Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani unanogeshwa na kauli mbiu "Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote" Mt 28:20. Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani unanogeshwa na kauli mbiu "Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote" Mt 28:20. 

Papa: Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani 2021 Umuhimu Wake!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani, tarehe 25 Julai 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Bibi, Babu na Wajukuu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20: Hii ni ahadi ya uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anasema, Siku ya Wazee Duniani ni fursa kwa mababu, mabibi na wajukuu wao kudemka kwani maisha yataka matao! Upweke hasi, janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; faraja kutoka kwa vijana na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na waja wake. Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii ili kuweza kuurithisha kwa kizazi kipya pamoja na kuwalinda vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani ili wasijikwae na hatimaye kukengeuka! Wazee hata katika uzee wao, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi kieleweke kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Wazee na vijana wanahitajiana, ili kukamilishana katika hija ya maisha yao na hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake. Baba Mtakatifu anawataka mababu, mabibi na wazee kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono” Yoe 2: 28-32.

Wazee wanahamasishwa kutumia ujuzi, uzoefu na mang’amuzi yao kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa dunia, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu anasema, wazee wengi wana kumbukumbu ya machungu katika maisha, lakini ikumbukwe kwamba, kumbukumbu ni sehemu ya maisha na kama ikutumiwa vyema inaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa haki na ukarimu na kwamba, msingi wa maisha ya kweli ni kumbukumbu! Sala ya wazee ina nguvu kiasi hata cha kuweza kuulinda ulimwengu. Ni maneno yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, hata katika uzee wake anaendelea kusali na kuliombea Kanisa. Huu ni msukumo mpya katika mchakato wa uinjilishaji. Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Tafakari ya Neno la Mungu ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika huduma.

Kwa upande wake, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha wakati wa kuwasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu, Jumanne, tarehe 22 Juni 2021 anasema, Siku ya Wazee Duniani ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na utahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Siku ya Mababu, Mabibi na Wajukuu ni muda wa kuserebuka, kutoa faraja na kuonesha upendo kwa wazee, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu ili kuvunjilia mbali hofu ya maambukizi ya magonjwa kama inavyojitokeza wakati huu wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Upendo na faraja ni tunu msingi katika maisha ya kijamii.

Ni muda kwa waamini kujifunza sanaa ya kupenda na kupendwa na katika muktadha huu, wazee wanaweza kuwa magwiji kwa vijana wa kizazi kipya! Ndoto, Kumbukumbu na Sala ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Wazee wawe ni wadau katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa. Wasaidiwe kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha ya kiroho, wahusishwe kikamilifu na uwepo wao uthaminiwe na Kanisa liwe tayari kuchota hekima na busara kutoka kwa wazee hawa. Wazee wana mang’amuzi, ujuzi, maarifa na uzoefu wa miaka mingi, walisaidie Kanisa kupambana na changamoto mamboleo katika maisha na utume wake! Kwa hakika wazee ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Wazee ni watu muhimu sana katika historia ya binadamu. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani iwe ni fursa ya kuwapenda zaidi, ili hatimaye, kujifunza kutoka kwao kama waalimu, walinzi na warithishaji wa hekima na busara kwa vijana wa kizazi kipya. Mama Kanisa anapenda kuwaambia na kuwahakikishia wazee kwamba, ataendelea kuwa pamoja na wazee hadi ukamilifu wa dahali!

Dr. Vittorio Scelzo, Afisa wa Huduma za Kichungaji kwa Wazee, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Baraza litaendelea kutoa sala, sera na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, Siku ya Wazee Duniani inaadhimishwa kikamilifu. Huu ni mwaliko kwa vijana kuwa tayari kwenda kuwafariji na kuwahudumia wazee hasa wale wanaoishi peke yao. Utume huu unaweza kutekelezwa na Watoto wa Utoto Mtakatifu, Vijana Wakatoliki pamoja na vyama mbalimbali vya kitume kwa upande wa watoto na vijana. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Julai 2021 majira ya Saa 4: 00 Asubuhi kwa Saa za Ulaya ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya wazee. Ibada ya Misa zitakazoadhimishwa sehemu mbalimbali za dunia, walau iwepo Ibada za Misa itakayowashirikisha wazee zaidi. Huduma hii inaweza pia kuendelezwa kwenye nyumba za wazee na hospitalini. Pale ambapo tayari kuna utamaduni kama huu ni kuendelea kuuboresha zaidi. Iwe ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea wazee waliotangulia mbele za haki, wakiwa na tumaini la ufufuko na uzima wa milele!

Kwa upande wake, Monique Bodhuin, Rais wa “Life Ascending International, VMI” Chama cha Kitume kinachokita mizizi yake katika: Urafiki, tasaufi na ushiriki katika shughuli za kijamii anasema, siku hii ni chemchemi ya matumaini kwa wazee wote duniani. Vijana na wajukuu wanapaswa kuwasindikiza na kuwashirikisha wazee furaha, upendo na huruma. Huu ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni unaowajali na kuwaenzi wazee. Watoto na vijana wa kizazi kipya, wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa wazee. Wazee washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua na kuheshimu: utu, heshima na haki zao msingi. Wazee wahamasishwe kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa lijenge madaraja yanayokuwatanisha wazee na vijana wa kizazi kipya!

Naye Mama Elena Liotta ambaye ni kati ya wazee waliofika kushuhudia kuhusu: umuhimu, dhamana na utume wa wazee katika ulimwengu mamboleo unaoonekana kujengeka katika misingi ya uchu wa mali, madaraka na mafanikio ya chapuchapu! Amesema, amezaliwa katika kizazi cha wachapakazi, waliovuja jasho kuijenga Italia kwa sadaka na majitoleo makubwa ili kuwajengea vijana wa kizazi hicho matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wakati wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 wazee wengi wameteseka, wamefariki katika upweke na wengi wao wameachiwa madonda ya kudumu. Umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ni neema, itakayosaidia kukuza na kudumisha kumbukumbu na hatimaye, kuendeleza ndoto ya kuwa na ulimwengu bora zaidi.

Mama Maria Sofia Soli, ametumia fursa hii, kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuanzisha Siku ya Mababu, Mabibi na Wajukuu Duniani, ili kurejesha tena ile nafasi na dhamana na wazee katika jamii. Ni wakati wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, huku wazee wakitekeleza kikamilifu wito wa maisha yao ya uzee. Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuyaangalia maisha kwa jicho la imani, matumaini na mapendo! Ni muda wa kuwasikiliza, kuwajali na kuwathamini vijana wa zamani, ili kunogesha majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wazee wanawapenda na kuwathamini wajukuu wao na kwamba, wangependa kunogesha mahusiano haya kwa kujikita katika ndoto, kumbukumbu na sala. Katika utamaduni ambako watu hawasali tena ni utamaduni ambao wazee si mali kitu! Kanisa na jamii inawahitaji wazee wanaokita maisha yao katika sala, kwa sababu huu ndio wajibu na utume wao! Hiki ni kielelezo cha upendo wa dhati kwa wale wanaowapenda na kuwathamini na kwamba, sala inapyaisha zaidi maisha yao kwa kukutana na jirani zao.

Papa Wazee

 

22 June 2021, 15:24