Tafuta

Papa Francisko asikitishwa na vifo vya watoto 215 vilivyotokea "Kamloops Indian Residential School" nchini Canada. Papa Francisko asikitishwa na vifo vya watoto 215 vilivyotokea "Kamloops Indian Residential School" nchini Canada. 

Papa Francisko Asikitishwa na Vifo vya Watoto 215 Nchini Canada

Papa anawahamasisha viongozi wa Serikali na Kidini nchini Canada kuendelea kushirikiana ili hatimaye, ukweli uweze kufahamika, na huo uwe ni mwanzo wa mchakato wa upatanisho na uponyaji wa kitaifa. Huu ni mwaliko wa kuondokana na mifumo ya kikoloni kwa kuthamini haki msingi za binadamu, tunu na amana za kitamaduni kwa watu wote wa Mungu nchini Canada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya wazawa nchini Canada inasema kwamba, ina uthibitisho wa makaburi ya wanafunzi 215 waliozikwa kwenye shule ya “British Columbia School”, moja ya shule zilizokuwa zimetengwa ili kutoa nafasi kwa wazawa kuweza kushiriki katika maisha ya jamii nzima. Makaburi haya yamegunduliwa kwenye eneo la “Kamloops Indian Residential School” iliyofanya kazi zake kuanzia mwaka 1890 hadi mwaka 1970. Hawa ni wanafunzi waliopotea katika mazingira ya kutatanisha na wazazi na walezi wao hawakupatiwa maelezo ya kutosha. Shule kama hizi zilikuwa zinaongozwa na kuendeshwa na Makanisa nchini Canada. Tume ya Haki na Upatanisho wa Kitaifa nchini Canada inasema kuna zaidi ya wanafunzi 4, 100 waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.

“Kamloops Indian Residential School” ni kati ya shule kubwa nchini Canada iliyokuwa inaongozwa na Kanisa Katoliki, ikiwa na wanafunzi zaidi ya 500 kabla ya Serikali kuanza kuingoza kunako mwaka 1969. Shule hizi kwa ajili ya wazawa nchini Canada zilipelekea mauaji ya kimbari. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini”, 6 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba, anafuatilia kwa uchungu mkubwa habari zinazokuja kutoka nchini Canada.

Hii ni baada ya kugunduliwa kwa masalia ya wanafunzi 215 kutoka katika shule ya “Kamloops Indian Residential School” waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii, kujiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada na watu wa Mungu nchini Canada katika ujumla wao, kuonesha uwepo wake wa karibu kutokana na habari hizi zinazohuzunisha na kutia simanzi moyoni. Baba Mtakatifu anawahamasisha viongozi wa Serikali na Kidini nchini Canada kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili hatimaye, ukweli uweze kufahamika, na huo uwe ni mwanzo wa mchakato wa upatanisho na uponyaji wa kitaifa. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na tabia ya ukoloni na hata ukoloni wa kiitikadi, kwa kutambua na kuthamini haki msingi za binadamu, tunu na amana  za kitamaduni kwa watu wote wa Mungu nchini Canada. Baba Mtakatifu ameziweka nyoyo za marehemu watoto hao 215 chini ya huruma ya Mungu. Anaiombea Jumuiya ya wazawa nchini Canada ili iweze kupokea changamoto hii kwa moyo wa utulivu.

Papa Canada

 

 

 

07 June 2021, 14:43