Tafuta

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Shirikisho la Shule za Wayesuit Amerika ya Kusini FLASCSI amekazia umuhimu wa elimu shirikishi. Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Shirikisho la Shule za Wayesuit Amerika ya Kusini FLASCSI amekazia umuhimu wa elimu shirikishi. 

Miaka 20 ya Shirikisho la Shule za Wayesuit Amerika ya Kusini!

Papa anakazia mfumo wa elimu: Itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiikolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu duniani unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote, kadiri ya dhamana zao, wanashiriki vyema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana wa kizazi kipya kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Baba Mtakatifu anakazia mfumo wa elimu itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiikolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu duniani unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote, kadiri ya dhamana zao, wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi katika ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa maboresho ya elimu!

Shirika la Wayesuit kwa miaka mingi limezamisha mizizi yake katika sekta ya elimu ili kuwatengenezea vijana wa kizazi kipya mazingira bora zaidi, yatakayowawezesha baada ya masomo yao, kutumia vyema karama na mapaji yao katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wanafunzi wanaohitimu kutoka katika shule, taasisi na vyuo vya elimu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Wayesuit wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini; watu wanaojizatiti katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii. Kila mwanafunzi baada ya kuhitimu masomo yake, anapaswa kuwa ni chombo cha mageuzi, matumaini na mshikamano. Elimu inayotolewa na Wayesuit inalenga pia kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Vijana wanafunzwa jinsi ya kuheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti zao msingi za kidini, kiimani, kitamaduni na kihali. Elimu bora na makini ni silaha madhubuti katika mapambano ya misimamo mikali ya kidini, kiimani na kiitikadi. Elimu bora na makini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na mambo mengine inapania kunogesha mchakato wa upatanisho na Mwenyezi Mungu, binadamu sanjari na kazi ya Uumbaji. Wanafunzi wanahimizwa kuendeleza uwezo, karama na mapaji yao kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao! Ni katika muktadha huu, “Federación Latinoamericana de Colegios de la Compañía de Jesús, (FLACSI) yaani Shirikisho la Shule za Wayesuit Amerika ya Kusini, linaadhimisha kumbukizi ya Miaka XX tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwatumia ujumbe kwa njia ya video, akiwatakia heri na baraka katika maadhimisho haya. Kristo Yesu anawafundisha waja wake, kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano mema na jirani zao pamoja na Kazi ya Uumbaji. Wanatumwa kuwaendea na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huu ni mwaliko wa kujikita katika furaha ya uinjilishaji inayopendeza na kufariji. Ni Injili inayowasukuma waamini kuacha hofu ya usalama wao kivukoni na kuchangamshwa na utume wa kuwasilisha maisha kwa wengine, kwa ajili ya msaada na huduma makini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kuona kwamba, shule zinakuwa ni mahali pa Injili ya ukarimu, mahali pa kuganga na kuponya madonda; mahali ambapo hata maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanaweza kupata nafasi ya kuboresha maisha yao kwa njia ya elimu. Shule ziwe ni mahali pa ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii; mahali ambapo udugu wa kibinadamu unajenga na kudumishwa. Udugu wa kibinadamu ujengwe na kusimikwa katika kanuni maadili na utu wema, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Binadamu wanapaswa kutambua kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe, wao ni familia kubwa ya binadamu wanaopaswa kuheshimiana kama ndugu wamoja!

Baba Mtakatifu anawataka Wayesuit kuhakikisha kwamba, shule zao zinawafundisha vijana wa kizazi kipya kufanya mang’amuzi ya maisha, kwa kupewa nyenzo za kuweza kusoma alama za nyakati na kujisadaka bila ya kujibakiza kama zawadi kwa ajili ya wengine. Watambue ikolojia ya mazingira, uchumi fungamanishi, ustawi, maendeleo na mafao ya jamii. Shule zisaidie kuunda dhamiri nyofu kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kutambua kwamba, vijana kimsingi ni mitume wamisionari kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini katika ulimwengu mamboleo! Mwishoni, anapenda kuwatia shime kusonga mbele katika kunogesha ubora katika sekta ya elimu kwa kukazia zaidi Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education”. Anawashukuru kwa huduma katika sekta ya elimu inayokoleza imani na haki.

Elimu Wayesuit

 

12 June 2021, 07:58