasi, hofu na udhaifu wa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni Sherehe inayopendwa sana na watu wa Mungu. Ni wakati wa kuvumbua amana na utajiri unaohifadhiwa kwenye “sakafu” ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili hatimaye, kujifunza kumpenda Mungu na jirani na hivyo, kujenga utamaduni wa upendo. Waamini wamwombe Kristo Yesu neema na baraka ili waweze kutakatifuza nyoyo zao na hivyo kuondoa makando kando yanayokwamisha ustawi na maendeleo yao ya kiroho. Wamwombe Kristo Yesu kuondokana na kiburi na hali ya kukosa utaratibu katika maisha. Na badala yake, ajaze nyoyo zao upendo na hofu ya Mungu, ili hatimaye, nyoyo za waamini ziweze kupata amani, faraja na utulivu wa ndani.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Juni 2019 aliwakumbusha waamini kwamba, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ukumbusho kwamba, Kristo Yesu anaishi “Christus vivit”. Kristo Yesu anawapenda waja wake, anaendelea kujisadaka kama chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na wokovu wa walimwengu. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia ili kuweza kupata: hifadhi, amani na utulivu wa ndani kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waamini wajitahidi kwenda kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa Sakramenti ya Upatanisho. Kamwe waamini wasisite kujiaminisha chini ya Moyo Mtakatifu wa Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani! Waamini wavutwe na hisia za upendo wa kweli unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Watumie siku hii kwa ajili ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa Mapadre na wanapofanya hivi, wamkumbuke hata yeye katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili maisha na utume wao wote, upate chapa ya upendo wa Mungu kwa wanadamu wote!

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 alitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuendelea kukesha kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha wongofu wa shughuli za kichungaji. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni dalili kwamba, wito na utume huu mtakatifu umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Mapadre wanaopitia vipindi vigumu vya maisha na utume wao, wanapaswa kusindikizwa kwa huruma na upole; wasikilizwe kwa makini; wasaidiwe kufikia mang’amuzi na ukomavu katika maisha. Huu ni wajibu wa kwanza kwa Maaskofu mahalia, lakini hata kwa Jumuiya nzima ya waamini pamoja na familia zao, ambazo mara nyingi zinabeba Msalaba mzito! Wakleri ni watu ambao wanapaswa pia kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wao! Kamwe Mapadre wasidhaniwe kuwa ni mashine za kutolea huduma ya mambo matakatifu! Mapadre wapendwe katika ukweli na uwazi; wasaidiwe kupata mahitaji yao msingi. Waamini walei, wakishirikiana, wakisaidiana na kushauriana na Mapadre wao, maisha na utume wa Kanisa vitasonga mbele kwa ari kubwa zaidi!

Pale Mapadre wanapoonekana kuchoka na kuanza kukata tamaa, waamini wawe mstari wa mbele kuwaenzi kwa sala na sadaka zao; kwa kutambua na kuthamini huduma zao pamoja na ushauri wa udugu wa kibinadamu. Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre, iwe ni fursa ya kuwasindikiza Mapadre katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Katika majitoleo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mama Kanisa anawaalika watoto wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: kushiriki Misa Takatifu, kupokea Ekaristi Takatifu na kutenda matendo ya huruma, kusali sala iliyoelekezwa na Mama Kanisa kama njia ya kulipia madhulumu dhidi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu yafanywayo na watu mbalimbali na hasa kwa kukosa heshima kwa Sakramenti Kuu, yaani Ekaristi Takatifu. Matunda ya majitoleo hayo ni neema zibubujikazo kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu! Ahadi zinazobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu: Nitawajalia neema zote watakazozihitaji katika hali yao ya maisha. Nitawajalia amani katika familia zao. Nitawafariji katika magumu yao yote. Nitakuwa kimbilio lao salama wakati wa maisha yao, na zaidi sana katika saa yao ya kufa. Nitawapa baraka tele katika shughuli zao zote. Wakosefu watapata katika Moyo wangu chanzo na bahari ya huruma isiyo na mwisho. Waamini walio vuguvugu watakuwa na bidii. Waamini wenye bidii watakwea kwa upesi katika ngazi za juu za ukamilifu. “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.”

Moyo Mtakatifu wa Yesu
09 June 2021, 15:51