Tafuta

Tarehe 12 Juni ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo. Tarehe 12 Juni ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo. 

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo: Nyanyaso!

Papa: Haiwezekani kabisa kufumbia macho dhuluma, nyanyaso na ukatili dhidi ya watoto wadogo wanaonyimwa haki yao ya kucheza, kusoma na kuota ndoto ya maisha bora zaidi. Takwimu za Shirika la Kazi Duniani, ILO zinaonesha kwamba, kuna watoto zaidi ya milioni 150 sehemu mbalimbali za dunia, wananyanyaswa, kudhulumiwa pamoja na kufanyiwa ukatili wa kutisha kiasi hiki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ulinzi wa utu na heshima ya binadamu ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake. Hizi ni haki ambazo zimebainishwa kwenye “Tamko la Haki ya Mtoto la Mwaka 1959” na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira salama katika maisha na utu wao. Hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Kristo Yesu anaonya kwamba, Ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini! Utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanafumbatwa katika: Kazi za suluba, ukahaba, biashara ya binadamu na viungo vyake. Kuna masuala ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge.

Matendo yote haya ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu na yanapaswa kutambulika hivi na viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa au kufumbiwa macho! Tarehe 12 Juni ya kila Mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Juni 2021 amekumbushia tena kuhusu maadhimisho haya. Baba Mtakatifu anasema, haiwezekani kabisa kufumbia macho dhuluma, nyanyaso na ukatili dhidi ya watoto wadogo wanaonyimwa haki yao ya kucheza, kusoma na kuota ndoto ya maisha bora zaidi. Takwimu za Shirika la Kazi Duniani, ILO zinaonesha kwamba, kuna watoto zaidi ya milioni 150 sehemu mbalimbali za dunia, wananyanyaswa, kudhulumiwa pamoja na kufanyiwa ukatili wa kutisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kupinga na hatimaye, kung’oa kabisa ajira za watoto wadogo.

Kanisa linataka pia kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kukomesha nyanyaso, biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake; vita na ghasia; mambo yanayofafanuliwa kwa kina na mapana na Umoja wa Mataifa katika Mikakati ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameshuhudia mateso na mahangaiko ya watoto hawa sehemu mbali mbali za dunia, changomoto na mwaliko kwa kuwawezesha tena watoto kuwa na furaha, amani na utulivu wa ndani kwa kuwajengea mazingira bora ya malezi na makuzi. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuunganisha nguvu kwa kujikita katika: haki, ujasiri na furaha ya kuwaangalia watoto machoni pao pasi na kuona aibu! Ikumbukwe kwamba, utu na heshima ya binadamu vinafumbatwa katika kazi yake halali! Kumbe, kazi isiwe ni mahali pa kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu! Kazi ni jina, heshima na utumilifu wa utu wa binadamu! Kila mtu ajisikie kuwa anawajibika kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo!

Papa Watoto
14 June 2021, 15:14