Tafuta

Tarehe 14 Juni Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani: Kielelezo cha ukarimu na sadaka ya upendo. Tarehe 14 Juni Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani: Kielelezo cha ukarimu na sadaka ya upendo. 

Papa: Siku ya Wachangia Damu Duniani 14 Juni 2021: Ukarimu!

Tarehe 14 Juni, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani. Lengo la maadhimisho haya ni kukuza uelewa kuhusu huduma ya damu salama, kuhamasisha jamii kuchangia damu kwa hiari pamoja na kuwatambua na kuwaenzi watu ambao wamekuwa wakichangia damu kwa hiari kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kuongezewa damu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Afya Duniani, WHO linasema kwamba, upatikanaji wa damu salama ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la huduma bora za afya kwa watu wote lakini pia ni kipengele muhimu katika utendaji kazi wa mifumo ya afya kote duniani. Kila mwaka ifikapo tarehe 14 Juni, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani. Lengo la maadhimisho haya ni kukuza uelewa kuhusu huduma ya damu salama, kuhamasisha jamii kuchangia damu kwa hiari pamoja na kuwatambua na kuwaenzi watu ambao wamekuwa wakichangia damu kwa hiari kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kuongezewa damu.

Aidha, Siku ya Wachangia Damu Duniani ni ukumbusho wa siku ya kuzaliwa ya Dr. Karl Landsteiner, ambaye ndiye aliyegundua mfumo wa makundi ya damu ya “A”, “B” na “O”, na alizawadiwa tuzo ya Nobel kutokana na ugunduzi huo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 13 Juni 2021 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Jumatatu tarehe 14 Juni 2021 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza watu wote wanaojitolea kuchangia damu. Anapenda kuwatia shime kusonga mbele kwa ari na mwamko huo kama ushuhuda wa tunu ya ukarimu, sadaka na majitoleo kwa ajili ya huduma kwa jirani.

Wachangia Damu
14 June 2021, 14:33